‘’Ziko changamoto, changamoto hizo sio za Dkt. Samia Suluhu Hassan ni sisi wasaidizi wake, kutokujua kutafsiri maono ya Rais wetu na kutekeleza kwa kasi, huu mradi huyu mkandarasi atamaliza mapema lakini hapatakuwa na umeme kwa sababu ya kusua sua kwa mkandarasi anayejenga laini ya kutoka Tabora kuja hapa, na kwa bahati mbaya mkandarasi huyo ni ETDCO kampuni yetu ya Tanesco, nimeuliza hapa meneja mkuu wa ETDCO yuko wapiwameniambia amenitumia mwakilishi, mimi wziri wa sekta niko hapa yeye yuko Mwanza amenitumia mwakilishi’’. Dkt. Doto Biteko Naibu Waziri mkuu na Waziri wa Nishati
Na. Hamis Ngangari
KIMEUMANA ndivyo unavyoweza kusema baada ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko kugeuka mbogo kwa watendaji walio chini ya wizara yake huku akikemea michezo na tabia za uzembe, kufanya kazi kwa mazoea na kushindwa kutafsiri maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuwatumikia watanzania kwa kasi sawa na anavyotamani rais iwe
Dkt. Biteko ameonyesha kutokuridhishwa na utendaji wa taasisi zilizo chini ya wizara hiyo huku akiagiza kubadilishwa haraka kwa meneja mkuu wa kampuni iliyo chini ya shirika la umeme nchini ETDCO kampuni ambayo inafanya shughuli mbalimbali za ujenzi na usambazaji wa vifaa vya Tanesco
Akiwa katika ukaguzi mradi wa ujenzi wa Kituo cha Kupoza umeme cha Uhuru kilichopo wilayani Urambo mkoani Tabora na ameonyesha kutoridhishwa kwake na kazi ya ujenzi wa laini ya umeme (kV 132) kutoka Tabora hadi Urambo ambayo inatekelezwa na kampuni hiyo tanzu ya TANESCO (ETDCO).
Kazi ya ujenzi wa Kituo cha kupoza umeme cha Uhuru imegawanyika katika sehemu mbili ambapo ujenzi wa kituo cha kupoza umeme unafanywa na kampuni ya TBEA kutoka China ambao wamefikia asilimia 84 ya utekelezaji huku kazi ya ujenzi wa laini ya umeme kutoka Tabora hadi Urambo (km 115) ikifanywa na kampuni ya ETDCO ambao wamefikia asilimia 10 tu ya utekelezaji.
Kufuatia hali ya kusuasua kwa ujenzi wa laini hiyo, Dkt. Biteko ameiagiza Bodi ya TANESCO kumwondoa Meneja Mkuu wa ETDCO Muhamed Abdallah ambaye ameonekana kutotoa kipaumbele katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati inayosimamiwa na Kampuni hiyo.
“Tarehe 17 Septemba, 2023 nilimtuma Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga kuja kukagua mradi huu ambaye aliwapa maelekezo ya kukamilisha mradi, pia nilimtuma aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya TANESCO, Mej.Jen. Paul Simuli kuja kukagua mradi huu 17 Desemba 2023 naye alitoa maelekezo ambayo hayajatekelezwa, hatari iliyopo hapa ni kuwa TBEA atakamilisha kazi mapema mwezi Juni lakini umeme bado hautapatikana kwenye kituo kwa sababu laini ya umeme itakuwa haijakamilika.” Amesema Dkt. Biteko
Dkt. Biteko ameongeza kuwa, kutokukamilika kwa wakati kwa laini ya umeme kutoka Tabora hadi Urambo kutapelekea Serikali kumlipa TBEA gharama ya kuwepo eneo la mradi bila kazi ambayo ni asilimia 0.2 ya gharama za mradi na hii ikiwa ni hasara kwa Serikali.
Amesema kuwa, kampuni ya TBEA na ETDCO zote zililipwa malipo ya awali ya utekelezaji wa kazi kwa asilimia 50 lakini ETDCO anatekeleza kazi kwa kusuasua huku TBEA akifanya kazi kwa wakati.
Kuhusu miradi ya umeme mkoani Tabora, Dkt. Biteko amesema kuwa, mkoa huo utaiunganisha mikoa miwili kwenye gridi ya Taifa kwani umeme kutoka mkoani humo utaenda pia Kigoma na Katavi kupitia kituo hicho cha Uhuru na baadaye kusafirishwa kwenda kituo cha kupoza umeme Nguruka na kwenda kituo cha Kidahwe mkoani Kigoma ili kuwaunganisha wananchi na gridi ya Taifa.
Ameongeza kuwa, Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan pia ametoa fedha kujenga laini ya umeme kutoka Tabora- Ipole-Mlele hadi Mpanda Mjini kwa urefu wa kilometa 393 na kwamba ujenzi wa kituo cha kupoza umeme Ipole umefikia asilimai 89, Mlele umefikia asilimia 87 na Mpanda Mjini umefikia asilimia 90 huku laini ya umeme ujenzi wake ukifikia asilimia 47.
Dkt.Biteko amesema nia ya Serikali ni kuwapa wananchi umeme na siyo maneno na ndiyo maana utekelezaji wa miradi mbalimbali inaendelea ikiwemo mradi wa Julius Nyerere ambao tayari mashine moja imeshaanza kuzalisha megawati 235 huku mashine nyingine ikikamilishwa mwezi huu ili kuingiza megawati 235 nyingine na hivyo kumaliza kabisa changamoto ya upungufu wa umeme.
Vilevile, Dkt. Biteko ameitaka kampuni ya ETDCO kujitathmini katika utekelezaji wa miradi yake kutokana na mingi kusuasua pamoja na kutathmini utendaji wake wa kazi ndani ya Menejimenti ambao si wa kuridhisha.
Vilevile amewataka Watendaji wanaoona kwamba hawawezi kuishi na kutafsiri maono ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kujiondoa kwenye nafasi zao wenyewe ili kutorudisha nyuma juhudi za Serikali kutatua chanagmoto za Wananchi.
Kwa upande wake, Mbunge wa Urambo, Mhe. Magreth Sitta amemshukuru Dkt. Biteko kwa kukagua mradi huo na kutoa maelekezo ambayo yatawezesha mradi huo kukamilika kwa wakati na kuondoa changamoto ya kukatika mara kwa mara ya umeme.
Aidha. Amemshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kupelekea fedha za utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme, maji, afya n.k katika Jimbo la Urambo