NA JIMMY CHIKA
ILIKUWA Saadan iliyogubikwa na giza, umasikini uliochagizwa ukosefu wa huduma za kijamii na kulifanya eneo hilo lisifikike kwa urahisi kutokea katika Miji mikubwa inayolizunguka kama vile yalipo makao makuu ya wilaya, Bagamoyo na Jiji la Dar es salaam.
Nyuma ya miaka ya 1960 hakukuwa na mwanga katika eneo hilo, wenyeji walioshi eneo hilo walijikita katika kazi ya uvuvi wakitumia nyenzo duni, pia kulikuwa na biashara nyingine kama vile ukataji wa ukindu, zao lililotumika sana kwa ajili ya ususi wa mikeka na vikapu, kadhalika ukataji miti ya Mikoko iliyokuwa ikisafirisahwa kwa majahazi kwenda katika miji ya Zanzibar na hata nje ya nchi Mombasa na Visiwa vya Comoro.
Mwanga ulijitokeza mwaka 1962 ilipoanzishwa Bustani ya wanyama, iliyojmumuisha wanyama wachache waliofungiwa katika Ng’enge (Zoo) kubwa na ndogo, zilizoanza kuvuta macho ya watalii kuanza kutembelea kijiji hicho kilichokuwa na wakazi wachache, wengi wao wakitokea maeneo mbalimbali ya nchi na kuafauata biashara ya uvuvi.
Enzi za Ukoloni Saadani iliwahi kukaliwa na Koloni la Waarabu walioendesha biashara ya utumwa, iliyotanabaishwa na kuwewpo mabaki ya magofu machache yaliyokuwa yakitumiwa katika biashara hiyo, pia gati kuu la kusafirishia watumwa kutoka bandari ndogo ya Saadani kuelekea Unguja na nchi nyingine za jirani.
Kwa mujibu wa simulizi za wazee wa mji huo hata jina hili la Saadani, lilitokana na Mzee mmoja wa Kiarabu aliyekuwa akimiliki saa ya ukutani, hivyo alipochoshwa na maswali ya kuulizwa muda “Saa ngapi? kila mara akawa anawajibu “kama unataka saa nenda kaangalie ndani.
Kwa vile hakuweza kutamka vizuri maneno ya Kiswahili ndipo alipokuwa akikatisha tu kwa kusema “Saadani” ndipo likazaliwa jina hili.
Ukuaji wa mbuga hiyo ya wanyama iliweza kuupa umaarufu mji huo mdogo ulipo kandoni mwa Bahari ya Hindi kwa kuanza kutembelewa na watalii pamoja na watu maarufu, akiwemo Mwanasiasa aliyeshika nyadhifa mbalimbali serikalini Mzee Rashid Mfaume Kawawa, aliyefika Saadani Mwaka 1974 na kuweka jiwe la Msingi la kumbukumbu ya ujiuo wake na uzinduzi wa bustani hiyo ya wanyama.
Kwa bahati nzuri kijiji cha saadan kiliweza kuonja maendeleo mapema kwa kupata zahanati pamoja na Shule ya Msingi iliyoanza ikiwa na madarasa manne na baadaye ikaendelea na kukamilisha madarasa yote saba, pia kiliwahi kununua gari aina ya Center kwa ajili ya shughuli za kijiji.
Kupitia uwepo wa bustani hiyi ya wanyama kijiji nhicho kilianza kupokea wafanyakazi wengi wakati huo wakijulikana kama ‘Game Scout’ kutoka maeneo mbali mbali na baadhi waliajiriwa wananchi wakazi wa kijiji hicho na vile vinavyozunguka bustani hiyo kama Uvinje, Buyuni Kuu na Buyuni Kitopeni.
Kwa kuwa mazingira ya hifadhi ya Saadani ni Jangwa wafanyabiashara wenye asili ya India chini ya Kampuni ya Albhai Panju and Sons walianzisha kilimo cha zao la chumvi na kuvuna maelfu ya tani waliyoisafisha kwenda maeneo mbalimbali ya nchi.
Kampunu hiyo iliweka kiwanda chake maeneo ya Malumbi nje kidogo ya Bustani ya Wanyama ya Saadan, na baadaye serikali kupitia Shirika la Madini la Taifa (Stamico) iliweza kuanzisha kiwanda cha kisasa cha uzalishaji chumvi na kupeleka watalaamu wa madini na kuanzisha mradi huo uliokuwa mkubwa sana.
Lakini katika kipindi chote Hifadhi hii iliyopo chini ya TANAPA, iliyoanzishwa mwaka 1962 ikiwa ni pori la akiba na Mwaka 2005, kupandishwa hadhi rasmi na kuwa hifadhi ya taifa, ikashuhudia ongezeko la wahamiaji waliovutwa na upatikanaji wa Samaki aina ya Kamba ambao katika kijiji hicho hujulikana kama Makaji ambayo yalikuwa yakiuzwa kwa bei kubwa na kuwa na maslahi mazuri kwa wavuvi.
Makampuni binafsi kama vile Dar Ocean Product na hata Tafico walikivamia kijiji hicho kwa ajili ya kununua samaki hao kutoka kwa wavuvi wenyewe moja kwa moja.
Lakini katika kipaindi chote hivyo huku zikipita awamu zote tano la utawala wa Serikali ya jamhuri ya Muungano wa Tanzania wana kijiji walikuwa na changamoto mbalimbali za maendelo kama vile ukosefu wa nishati ya umeme na maji.
Kadhalika miundombinu ya barabara inayotokea mwishoni mwa daraja la kisasa la Wami kuingia kulia katika Vijiji vya Mandela na baadaye Miono, Zimbili, Mkange na kuingia Saadan ilikiuwa ipo katika hali mbaya.
Serikali ikaifanyia kazi changamoto hiyo baada ya kufanya ujenzi wa kisasa wa baraba inayotokea eneo la Makurunge Bagamoyo yalipokuwa mashamba ya mifugo ya Ranchi ya Zanzibar Bagamoyo (RAZABA) hadi kuingia Kijiji cha Saadani kupitia miji iliyokuwa kandoni mwa bahari ya Hindi kama vile Mkwaja na Buyuni.
Katika utawala huu wa awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, Mbunga ya Saadani inang’aa,baada ya kupatiwa umeme wa kutosha.
Kwa takriban mwaka sasa wakazi wa Saadani wanafaidika na uwepo wa nishati ya umeme, waliyoikosa tangu nchi kupata uhuru.
Kufuatia kupatikana kwa nishati hiyo kijiji cha Saadan kilichokuwa kikikumbana na matukio ya kuvamiwa na wanyama wakati na waharibifu kama vile Tembo na Simba sasa imepungua na kuwa sehemu salama toka kijiji hadi mmbuga yenyewe.
Hivi sasa mkazi wa Saadani atakayetafuta bughudha ya kukutana na wanyama ni yule atayekwenda misituni kwa ajili ya kufanya shuguli za kibinadamu kama vile kuzoa chumvi au kuvua katika maeno yasiyokuwa rasmi kwa shuguli hiyo.
Wakazi wa Saadani kwa sasa wanaliimba jina la Rais Samia kwamba ndiye aliyendika historia ya kuing’arisha Saadani, kizazi kipya kutoka eneo hili sasa hakina tena histoiria ya enzi hizo ambazo wakazi walifuata taa aina ya Karabai iliyokuwa ikiwashwa na wafanyabiasha maarufu enzi hizo Mohamed Mwarabu al maarufu Mzee Ganda na Mfaume Akida Mimi na Sheikh Said waliokuwa wakimiliki maduka zama hizo.