NA BASHIR YAKUB – WAKILI
Matunzo ya mtoto hasa kwa wazazi waliotengana ni pamoja na chakula, makazi, mavazi, elimu, pamoja na malezi bora. Wazazi wote kwa pamoja yaani baba na mama wanao wajibu kila mmoja kwa nafasi yake kuchangia katika matunzo ya mtoto.
Aidha makala haya kupitia Sheria ya Mtoto ,Na. 21 ya 2009 yatajibu ikiwa suala kutoa matunzo ya mtoto ni la milele au linao muda maalum. Lakini kabla ya hayo tutizame nani ana mamlaka ya kufungua shauri kudai matunzo ya mtoto.
- NANI ANAWEZA KUFUNGUA SHAURI LA MATUNZO.
Wengi wetu twajua kuwa ni mama wa mtoto pekee ndiye anayeweza kufungua shauri la mtoto kupatiwa matunzo. Dhana hii si kweli.
Kifungu cha 42( 1 ) cha Sheria ya Mtoto kinawataja wafuatao kuwa na mamlaka ya kuomba mtoto apatiwe matunzo :
( a ) Mzazi wa mtoto. Kifungu hakikutaja mama wa mtoto bali mzazi wa mtoto. Kwahiyo hata baba anaweza kufungua shauri akimtaka mama kutoa matunzo ya mtoto. Mama kumtelekeza mwanae nako ni kumnyima mtoto matunzo .
Wako mama wanakimbia nyumba zao na kuwaacha watoto. Unaweza kutumia kifungu hiki kumtaka mama amchukue mwanae na akae nae ikiwa ni sehemu ya matunzo.
( b ) Mlezi wa mtoto naye amepewa mamlaka ya kufungua shauri kuomba matunzo ya mtoto. Wako watu wako mjini lakini wamewaacha watoto vijijni wakilelewa na ndugu au rafiki.
Lakini pia yapo mazingira ambapo kwa amri ya mahakama imeamriwa mtoto asikae na wazazi bali akae na mlezi kutokana na sababu mbalimbali. Au kwasababu nyingine yoyote mtoto anakaa na mlezi .
Basi ni katika hali hiyo mlezi huyo anayo mamlaka ya kuomba au kufungua shauri akishinikiza mzazi/wazazi kutoa matunzo ya mtoto.
( c ) Mtoto mwenyewe kama anao uwezo anaweza kuomba. Anaweza kuomba mwenyewe au kwa kumtumia ndugu yake au rafiki yake. Hii haswaa ni pale ambapo mtoto anakuwa ametelekezwa na mzazi mmoja au wote wawili lakini akiwa anajua wazazi walipo.
Wapo watoto wako mitaani hasa wale wanaoitwa machokoraa lakini wazazi wao wapo na wanajulikana na watu wanawajua kabisa. Kwahiyo mtoto mwenyewe au mwanajamii kwa kutumia jina la mtoto huyo unaweza kufungua shauri kuwalazimisha wazazi/mzazi aliyepo kumpatia mtoto huyo mahitaji akiwemo elimu.
( d ) Wengine ambao wanaweza kufungua shauri la matunzo ni ustawi wa jamii pamoja na ndugu wa mtoto husika.
- JE MWISHO WA KUTOA MATUNZO NI MIAKA MINGAPI ?.
Kifungu cha 47 cha Sheria ya Mtoto kinasema amri ya kutoa matunzo ya mtoto itakoma mtoto huyo atakapofikisha umri wa miaka 18. Sheria inamtambua mtu mwenye umri wa miaka 18 kuwa mtu mzima.
Pia atakupokuwa amepata ujira wa kumuingizia kipato au amefariki dunia napo amri ya matunzo ya mtoto itakoma.
Hata hivyo kifungu cha 48( 1 ) cha sheria hiyo kinasema kuwa ikiwa mtoto amefikisha miaka 18 lakini bado anasoma shule au chuo cha mafunzo basi kutoa matumizi hakutakoma mpaka hapo atakapokuwa amehitimu.
Kwahiyo kwa ujumla mwisho wa kutoa matumizi ni miaka 18 lakini ikiwa mtoto anaendelea na shule au chuo cha mafunzo basi matumizi yataendelea kutolewa mpaka ahitimu.