Kilimanjaro, Hifadhi ya Taifa Kilimajaro (KINAPA) imewekeza nguvu katika matumizi ya gesi asilia ili kutunza mazingira na kuepusha utegemezi wa jamii katika nishati itokanayo na misitu kutoka hifadhini.
Hayo yamebainishwa leo tarehe 06.02.2025 na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Angellah Nyaki (Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro) wakati akisoma taarifa ya utekelezaji wa shughuli za uhifadhi na utalii za hifadhi hiyo wakati wa ziara ya kikazi ya Kamishna wa Uhifadhi TANAPA, Musa Nassoro Kuji.
“Hifadhi imejikita katika kutekeleza miradi ya utunzaji wa mazingira ili kuepuka utegemezi wa jamii kwenye nishati kutoka hifadhini. Miradi hiyo ni ugawaji wa majiko banifu yatakayotumia biogas na gesi ya kawaida” alisema Kamishna Nyaki.“Katika mwaka wa fedha 2024/2025-2025/2026 hifadhi imepanga kutekeleza miradi ya mahusiano ya jamii yenye thamani ya jumla ya shillingi Millioni 369.9 ambapo miradi ya utunzaji wa mazingira ina thamani ya jumla ya shillingi Millioni 222” aliongeza Kamishna Nyaki.
Aidha, Kamishna Nyaki aliongeza kuwa maeneo ya hifadhi ambayo yaliyokuwa wazi bila ya kuwa na miti kwa sasa yamefunga kutokana na jitahada za kurejesha uoto wa asili ambapo kati ya mwaka 2021 hadi 2024, jumla ya miti ya asili 238,958 imeoteshwa na hifadhi kwenye eneo la hekta 352.
Programu hiyo ni endelevu kwani inachangia kwa kiasi kikubwa kutunza barafu iliyopo katika Mlima Kilimanjaro.
Pia, Kamishna Nyaki aliongeza kuwa juhudi zinazofanywa katika utunzaji wa Mazingira zinapelekea hifadhi hiyo kuwa na uwezo wa kuanzisha mazao mapya ya utalii ambapo hifadhi imejipanga kuongeza mapato kwa kukusanya bilioni 110 kwa mwaka ujao wa fedha wa 2025/2026 kupitia zao jipya la “Scenic Flight” pamoja na kufungua njia ya Kidia itakayokuwa maalum zaidi kwa watu maarufu kupanda Mlima Kilimanjaro.
Kamishna wa Uhifadhi TANAPA, Musa Nassoro Kuji katika kikao kazi chake na Maafisa na Askari wa Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro aliipongeza hifadhi hiyo kwa juhudi kubwa za kuhifadhi mazingira kwa niaba ya Watanzania na kubuni mazao mapya ya utalii ili kuongeza mapato yatokanayo na shughuli za utalii.
“TANAPA tumeweka ahadi ya kutoka kwenye makusanyo ya mabilioni kwenda kwenye makusanyo ya trilioni na ili azma hiyo iweze kutokea, tunapaswa kuwa na utendaji kazi wa kujitoa, na weledi wa hali ya juu huku tukiishi kwenye viapo vyetu” alisema Kamishna Kuji.“Nipongeze juhudi kubwa zinazofanywa na Maafisa na Askari wa Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro na Shirika zima kwani kazi inaonekana na kuthibitisha kauli mbiu ya “TANAPA Next Level” na “TANAPA Nyumbani kwa Tuzo. Ni dhahiri kuwa utendaji kazi wenu makini na wa kujituma umepelekea hifadhi hii kupata tuzo ya kimataifa ya kuwa Kivutio Bora cha Utalii barani Africa kwa mwaka 2024 (Africa’s Leading Tourist Attraction 2024). Tuzo hiyo imeliletea heshima Shirika na Nchi kwa ujumla” aliongeza Kamishna Kuji.
Naye, Askari Uhifadhi Daraja la Pili, Abdillah Kondo kwa niaba ya watumishi wa Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro alimshukuru Kamishna wa Uhifadhi Musa Nassoro Kuji kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuwatembelea uwandani, kuongea nao na kuwasikiliza kwani ni ishara ya kuthamini kazi zinazofanywa na Maafisa na Askari hao.
“Afande Kamishna wewe ni mfano wa uongozi unaoacha alama nzuri kwani tumekuona ukifanya vikao kazi na wapiganaji wako katika kila Hifadhi na hivyo tuna kila sababu ya kukupongeza wewe kwa kazi hii. Sisi askari kwa ujumla tunajisikia faraja sana kukutana na kuzungumza na wewe na kwa ujumla wetu tukuahidi kuchapa kazi na tunakuombea Mungu akuongoze katika kazi zako”. Alisema Abdillah.
