UTUPA ni aina ya mmea unaopatikana zaidi sehemu zenye baridi hasa nyanda za juu na unastawi sehemu zenye mvua za wastani na nyingi. Mmea huu hauhimili ukame.
Utupa hukua haraka na kusambaa kama usipodhibitiwa, baadhi ya nchi mmea huu umepigwa marufuku kupanda kwa sababu ya kutishia uoto wa asili.
Lakini una matumizi makubwa zaidi ambayo yanaweza kukushangaza na hata kukufurahisha na kama ulikuwa hujui unapaswa kulijua hili.
Kufukuza panya, mchwa
Mmea wa utupa ni moja ya njia za asili zinazotumika kufukuza wanyama na wadudu wa aina mbalimbali wanaoharibu mazao shambani.
Endapo shamba lako limevamiwa na panya wanaochimba ardhini, unaweza kupanda utupa kwa kuchanganya na mazao mengine.
Nafasi
Panda utupa pamoja na mazao mengine kwa umbali wa mita 3 kila upande (3m * 3m) na mpakani mwa shamba.
Baada ya kipindi cha mwaka mmoja shamba halitakuwa na mashimo ya panya wala fuko.
Njia hii pia itakuwezesha kufukuza mchwa, kwenye majumba. Unaweza kuupanda mmea huu kwenye kingo za nyumba na mpakani, kama kuna kichuguu cha mchwa panda miche hii na kichuguu kitakufa baada ya mchwa kuhama.
Kuogeshea mifugo
Unaweza kutumia mmea wa utupa kutengenezea mchanganyiko maalumu, ambao unaweza kuutumia kuogesha mifugo ili kuwakinga na kuwaondolea maradhi ya ngozi.
Namna ya kuandaa
Chukua kilo moja ya majani ya utupa na maji lita 25, loweka kwa saa mbili mpaka tatu au chemsha kwa dakika 30 na lita 27 za maji, chuja kwa kitambaa kisha weka kwenye bomba la kuogeshea mifugo, changanya na sabuni ya unga kidogo ili iweze kunata kwenye mwili wa mnyama, na hapo inakuwa tayari kwa matumizi.
Onyo
Kamwe usitumie kuogeshea nguruwe hawana uwezo wa kuhimili dawa hii kwenye ngozi zao.
Kunyuzia shambani, bustani
Utupa unaweza kutumika kwenye mazao ya aina mbalimbali, hii ikiwa ni njia mojawapo ya kukabiliana na wadudu waharibifu na magonjwa yatokanayo na wadudu hao.
Namna ya kuandaa
Chukua kilo moja ya majani ya utupa na maji lita 5 loweka kwa saa mbili mpaka saa tatu au chemsha kwa dakika thelathini na lita 6 za maji.
Chuja kwa kitambaa kisha weka kwenye bomba na kunyunyuzia shambani au majumbani kwa ajili ya kuua wadudu kama vile mbu, mende, n.k
Kuhifadhi nafaka kwenye ghala
Chukua gramu 100 za unga wa majani ya utupa changanya na mahindi au maharagwe kilo 100, funga vizuri gunia lako na hifadhi kwenye ghala. Dawa hii huwa na nguvu kwa muda wa mwaka mzima.
Matumizi mengine
Endapo utupa utapandwa mchanganyiko na mazao mengine huongeza rutuba ardhini kwa kuongeza kiasi na naitrojeni.
Mbegu zake zinaweza kutumika kama moja ya chanzo cha protini kwenye vyakula vya mifugo, hususani mbuzi.
Tahadhari
Usilishe kwa kiwango kikubwa kwani mbegu za utupa zina chembechembe za sumu zinazoweza kudhuru mifugo endapo zitaliwa kwa wingi.
Unga wa mbegu za utupa, unaweza kusababisha samaki wapooze (paralyze).