Na WMJJWM- Dodoma
Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kushirikiana na Taasisi nyingine za Serikali pamoja na wadau inaandaa mfumo wa rufaa kwa wahamaji walio katika mazingira hatarishi nchini utakaosaidia kutoa huduma kwa makundi maalum wakiwemo watoto.
Hayo yamebainika wakati wa kikao kilichowakutanisha Wakurugenzi na Makamishna kutoka Wizara za Kisekta na wadau mbalimbali kujadili uandaaji wa mfumo wa rufaa kwa wahamaji walio katika mazingira hatari Machi 27, 2024 jijini Dodoma.
Akifungua kikao hicho Kamishna wa Ustawi wa Jamii kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Nandera Mhando amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua mchango unaotolewa na wadau katika kuhudumia makundi yenye uhitaji wakiwemo wahamaji walio katika mazingira hatarishi hivyo kama Wizara yenye dhamana na makundi maalum wakiwemo watoto imeona ni vema kuwa na mfumo wa rufaa kwa wahamaji walio katika mazingira hatarishi hususan watoto ili kuhakikisha kuwa kundi hili nalo linapata huduma stahiki kwa wakati.
Ameongeza, kuwepo kwa mfumo huo kutasaidia ushirikiano kati ya Wizara za Kisekta,Taasisi za Serikali na wadau katika kutoa huduma kwa wahamaji walio katika mazingira hatarishi ambapo huduma hizo zinajumuisha kuwaunganisha na nchi zao watoto waliovuka mipaka na kuingia Tanzania ikiwa ni pamoja na wale walio katika mkinzano na Sheria kwa kosa la kuingia nchini kinyume na Sheria.
“Kikao hiki ni cha muhimu sana kwetu na niombe tukipe uzito mkubwa kwani tutakayo yajadili leo yatatuwezesha kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi zetu za Serikali na wadau katika kuwapatia huduma wahamaji ambao ni walengwa wa mfumo huu ambapo baadhi yao ni watoto waliokinzana na Sheria kwa kuingia nchini kinyume cha Sheria, watoto waliotengana na wazazi wao na wale waliovuka mipaka bila ya kuwa na uangalizi” amesema Dkt. Nandera
Kamishna Dkt. Nandera amesisitiza kwamba kuna umuhimu wa kuwa na mfumo wenye uratibu mzuri utakaosaidia wadau wote kutimiza wajibu wao kwa wakati pamoja na kuboresha upatikanaji wa huduma kwa walengwa. Hivyo amewaomba wadau kutoa michango na maoni ya kitalam yatakayowezesha kuwa na mfumo mzuri wa rufaa utakaosaidia upatikanaji wa huduma kwa wahamaji walio katika mazingira hatarishi hapa nchini.
Kwa upande wake Afisa Mwandamizi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Honesta Ngolly ameshauri kamati ya uandaaji mfumo huo kuhakikisha wanatoa elimu kwa watumiaji na wadau wengine ili kuwa na mfumo utakaojumuisha walengwa wote ili kuondokana na changamoto katika kupata rufaa kwa wahamaji walio katika mazingira hatarishi nchini.
Naye Afisa Programu Msaidizi kutoka Shirika la IOM Ken Heriel amesema Shirika hilo limeamua kushirikiana na Serikali kuwa na mfumo utakaosaidia kuwa na namna bora ya utoaji huduma za rufaa kwa wahamaji waliokatika mazingira hatari ili kuwasadia kupata huduma muhimu wakati wakiwa katika njia ya uhamiaji.