RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameendelea kufanya kweli kwa Watanzania baada ya kutoa kiasi cha Sh bilioni 28.1 katika sekta ya mifugo ili kutekeleza mapinduzi makubwa katika mifugo.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Dkt. Ashatu Kijaji, ambaye amesema Serikali ya Awamu ya Sita imetenga fedha Shilingi Bilioni 28.1 kwa mwaka wa fedha wa 2024/2025 kwa ajili ya sekta ya mifugo pekee ili kutekeleza mapinduzi ya sekta hiyo ikiwemo kufanya kampeni ya chanjo ya mifugo ili kuhakikisha mifugo hapa nchini inakuwa na ubora unaohitajika kimataifa.
Waziri Kijaji aliyasema hayo alipokuwa wilayani Mvomero katika Kijiji cha Kambala ambacho ni maalum kwa ajili ya wafugaji ikiwa ni siku ya mwisho ya ziara yake ya kikazi ya siku mbili mkoani Morogoro.
Akifafanua zaidi, Waziri Dkt. Ashatu Kijaji amesema, fedha hizo zimelenga kutoa chanjo za homa ya mapafu ya ng’ombe, ugonjwa wa sotoka ya mbuzi na kondoo na ugonjwa wa kuku wa kideli huku fedha nyingine kutumika kununua pikipiki 700 na vishikwambi 4500 kwa ajili ya maafisa ugani wa mifugo ili kurahisisha utendaji kazi wao hivyo kutimiza maono ya Rais Dkt. Samia.
“Kwa mara ya kwanza ndani ya miaka 60 tangu tupate uhuru, Mama (Dkt. Samia) katupa Shilingi Bilioni 28.1 kwa ajili ya wafugaji tu…” amesema Dkt. Ashatu Kijaji.
Aidha, Waziri amemuagiza Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na uvuvi anayeshughulikia mifugo kufanya utafiti wa haraka ili kujenga kisima au bwawa katika kijiji cha Kambala kabla ya bajeti ya mwaka 2025/2026 ili wafugaji hao kuacha kufuata maji umbali mrefu na kusababisha migogoro baina yao na wakulima.
Katika hatua nyingine, Waziri Ashatu Kijaji amewataka wafugaji kwenda na kasi ya mapinduzi ya sekta hiyo na kutekeleza kwa vitendo utaalamu wanaopewa na maafisa ugani kwani amesema Dkt. Samia Suluhun Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ana dhamira ya dhati ya kuhakikisha mapinduzi ya sekta hiyo yanafanikiwa.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amesema Mkoa wa Morogoro una agenda ya mapinduzi ya mifugo kwa kupata mbegu za mifugo hasa ng’ombe ambao watafugwa kisasa na kuondokana na mkoa kuwa na mifugo mingi isiyo na tija, badala yake kuwa na mifugo michache lakini yenye ubora na inayokidhi masoko ya nje.
Katika hatua nyingine, Malima amesema migogoro mingi baina ya wakulima na wafugaji mkoani humo inasababishwa na ukosefu wa maji, kwani amesema wafugaji wanapotafuta maji kwa ajili ya mifugo yao mara nyingi mifugo yao hupata nafasi ya kula mazao ya wakulima hivyo amemuomba Waziri kuchimba kisima kwenye kijiji cha Kambala ili wananchi wake kupata maji ya uhakika kwa ajili ya mifugo yao.
Naye Askofu Jacob Mameo wa Kanisa la Kilutheri la Kiinjili Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Morogoro amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwani ana mchango chanya katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya mifugo kwani amesema migogoro iliyokuwa ikizikumba Wilaya za Kilosa na Mvomero miaka ya nyuma imepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na juhudi za serikali yake.
Nayo Serikali nchini kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imewahakikishia wafugaji kuwa hakuna mifugo itakayopotea kutokana na magonjwa mbalimbali.
Haya yameelezwa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega wakati akizungumza na wafugaji wa Wilaya ya Kibaha Mkoani Pwani, wakati wa ziara ya kikazi ya siku moja alioifanya Mkoani humo kwa lengo la kukagua miradi iliyoko chini ya wizara hiyo.
Amesema Serikali ilibinafsisha Sekta hiyo kwa watu binafsi, lakini kwa sasa imerejeshwa serikalini ili kuwasaidia wafugaji wa aina zote. “Kwa sasa tunazalisha chanjo ya mdondo zaidi ya milioni 100 kwa mwaka, lengo ni kuwafanya wafugaji wa kuku na hasa akinamama waweze kuondokana na umasikini,”amesema Ulega.
Ameongeza madhumuni ya Serikali ya Awamu ya tano ni kuhakikisha nchi inakuwa na mifugo mizuri yenye kuleta tija kwa wafugaji na wawekezaji wa nyama, hivyo amewataka wafugaji kuamini serikali kwa jinsi inavyowapambania katika kuhakikisha soko la bidhaa hiyo inakuwa kubwa na yenye tija kwao.
Aidha ameongeza kuwa kipindi hiki wafugaji nchini wamekuwa wakinyanyaswa na wafanya biashara kwa kuuza chanjo hizo kwa bei ya Sh.35,000 mpaka Sh. 45,000 kutokana na hali hiyo Serikali imeamua kusambaza dawa hizo za chanjo kwa bei ya Sh.20,000, hivyo itawasaidia watanzania wengi na kuondoa vifo vya mifugo.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala maabara ya Vetenari Tanzania, Dkt. Furaha Mramba amesema chanjo zinazozalishwa katika maabara hiyo zinaubora uliothibitishwa na mamlaka za maabara za Mifugo Afrika na itakapokamilika itatosheleza mahitaji ya ndani na nyingine kuuzwa nje ya nchini.
Katika ziara hiyo Ulega pia ametembelea shamba la kuzalisha malisho ya mifugo lililopo Vikuge Wilayani Kibaha, pamoja Halmashuri ya Chalinze wilayani Bagamoyo kisha kuhutubia mkutano wa hadhara katika kata ya Pangani na kuwaomba wakazi wa kata hiyo kuacha tabia ya kuvamia maeneo yaliotengwa na Serikali kwa ajili ya miradi mbalimbali ya Maendeleo.