RAIS wa DRC, Felix Tshisekedi, hatahudhuria mkutano usio wa kawaida wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ulioitishwa na Rais William Ruto wa Kenya kuhusu mgogoro wa kiusalama mashariki mwa jimbo la Kivu Kaskazini.
“Rais Felix Tshisekedi anafuatilia kwa karibu matukio yanayoendelea mashariki mwa nchi. Hata hivyo, hana mipango ya kuhudhuria mkutano ulioitishwa na Rais William Ruto,” anasema Giscard Kusema, Naibu Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano katika Ofisi ya Rais.
Ndicho kinachotukia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC)? Mauaji. Kile kinachotukia nchini humo kwa sasa kinamsikitisha kila mmoja, kwani kimewaacha wakazi wa Mashariki mwa nchi hiyo katika hali tete.
Waasi wanaonekana kukaribia kuudhibiti moja kwa moja mji muhimu wa Goma mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kufuatia ripoti kwamba wameuteka uwanja wake wa ndege.
Serikali ya Congo imesisitiza kuwa bado inaudhibiti huku mapigano katika baadhi ya maeneo ya mji huo yakiendelea. Maghala yenye chakula na vifaa vya matibabu yameporwa, mashirika ya misaada yanasema.
Mapigano kati ya waasi wa M23 na jeshi na washirika wake yamesababisha hospitali kuzidiwa na majeruhi na miili iliyolala mitaani, kulingana na Umoja wa Mataifa.
Kuongezeka kwa hasira kuhusu mashambulizi ya waasi kulisababisha waandamanaji kulenga balozi za kigeni katika mji mkuu, Kinshasa. Wito wa mazungumzo ya amani kukomesha mapigano unazidi kuongezeka.
Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wameelezwa jinsi ushindani wa uchimbaji kupita kiasi na biashara ya maliasili huko Mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC unavyozidi kuchochea mapigano kwenye eneo hilo, madini kama vile dhahabu na Koltani.
Biashara kutoka eneo la Rubaya linalokadiriwa kuchangia zaidi ya asilimia 15 ya uzalishaji wa madini ya Tantalum, inaipatia M23 dola 300,000 kila mwezi. Hii inatia hofu na lazima ikomeshwe.
Kuna athari nyingi huko na moja ni zitokanazo na janga la kibinadamu hivi sasa Mashariki mwa nchi; Pili, ushiriki wa wanawake kwenye michakato ya kisiasa na amani; na Tatu, umuhimu wa kuchukua hatua mahsusi kulinda raia na wanawake.
Janga la kibinadamu nchini DRC limeathiri vibaya wanawake, wasichana na watoto likiwa viwango vikubwa vya wakimbizi wa ndani, ongezeko la ukosefu wa usalama na uhaba wa chakula.
Zaidi ya hapo ni ongezeko la ukatili wa kingono na kijinsia pamoja na ndoa za lazima kwa watoto wa kike na watoto hao kujikuta wanalazimika kujitumbukiza kwenye biashara ya ngono ili kujikimu kimaisha.
Nchi jirani ya Rwanda imeshutumiwa kwa kuunga mkono kundi la M23 linaloongozwa na Watutsi huku likipiga hatua haraka katika miezi ya hivi karibuni katika eneo hilo lenye utajiri mkubwa wa madini.
Mji wa Goma ulio kando ya ziwa, kwenye mpaka na Rwanda, ni kitovu muhimu cha usafiri na biashara karibu na vyanzo vikubwa vya madini ambayo ni muhimu katika utengenezaji wa simu za mkononi miongoni mwa mambo mengine.
Kufuatia mkutano wa Jumanne, Umoja wa Afrika (AU) ulitoa wito kwa M23 kuweka chini silaha zake.
Kamishna wa amani na usalama wa AU, Bankole Adeoye, alilaani vurugu za M23 na vikosi vingine vyote hasi na anatoa wito wa kuheshimiwa kikamilifu uhuru wa DR Congo, umoja na uadilifu wa eneo.
Wanadiplomasia walipokuwa wakijadili hali hiyo, waasi hao walionekana kupata nguvu huko Goma.
“Wamechukua udhibiti wa uwanja wa ndege, wapiganaji wa M23 wapo,” chanzo cha usalama kiliambia shirika la habari la AFP.
“Zaidi ya wanajeshi 1,200 wa Congo wamejisalimisha na wamezuiliwa katika (kambi ya Umoja wa Mataifa) kwenye uwanja wa ndege.”
Mapema Jumanne, Adelheid Marschang, mratibu wa dharura wa Shirika la Afya Ulimwenguni kwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo alisema kuwepo kwa “mamia ya watu hospitalini, wengi wamelazwa wakiwa na majeraha ya risasi”.
Wakizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC) imesema hospitali yake mjini Goma imepokea zaidi ya majeruhi 100 katika muda wa saa 24 pekee, idadi ambayo ilipokea awali kwa muda wa mwezi mmoja.
Ilisema kuwa hali hii iliwalazimu wafanyakazi wake kugeuza maegesho ya gari ya hospitali kuwa kitengo cha kufanya tathmini ya awali ya wagonjwa au majeruhi.
Utumiaji wa silaha nzito za kivita katika maeneo yenye watu wengi husababisha majeraha makubwa, haswa miongoni mwa watoto, iliongeza.
Mjini Kinshasa, umati wa watu wenye hasira ulilenga balozi za Ufaransa, Kenya na Uganda miongoni mwa nyingine. Walivamia barabarani, wakichoma magurudumu na kusababisha msongamano wa magari.