KWA sasa Simba inaonekana kujipata, haswa baada ya kufanya vyema katika Kombe la Shirikisho Afrika na Ligi Kuu, huku wapinzani wake wakionekana kuanza kucheza ‘beats’ za kocha Fadlu Davids.
Kocha wa Simba, Fadlu Davids ameonyesha kujipata kutokana na namna ya upangaji wa kikosi chake cha kwanza kilichompa heshima kubwa katika dakika 270 sawa na mechi tatu za mwisho kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, Ukitazama kwa makini, mechi hizo ziliipa Simba pointi zilizoivusha kwenda robo fainali ikiwa ni mara ya sita inafanya hivyo kwenye michuano ya CAF kati ya misimu saba kuanzia 2018- 2019.
Katika mechi hizo, Simba imecheza mechi ngumu katika mataifa matatu tofauti, Tunisia dhidi ya CS Sfaxien, Angola dhidi ya Bravos do Maquis na nyumbani Tanzania dhidi ya CS Constantine, timu hiyo ilikusanya pointi saba ikishinda mechi mbili na sare moja.
Haijapoteza huku ikifunga mabao manne na kuruhusu moja ikiwa na clean sheet mbili, huku ikimaliza kinara wa Kundi A. Fadlu raia wa Afrika Kusini, ni wazi kile ambacho alikuwa akikitengeneza kwa miezi mitano tangu akabidhiwe kikosi hicho sasa ni kama amekipata na anatamba nacho.
Katika michezo hizo tatu mfululizo, kikosi chake cha kwanza kilikuwa hivi; Moussa Camara, Shomary Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Che Malone Fondoh, Abdulrazack Hamza, Yusuph Kagoma, Elie Mpanzu, Fabrice Ngoma, Leonel Ateba, Jean Charles Ahoua na Kibu Denis.
Simba imeruhusu bao moja tu ambalo ilikuwa Januari 12 wakiwa Angola ambako walitoa sare ya bao 1-1 na ilikuwa ni baada ya Che Malone kufanya makosa, nyavu zao hazikuguswa wakiwa nyumbani, Januari 19 dhidi ya Constantine na hata walipokuwa ugenini pia, Januari 5 huko Tunisia dhidi ya CS Sfaxien.
Camara akiwa golini, amefanya kazi kubwa akisaidiwa na Kapombe, Tshabalala, Che Malone na Hamza huku mbele yao, Ngoma na Kagoma wakidumisha ulinzi. Vijana hao wa Fadlu, wamefunga mabao manne katika michezo hiyo, ambayo wameonyesha ufanisi mkubwa kwa kushambulia mara 52, changamoto iliyopo bado ni katika utumiaji wa nafasi ambazo wanatengeneza.
“Safari yetu inaendelea na hatujafika mwisho. Tunapambana kwa ajili ya mafanikio makubwa zaidi. Tunahitaji kuendelea kuboresha kila kipengele cha mchezo wetu, kutoka kwa ulinzi hadi kwenye kumalizia nafasi,” alisema Fadlu.