USAJILI wa mchezaji wa kigeni ukifanywa vizuri huibua mijadala mingi yenye kila sababu ya kumfikirisha vilivyo shabiki wa timu zetu na Taifa Stars. Udhaifu wa wachezaji wetu wazalendo huanikwa hadharani.
Pengine hata udhaifu wa ufundishaji uliotumika mpaka wachezaji wetu wakafikia hadhi ya kuchezea timu za Ligi Kuu na wenyewe huonekana dhahiri kabisa. Pascal Wawa alifikia hatua ya kucheza mechi kama vile yupo mazoezini, mara kwa mara akijiamini na kusogea na mpira mpaka mbele zaidi ya mistari wa katikati ya uwanja.
Huyo Pascal Wawa ni beki ambaye hata Timu ya Taifa ya Ivory Coast walikuwa wakimuacha. Nakukumbusha tu, katika ubora wake wakati huo Pascal Wawa alikuwa anaweza kuwa jeshi la kukodi la Taifa Stars katika zile mechi za kutafuta nafasi za kushiriki CHAN, AFCON na hata Kombe la Dunia.
Wakati huo, Azam ilisajili beki imara kutoka El Merreikh ya Sudan na wakati huo huo ilichokifanya kilikuwa ni kutuonyesha mashabiki na wadau, ni kwa jinsi gani mchezaji huyo wa kigeni anaweza hata kuvaa jezi ya Taifa Stars.
Watazame wachezaji wengi tu wanaokipiga Ligi Kuu ambao kucheza ndani ya Taifa Stars na hii si kwamba tunawadharau wachezaji wa ndani, hapana, ila kuna nyakati lazima ukweli unaweza kubaki ukweli. Mtazame Maxi Nzengeli kiungo anayekuwa karibu na mabeki wawili wa kati na anao pia uwezo wa kucheza kiungo anayekuwa karibu zaidi na mshambuliaji wa kati pamoja na namba kumi.
Ni huyu huyu Nzengeli ambaye hapati namba katika kikosi cha kwanza cha DRC, kwa sababu kuna mafundi wengi wanaofikiriwa kwanza na kocha kabla hajatazamwa yeye. Katika ubora wa usambazaji wa pasi zake, Nzengeli sio mchezaji wa kukosa namba katika kikosi cha kwanza cha Taifa Stars.
Sina nia ya kuwadharau viungo tulionao, kwa kumtazama Nzengeli na ubunifu wake mwingi uwanjani, simuoni kiungo mzalendo mwenye uwezo wa kumpoka namba iwapo angekuwa ni mchezaji mwenye sifa za kuivaa jezi ya Taifa Stars.
Wakati ule wa Donald Ngoma nilimtazama kwa makini na kuona mfungaji wa magoli mwenye uwezo mkubwa wa kuhangaika katika eneo la mwisho la upokeaji wa pasi kutoka kwa viungo wachezeshaji. Nakumbusha tu, ila Ngoma alikuwa anao utulivu mkubwa akiwa karibu na goli, anajua namna ya kumtazama na kumchambua golikipa.
Sina nia ya kuwadharau wafungaji wazalendo, lakini kwenye uwezo wa kutisha mabeki, unaweza kuwaona hawa wazawa kuna vitu wanavikosa. Mfano John Bocco amepewa nafasi nyingi sana na makocha wa Taifa Stars, ni kipi cha ajabu ambacho ameshakifanya? John Bocco hawezi kupiga chenga kila anapobakia na beki mmoja wa mwisho.
Ni mzito sana kiasi cha kushindwa kuwatisha mabeki wakati wa shambulizi la kushtukiza. Jaribu kwenye akili za kishabiki tu, kumuweka Nzengeli pembeni ya Mbwana Samatta na Simon Msuva, kwenye mechi ngumu ya Taifa Stars.
Lakini kocha wa timu ya DRC anao wafungaji wengine ambao anawapa kwanza kipaumbele, ni wazi kwamba mpaka mchezaji kama Max Nzengeli aweze kuchaguliwa maana yake ni kwamba hao wengine wawe labda ni majeruhi. Ushambuliaji wa Taifa Stars unakuwa butu sana wakati wanapokosekana Mbwana Samatta na Simon Msuva.
Mchezaji wa kiwango cha Nzengeli na mwingine yeyote mwenye hati ya kusafiria ya Tanzania, angekuwa na msaada sana. Sioni kuwa ni dhambi kwa Taifa Stas kuwa na majeshi ya kukodi.
Diego Costa ni Mhispania aliyezaliwa nchini Brazil. Alivaa jezi ya Hispania na kuichezea kwenye Kombe la Dunia. Iwapo kina Morata na wengine wakipata majeraha, kocha Vicente Del Bosque wakati huo alikuwa anao uwezo wa kumtumia tena Diego Costa.
Hispania ambayo ilikuwa tayari kumtumia Diego Costa kwenye mechi kubwa za ushindani imewahi kubeba Kombe la Dunia na ambayo ina misingi mizuri sana ya ukuzaji wa wachezaji, huku Tanzania ambayo bado ipo kwenye michakato ya kuifahamu soka na misingi yake, itakuwa imefanya kosa gani katika kuwashawishi na kuwatumia wachezaji wa kigeni wanaokuja kuchezea timu za Ligi Kuu?