MWENYEKITIi wa Chadema, Kanda ya Victoria, Ezekia Wenje amedai kuwa suala la maridhiano ambalo kwa sasa limeibua sintofahamu ndani ya chama hicho lilianza tangu wakati wa Rais wa awamu ya tano, John Magufuli.
Wenje ameyasema hayo leo Alhamisi Januari 16, 2025 alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
Mgombea huyo wa umakamu mwenyekiti bara Chadema, amedai kuwa Hayati Magufuli aliwahi kumpigia simu Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe na kumtaka wahudhurie sherehe za uhuru na baada ya hapo watazungumza.
“Mwenyekiti (Mbowe) alituambia kuhusu mwaliko wa Magufuli na tulikubaliana, tukaelekea Mwanza kwenye sherehe hizo… Hata Lissu akiwa Ubelgiji alipokutana na Rais Samia moja ya alichokisema ni kutaka Mbowe aachiwe, hayo ni maridhiano,”amesema Wenje.
Majibu ya Wenje ambaye ni mgombea wa nafasi ya makamu mwenyekiti wa Chadema Bara, yanakuja ikiwa ni siku chache kuelekea uchaguzi wa chama hicho huku minyukano baina yao ikiendelea.