KATIBU Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Mweli amekabidhi rasmi Mradi wa Kituo cha Uhaulishaji Teknolojia (Lot 1&3) kwa Wakala wa Taifa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ikiwa ni sehemu ya Kituo Mahiri cha Usimamizi wa Mazao ya Nafaka kupitia Mradi wa Kudhibiti Sumukuvu nchini (TANIPAC) baada ya kuvuna. Hafla hiyo imefanyika mwishoni mwa wiki huko Mtanana Wilayani Kongwa Mkoani Dodoma ambapo Katibu Mkuu Mweli ameipongeza timu ya usimamizi wa mradi huo tangu kuanza kwa ujenzi hadi sasa.
“Kituo hiki kinakwenda kumnufaisha mkulima, kutengeneza ajira na ndani yake tumetengeneza kituo maalumu kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa vijana na wanawake kwenye teknolojia mbalimbali zilizopo kwenye mnyororo wa thamani wa mazao yetu ya nafaka,” amesema Mweli.
Sambamba na hilo, amesema wizara inaendelea na utekelezaji wa ajenda 10/30 ambapo moja ya mikakati ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2030 Tanzania iwezekuhifadhi angalau tani million 3 za chakula, huku kupitia kituo hicho kinakwenda kuhifadhi karibu tani 20,000.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakala wa Taifa Hifadhi ya Chakula (NFRA), Balozi John Ulanga ameipongeza hatua ya Wizara ya Kilimo kuiamini kwa kuona kwamba NFRA inastahili kupewa kituo hicho cha umahiri ambacho ni cha mfano kwa ukanda wa Afrika Mashariki.
“Tutahakikisha kituo hiki kinaendelea kuwa cha mfano na panaendea kuwa bora zaidi,” amesema Balozi John Ulanga.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa Kituo hicho, Mratibu wa Mradi, Clepin Josephat amesema Wizara ya Kilimo kupitia mradi wa TANIPAC imekamilisha utekelezaji wa ujenzi wa Mradi wa Soko (Lot 1) na Kituo cha Uhaulishaji Teknolojia (Lot 3) ikiwa ni sehemu ya Kituo Mahiri cha Usimamizi wa Mazao ya Nafaka Baada ya Kuvuna na ujenzi huo umegharimu jumla ya kiasi cha shilingi 10,762,683,129.25 na umekamilika kwa asilimia 100