
Wenyeviti wa Serikali za Mitaa Wilaya ya Kigamboni wameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kwa juhudi na kasi kubwa inayoendelea ya Kusambaza huduma ya maji katika Wilaya ya Kigamboni.

Wameyasema hayo wakati wa ziara ya muendelezo wa mafunzo kwa Viongozi wa Mitaa juu ya shughuli mbalimbali zinazofanywa na DAWASA katika Wilaya ya Kigamboni ambapo wametembelea mradi wa uchimbaji Visima virefu vya Kimbiji pamoja na Mradi wa kusogeza huduma Mtaa wa Kigogo.

Mwenyekiti wa mtaa wa Kigogo Ndugu Ramadhani Mohammed amesema utekelezaji wa mradi huo kupelekewa mradi wa usambazaji Maji wenye umbali wa Kilomita zaidi ya 23.

“Tunashukuru sana DAWASA Kwa ziara hii ya viongozi, hakika inatuweka karibu zaidi na tumepata kujua ni maeneo gani ya kushirikiana baina ya Wenyeviti na DAWASA, Elimu hii tunarudi nayo kwa wananchi wetu mtaani na kuwaelimisha maendeleo ya miradi inayoendelea katika kuwafikishia huduma Wananchi.” ameeleza ndugu Mohammed.
Mkurugenzi wa Miradi DAWASA, Mhandisi Ramadhani Mtindasi ameeleza kuwa kwa sasa mradi wa visima vya Kimbiji unazalisha maji mengi kupita mahitaji ya Wilaya ya Kigamboni na hivyo kutoa fursa ya kuyasambaza maeneo mengi zaidi.

“Mradi huu umekamilika na Wananchi takribani 8020 wanapata huduma na kazi kubwa tunayoendelea nayo ni kusambaza huduma ya maji katika Mitaa mbalimbali Wilaya ya Kigamboni, lengo likiwa kila mwananchi apate huduma ya maji” aliongeza Mhandisi Mtindasi

Mhandisi Mtindasi ameongeza kwa kuwaomba wenyeviti Serikali za Mitaa kuwa mabalozi kuhamasisha Wananchi wanajitokeza kwa wingi kuunganishwa huduma ya maji kwani Wilaya ya Kigamboni ina maji ya kutosha.

Vikao kazi kati ya DAWASA na Wenyeviti wa Serikali za Mitaa na DAWASA inaongozwa na kauli mbiu isemayo Serikali za Mitaa chachu ya huduma endelevu za maji



