NDOTO ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuongeza idadi ya watalii nchini hadi kufikia milioni tano ifikapo mwaka 2025 na pato la Taifa linalotokana na utalii kufikia Shilingi bilioni sita kwa mwaka, imeshikwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Pindi Chana.
Juni 7, 2022 Rais Dkt. Samia akiwa kwenye Mkutano wa Baraza la Taifa la Biashara, aliiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii kukutana na wadau wa Sekta ya Utalii kujadili mapendekezo ya mageuzi ya sera, sheria, taratibu na kanuni ili kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji katika sekta hiyo ili kufikia lengo la kuongeza watalii wanaotembelea nchini hadi kufikia milioni tano, mwaka 2025 sambamba na mapato yatokanayo ya biashara ya utalii.
Katika kutekeleza maagizo hayo ya Rais Dkt. Samia, Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) ambalo ni muhimili muhimu wa Sekta ya Utalii nchini, limevutia watalii kutoka pande mbalimbali duniani kutembelea Hifadhi za Taifa.
Ukichukua kwa karibu zaidi utaona hadi Aprili 2024, watalii 1,598,608 walitembelea Hifadhi za Taifa. Idadi hiyo ni ongezeko la asilimia 11.4 ikilinganishwa na watalii 1,435,069 waliotembelea Hifadhi za Taifa mwaka wa fedha 2022/2023.
TANAPA imekusanya mapato ya Shilingi 353,441,080,170.15 ambazo ni sawa na ongezeko la asilimia 21.58 ikilinganishwa na mapato ya Shilingi 290,698,543,140.17 zilizokusanywa kwa kipindi kama hicho, mwaka wa fedha 2022/2023. TANAPA chini ya miongozo na maelekezo ya Serikali limeimarisha na kuendeleza miundombinu ya utalii kwa kufungua barabara mpya zenye urefu wa kilometa 694.5 katika Hifadhi ya Taifa Nyerere.
Pia TANAPA imejenga vituo nane vya askari katika Hifadhi za Taifa Nyerere, Mto Ugalla, Burigi-Chato, Ruaha, Ibanda-Kyerwa na Rumanyika[1]Karagwe na pia limejenga nyumba 29 za watumishi katika Hifadhi za Taifa Nyerere, Ruaha, Mkomazi, Mto Ugalla, Gombe na Tarangire.
Katika hilo, TANAPA lmekarabati barabara zenye urefu wa kilomita 3,631 katika Hifadhi za Taifa Arusha, Ziwa Manyara, Katavi, Kilimanjaro, Tarangire, Ruaha, Saadani, Burigi-Chato, Mikumi, Rumanyika-Karagwe, Serengeti na Mkomazi pamoja na njia za kupandia milima zenye urefu wa kilomita 157.
TANAPA pia imekarabati viwanja vya ndege 12 katika Hifadhi za Taifa Nyerere, Serengeti, Katavi, Tarangire na Mkomazi na pia ujenzi unaendelea wa viwanja vya ndege vinne katika Hifadhi za Taifa; Ruaha vipo viwanja viwili, Mikumi kiwanja kimoja na Nyerere kiwanja kimoja.
Kwa upande mwingine, Hifadhi ya Taifa Serengeti imeendelea kupokea tuzo za Africa’s Leading National Park inayotolewa na World Travel Awards mara tano mfululizo kuanzia Mwaka 2019, 2020, 2021, 2022 na 2023.
Tuzo nyingine ni Best Nature Destination World 2023 inayotolewa na Trip Advisor, Tuzo ya ubora wa kimataifa inayotolewa na European Society for Quality Research (ESQR) mara nne mfululizo kuanzia mwaka 2020 (Gold category), 2021 (Platinum category ), 2022 ( D i a m o n d category) na mara nyingine tena 2023 (Diamond category) na tuzo ya Top Attractions kwa Afrika 2023 iliyotolewa na Trip Advisor kwa Hifadhi za Taifa Serengeti na Tarangire.
TANAPA pia inatekeleza miradi 108 ya ujirani mwema katika sekta za elimu, afya, usalama, maji na barabara yenye thamani ya Shilingi bil. 40.7 ambapo Shilingi bil. 36.5 ni kupitia ufadhili wa mradi wa Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW) na Shilingi bil. 4.2 kupitia fedha za miradi ya maendeleo.
TANAPA imewezesha uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi kwa vijiji 74 vinavyopakana na Hifadhi za Taifa Serengeti ni mipango 37, Ziwa Manyara mipango 25 na Tarangire mipango 12.
Ukitazama TANAPA imewezesha vikundi 166 vya kiuchumi vya jamii katika Wilaya za Chamwino ni tisa, Iringa 25, Kilolo tisa, Kilombero 56, Kilosa 15, Mvomero 10, Morogoro 26, Meatu vitatu, Itilima tisa na Busega vinne