JUZI Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alisema kuwa Mpango Mahsusi wa Kitaifa kuhusu Nishati (National Energy Compact) uliozinduliwa unalenga kuiwezeseha Tanzania kuunganisha umeme kwa kaya milioni 8.3 zaidi ifikapo mwaka 2030.
Rais Dkt. Samia aliyasema hayo wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Afrika kuhusu Nishati uliofanyika kwa muda wa siku mbili katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere, Dar es Salaam na kumalizika juzi.
Tanzania ilikuwa mwenyeji wa mkutano huo uliohudhuriwa na Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka Burundi, Botswana, Congo, Comoros, Djibouti, Ethiopia, Gabon, Ghana, Guinea Bissau, Kenya, Lesotho, Liberia, Libya, Madagascar, Malawi, Mauritania, Nigeria, Sierra Leone, Somalia na Zambia.
Vile vile, mkutano huo ulihudhuriwa na Wawakilishi wa Wakuu wa Nchi na Serikali, Wakuu wa Mashirika ya Fedha ya Kimataifa, Mashirika ya Kimataifa, Sekta Binafsi na Asasi za Kiraia kwa lengo la kuongeza kasi ya usambazaji umeme barani Afrika ili kuwaunganisha watu milioni 300 na umeme katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Rais Dkt. Samia alisema kuwa kwa kutoa kipaumbele katika upatikanaji wa nishati ya umeme, mkutano huo ulioandaliwa kwa ushirikiano na Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika utawezesha kuleta mageuzi ya kiuchumi, kukua kwa viwanda, kupunguza umaskini na kuimarisha ustawi wa watu.
Mkutano huo ulifanikiwa kupata ahadi za ufadhili wa Dola za Marekani Bilioni 40 kutoka Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika kwa ajili ya kuwezesha usambazaji wa umeme barani Afrika. Aidha, jumla ya nchi za Afrika 12 zimeingia kwenye Mipango Mahsusi wa Kitaifa kuhusu Nishati.
Rais Dkt. Samia amesema kuwa kupitia Mpango Mahsusi kuhusu Nishati, Tanzania inakusudia kuvutia mitaji na uwekezaji zaidi itakayowezesha kuongeza uzalishaji wa umeme nchini na kukukamilisha kuunganisha Mtandao wa Umeme wa Tanzania na nchi jirani ili kuwezesha biashara ya kuuza na kununua nishati hiyo.
Mpango huo utawezesha Serikali kukamilisha usambazaji umeme katika Vitongoji vyote 64,359 nchini ifikapo 2030. Vilevile, Mpango huo utapandisha kiwango cha uunganishaji wa umeme kutoka 46% ya sasa hadi kufikia 75%.
Kwetu Rais Dkt. Samia ambaye amekuwa kinara wa matumizi ya nishati safi ya kupikia, alifurahisha wengi kwa kuweka bayana kuwa mpango huo wa nishati pia utasaidia kuongeza upatikanaji wa nishati safi ya kupikia, ikiwemo gesi asilia na majiko banifu.
Kila la kheri Rais Dkt. Samia katika mpango mkakati huo na tunaamini kwa dhati kabisa utafanikiwa katika hili, sisi tutaendelea kukuunga mkono ili utimize hili kwa Watanzania.