NA MWANDISHI WETU
SIMBA inaendelea kujivunia usajili wa kiungo wake mshambuliaji hatari Elie Mpanzu aliyeanza kuitumikia timu hiyo baada ya usajili wa dirisha dogo, akitokea katika klabu ya As Vita nchini DRC.
Mpanzu alianza kuonyesha cheche zake muda mfupi alipoanza kuichezea timu hiyo ya Msimbazi, akiwa na uwezo mkubwa wa kujenga mashambulizi na kusaidia upachikaji wa mabao.
Hata hivyo Kocha Mkuu wa Simba Fadlu Davis alikuwa akimchezesha kwa muda mfupi akidai kwamba, nyota huyo alihitaji mazoezi ya kutosha ili aweze kurudisha kiwango chake.
Hata hivyo katika muda huo huo mdogo aliopata kuitumikia timu yake hiyo mpya, alionyesha uwezo mkubwa kiasi cha kuwa midomoni mwa mashabiki wa Msimbazi, wakijisifu kuwa usajili wao umeramba dume.
Habari mpya kutoka Simba zinasema kuwa mwamba huyo kadri siku zinavyodizi kwenda, anazidi kuwa ‘Mtamu’ na hasa akionyesha uwezo mkubwa wa kupachika mabao mazoezini, tofauti na wakati wote alipokuwa akiichezea timu hiyo.
Mpanzu aliyeacha simulizi nchini Angola wakati timu yake hiyo ilipoibana Onze Bravos ya Angola ikipata sare ya bao 1-1 iliyoipeleka Simba hatua ya Robo fainali ya michuano ya Kombe la Shirilisho, anatarajia kuonyesha moto wake katika michuano ya ASFA itayoanza Jumamosi.