Vitu vikubwa, mambo makubwa ndiyo yanayofanywa na Mhandisi Manala Tabu Mbumba, kubwa zaidi ikiwa ni kuzipigania na kuzitimiza ndoto za Rais Dk. Samia Suluhu Hassan juu ya matumizi ya nishati safi na maendeleo ya Watanzania kwa ujumla.
Mhandishi Manala amejipambanua vyema ndani ya Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, kutokana na kazi anayofanya ya kutimiza maatumizi ya nishati safi, huku akiwa msaada mkubwa kwa jamii kwa mambo mbalimbali.
Kupitia asasi ya Manala Foundation, mhandisi huyu aliyebobea katika masuala ya nishati, taasisi yake imefanikiwa kwa kiwango kikubwa kuboresha maisha ya wananchi wa Manispaa ya Kahama, mkoani Shinyanga.
Katika mahojiano maalumu na DARASA HURU, Mhandisi Manala alieleza malengo ya taasisi hiyo, ambayo ni kushirikiana na serikali ili kufanikisha maendeleo endelevu kupitia miradi ya kijamii.
NISHATI SAFI
Mhandisi Manala anakiri kwamba kupambana juu ya nishati safi na mbadala ni jambo la lazima, huku akimsifu Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kulipambania kwa kiwango kikubwa.
“Tunamuunga mkono Rais Dk. Samia katika hili, si kwa maneno ila kwa vitendo na tutakuwa naye bega kwa bega na tunamuhakikishia kuwa hatutamuacha,” alisema Mhandisi Mbumba.
Wakati taifa likiyapigania hayo takwimu zinaonyesha kuwa takribani Watanzania 33,000 wanafariki dunia, ikiwa ni moja ya athari ya matumizi ya nishati isiyo safi na salama.
Hii ina maana takribani asilimia 82 ya Watanzania hutegemea kuni na mkaa kwa kupikia, hali inayochangia madhara makubwa ya kiafya, kimazingira na kijamii.
Takwimu zinaonyesha kwamba watu takriban bilioni 2.3 duniani bado hawajafanikiwa kutumia nishati safi ya kupikia huku chini Jangwa la Sahara kwa Afrika wakiwa watu milioni 990.
Hii inaonyesha takribani watu milioni 3 dunia nzima huwa wanafariki kwa magonjwa ya hewa ambayo yanatokana na matumizi ya nishati isiyo safi, ambapo katika watu hao milioni 3, takribani asilimia 60 huwa ni wanawake na watoto.
Hivyo katika kuunga mkono juhudi za serikali za kulinda mazingira, Mhandisi Manal kupitia Manala Foundation wanafanya kazi ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi na mbadala, ili kupunguza utegemezi wa nishati za kuharibu mazingira kama mkaa na kuni, ambavyo pia vinachangia idadi hiyo ya watu.
Mhandisi Manala ambaye ni mtaalamu wa nishati safi, alisema kuwa ni muhimu kwa jamii kuona umuhimu wa kutunza mazingira kwa kutumia vyanzo vya nishati ambavyo haviharibu misitu.
“Ni jukumu letu kama taifa kuhakikisha tunapunguza madhara ya matumizi yasiyo endelevu ya nishati. Kama Manala Foundation, tutahakikisha tunasimamia kampeni za kuhamasisha matumizi ya nishati safi kwa ustawi wa familia na mazingira,” alisema Mhandisi Manala Mbumba.
KUMUUNGA MKONO DK. SAMIA
Mhandisi Manala Mbumba anasema, Manala Foundation ilianzishwa kwa lengo la kuunga mkono juhudi za serikali ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ambaye ameonyesha msukumo mkubwa katika kuleta maendeleo nchini.
Taasisi hiyo ililenga kuchangia katika nyanja muhimu kama elimu, afya, uchumi, na mazingira, ili kuhakikisha malengo ya maendeleo ya Taifa yanafikiwa.
“Tumeona juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali yetu katika sekta mbalimbali kama elimu, afya, miundombinu, kilimo na kama Manala Foundation, tumeona kuna haja ya kusaidia kwa kushirikiana na Serikali ili kuhakikisha maendeleo haya yanapatikana kwa jamii ya wana Kahama,” alisema Mhandisi Manala Mbumba.
ELIMU
Elimu ni moja ya maeneo muhimu ambayo Manala Foundation inatilia mkazo. Katika kipindi cha miezi mitano tangu taasisi hiyo isajiliwe, imeweza kufikia kaya 32 katika Manispaa ya Kahama.
Hii ni kwa kuwasaidia watoto wa familia zenye mahitaji maalumu kwa kutoa msaada wa vifaa vya shule na miundombinu muhimu. Lengo ni kuhakikisha watoto hao wanapata elimu bora bila vikwazo vya kimaisha.
