SERIKALI imekiri bado inaendelea na mpango wa kuwasaidia wajasiriamali kuzalisha bidhaa bora ili kupata masoko ya uhakika ndani na nje ya nchi.
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe amebainisha mpango wa Serikali katika kuwasaidia wajasiriamali kuzalisha bidhaa bora ili kupata masoko ya uhakika.
Kigahe alisema Serikali imeweka mipango kadhaa ya kuwasaidia wajasiriamali kuzalisha bidhaa bora ili kupata masoko ya uhakika ikiwa ni pamoja na kupitia Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).
Hii ikiwa ni kuwasaidia wajasiriamali wadogo kupata maeneo pamoja na majengo ya kuzalishia bidhaa zao, kuwapatia mitaji kupita Mfuko wa NEDF na nembo ya ubora wa bidhaa zao kwa miaka mitatu bila gharama.
Amesema pia kupitia SIDO, TBS na Wakala wa Vipimo (WMA) wataendelea kutoa mafunzo kwa wajasiriamali kuhusu kanuni za uzalishaji wenye tija, elimu ya utambuzi wa vifungashio na ufungashaji bora
Pia amesema SIDO kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) itaendelea kuandaa na kuratibu maonesho mbalimbali ndani na nje ya nchi ikiwa ni sehemu ya kuchagiza ukuaji wa soko la bidhaa zinazozalishwa na wajasiriamali.
Kigahe alisema, kwa sasa SIDO imekuwa na uwezo mdogo wa kuwezesha mitaji kwa wajasiriamali ambao wamekuwa wakiongezeka kila wakati.