Wakati Mkutano wa Mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika ujulikanao kama Mission 300, ukiwa umeanza jana, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa ‘kuishusha pumzi’ Afrika pale atakapounguruma kwenye mkutano huo leo Rais Dkt. Samia ambaye amejitwisha zigo la kuipigania nishati safi, anatarajiwa kusikilizwa na wengi haswa kina mama wa Afrika, ambao wengi wana matarajio makubwa naye ya kuwasemea juu ya adha wanazopata kutokana na ukosefu wa nishati safi.
Akiwa ameibeba ajenda ya nishati salama mkononi mwake, Rais Dk. Samia amevunja na kuandika rekodi ya aina yake kwa kuwa Rais wa kwanza nchini aliyewahi kupokea idadi kubwa ya wakuu wa nchi 25 kujai kwa pamoja nchini.
Nchi ambao wakuu wake wamethibitisha kushiriki ni Algeria, Comoro, Liberia, Lesotho, Botswana, Kenya, Ghana, Gabon, Sierra Leone, Ethiopia, Sudan, Malawi, Zambia, Somalia, Guine Bisau, Burundi, Mauritania, Kongo Brazzaville, Madagascar, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Libya, Nigeria, Djibouti na Gabon.
Wakati akizungumzia kwa kina mkutano huo, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt.Doto Biteko alisema, utakuwa ni fursa kubwa sana kwa Watanzania.
“Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa sana ya kuitangaza Tanzania kimataifa, hii imepeleka taasisi za kimataifa, kampuni na wawekezaji kuona Tanzania kuwa ni sehemu sahihi ya kufanya biashara na uwekezaji na mfano halisi ni Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo Afrika kuichagua Tanzania kufanya mkutano huu mkubwa wa kimataifa utakahudhuriwa viongozi kitoka nchi 54 barani Afrika.” Amesema Dkt. Biteko
Ameongeza kuwa, sababu nyingine kubwa ya Tanzania kuchaguliwa kuwa mwenyeji wa Mkutano huo ni mafanikio yaliyofikiwa katika sekta ya nishati ikiwa ni pamoja na kupeleka umeme kwa wananchi suala linaloendanana Ajenda ya mkutano huo ya kuharakisha kupeleka umeme kwa wananchi milioni 300 barani Afrika ifikapo 2030 kati ya watu milioni 685 ambao bado hawana umeme.
“Taifa limepiga hatua kubwa katika Sekta ya Nishati, tunamshukuru Rais kwa msukumo mkubwa anaotoa katika Sekta ya Nishati, taifa lina umeme wa kutosha na wa ziada, uzalishaji sasa umepanda kutoka megawati 1470 hadi megawati takriban 3,077.” Amesema upatikanaji wa umeme barani Afrika kwa sehemu kubwa uko chini ya asilimia 50 lakini Tanzania imepiga hatua kubwana ipo kwenye asilimia zaidi ya 78.
Akiongeza kuhusu mafanikio ya Sekta ya Nishati, Dkt.Biteko amesema vijiji vyote 12,318 Tanzania sasa vimesambaziwa umeme na tathmini iliyofanywa na Benki ya Dunia barani Afrika mwaka jana imeonesha kuwa Tanzania iliongoza kwa kusambazia wananchi umeme vijijini . Dkt. Biteko ameeleza kuwa, baada ya umeme kufika kwenye vijiji vyote sasa kasi inaelekea kwenye vitongoji ambapo katika vitongoji 64,000 nchini, vitongoji takriban 36,000 vimepelekewa umeme.
Ametaja faida za mkutano wa M300 kwa Tanzania kuwa ni pamoja na kuongeza fursa za kupata fedha za kuendelea miradi mbalimbali, kuongeza fursa za uwekezaji, kupata uzoefu kutoka kwa waliofanikiwa zaidi kwenye sekta ya nishati na kuongeza heshima ya nchi kimataifa.
Ameongeza kuwa faida nyingine ni kuharakisha upatikanaji umeme nchini ambapo kiasi cha wananchi watakaounganishiwa umeme kupitia M300 ni milioni 8.3 ifikapo 2030 na hivyo kuifanya Tanzania kuunganisha wateja milioni 13.5 kufikia 2030 Kutoka milioni 5.2 ya sasa.