BADO imekuwa kitendawili kisicho na jibu pale Wajumbe wa Mkutano Mkuu maalum wa CCM, watakapokutana Jijini Dodoma kati ya Januari 18 na 19 ili kuweza kumtafuta mrithi wa Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, nafasi iliyoachwa na Komred Abdrahman Kinana aliyejiuzulku wadhifa huo.
CCM inayo hazina ya wanachama wakewengi ambao wana sifa nyingi za uongozi ikiwamo hiyo ya ziada ambayo ni upenzi wa chama hicho wengi wakiwa waasisi.
Baadhi ya wafuatiliaji wa masuala ya siasa wanalitaja jina la Waziri Mkuu mstaafu Mizengo Peter Pinda kuwa ndiye anayestahili kuwa Makamu Mwenyekiti mpya, Huku wengine akina Abdalah Bulembo, Steven Wasira, Anne Makinda au mwingine, wanaweza kutumia turufu ya uzoefu wa na kuwashawishi wapiga kura.
Kwa ukubwa wa chama hicho, ni dhahiri atakayechaguliwa anatakiwa awe na uzoefu kwa vile ukiangalia nbafasi hiyo nyeti imewahi kupitiwa na vigogo haswa waliobobea katika masuala ya utawala na hasa siasa za Tanzania.
Wajihi wa Makamu Mwenyekiti ajaye penhgine ashabihiane na uwezo wa watangulizi kama akina Mzee John Malecela, Mzee Pius Msekwa, Mzee Philip Mangula, na Komredi Abdulrahman Kinana katika kukabili siasa za ushin dani wa vyama vingi na kudhibiti makundi ndani ya CCM hasa kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu.
Makamu wenyeviti niliowataja awali, kila mmoja na haiba yake, lakini wote wanafanana kwa uwezo, hekima na busara katika kushughulikia masuala ya siasa hasa ya chama tawala.
CCM wanahitaji Makamu Mwenyekiti msemaji, mwenye mvuto, ushawishi wa makundi na rika tofauti, mtu mkweli na asiyeyumbishwa kwa maslahi binafsi au ya kikundi.
Makamu Mwenyekiti mpya wa CCM ni lazima awe na mtaji binafsi wa kumuongezea kura mgombea urais wa CCM katika Uchaguzi Mkuu.
Je, ni Komredi Bulembo, Pinda, Wasira, Anne Makinda au ni kada yupi kati ya wale tuliowagusia siku za nyuma?
Kwa upande mwingine, CCM wanahitaji Makamu Mwenyekiti licha ya kuwa ni wa Tanzania Bara, lakini mwenye kukubalika Tanzania nzima ikiwamo Tanzania Zanzibar.
Wakati huu ambao wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM wanajian daa kwa safari ya kwenda Dodoma, ni muhimu sana wakumbuke kuwa siasa ni shughuli ya makundi, mwanasiasa asiye na kundi hawezi kukisaidia au kumudu mikikimikiki ya siasa.
Makamu Mwenyekiti mpya atakayepatikana anahitajika mtu mwenye ushawishi na mwenye watu ambaye hatolazimika kuanza kujitambulisha kwa umma.
Mwenyekiti mstaafu wa CCM Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema kwamba alikumbana na mgombea ubunge ambaye hata mwenyekiti wake wa chama hamjui.