AFYA
Katika sekta ya afya, Mhandisi Manala Mbumba alisema, Manala Foundation imejidhatiti kuhakikisha jamii inapata huduma bora za afya.
Alikiri kuwepo ushirikiano wao na Hospitali ya Manispaa ya Kahama katika kuhamasisha wananchi kuchangia damu salama wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru zilizofanyika katika Kata ya Kagongwa.
Alisema kuwa zoezi hilo liliweza kupata unit 51 za damu salama ndani ya siku mmoja, huku pia ikitoa huduma za bima ya afya kwa watoto yatima na wasichana ili kuwawezesha kupata matibabu bila vikwazo.
Katika uchangiaji damu walishirikiana na Shirika la Red Cross Tanzania na Ofisi ya Mganga Mkuu Manispaa ya Kahama kupitia Kitengo cha Damu Salama wamefanikisha zoezi la kuchangia damu kwa hiari.
Mratibu wa Damu Salama, Elibahati Molle alipongeza juhudi za Manala Foundation kwa kuhamasisha jamii hiyo katika kuchangia damu kwa hiari na kukusanya unit 51 za damu.
Mhandisi Manala Mbumba, alisema taasisi yake itaendelea kuunga mkono juhudi za serikali katika nyanja mbalimbali kwa kushirikiana na wadau wengine wa maendeleo na ustawi wa jamii, pia kuunga juhudi za Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
Mhandisi Manala aliishukuru Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi Mtendaji Kahama, pamoja na Mganga Mkuu wa Manispaa ya Kahama kwa ushirikiano wao kuhakikisha zoezi hilo linafanikiwa, ambapo aliwashauri wadau mbalimbali kujitokeza na kushirikiana na Serikali katika kutatua changamoto zinazoikumba jamii.
Naye Mkurugenzi wa Huduma za Afya Ustawi wa Jamii na Lishe (TAMISEMI), Dk. Rashid Mfaume alikiri hivi karibuni kuhusu suala la uchangiaji damu ndani ya Kahama akisema, hilo ni jambo linalopaswa kupewa kipaumbele.
“Kuhusu uchangiaji wa damu salama Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Kahama, mashirika ya asasi za kiraia pamoja na ofisi ya mkuu wa wilaya wanapaswa kuhamasisha uchangiaji wa damu salama kwa wananchi ili kulinda benki ya damu salama ili kuokoa uhai wa watu wanaopata ajali mbalimbali,” alisema Dk. Rashid Mfaume.
Miongoni mwa wananchi waliochangia damu, Juma Mabula, ameeleza kuwa kupitia uhamasishaji wa Taasisi ya Manala Foundation ameweza kuchangia damu ambayo inaenda kuwasaidia wahitaji.
Kutokana na umuhimu wa afya, Kaimu Mganga Mkuu wa Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga Dk. Fredrick Malunde ametoa ombi kuwa Hospitali ya Manispaa ya Kahama Mkoani Shinyanga ipande hadhi na kuwa Hospitali ya Rufani kutokana na kuelemewa na wagonjwa 1000, kwa siku.
Amesema kwa siku wanahudumia wastani wa wagonjwa 1,000 kutoka katika Wilaya ya Kahama na Mikoa jirani ya Tabora na Geita pia na kupata rufaa za wagonjwa kutoka katika Hospitali za Halmashauri za Ushetu na Msalala.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kahama, Masudi Kibetu amesema wamejipanga vyema kuendelea kuboresha miundombinu na vifaa tiba pamoja, dawa na watumishi kwenye hospitali hiyo.
Katika hili Mhandisi Manala, amesema Manala Foundation itashirikiana bega kwa bega na uongozi wa hospitali ili kutatua baadhi ya changamoto inazozikabili na wanaamini watafanikiwa katika hilo.
MIRADI
Katika kuinua wananchi kwa miradi ya maendeleo
Manala Foundation pia inajivunia miradi inayolenga kuinua uchumi wa wananchi wa Kahama.
Mhandisi Manala alisema, taasisi hiyo imeanzisha miradi ya ufugaji wa kuku kwa vikundi vya wanawake na vijana, ambapo wamekuwa sehemu ya ufadhili.
Aidha, wanahamasisha vikundi vya bodaboda kutumia mapato yao kwa ufanisi na kwa sasa wanajiandaa kuanzisha biashara ya migahawa ya vyakula ili kuongeza kipato cha vikundi hivyo.
“Tunaendelea kuhamasisha wananchi wa Kahama na maeneo mengine kuhusu umuhimu wa kujitegemea kupitia miradi ya maendeleo na mikopo ya halmashauri, hasa kwa makundi ya wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu,” alisisitiza Mhandisi Manala.
MIKAKATI 2025
Akizungumzia mikakati ya mwaka 2025, Mhandisi Manala alisema kuwa taasisi yake inakusudia kuongeza wigo wa huduma kwa jamii na kuendelea kushirikiana na Serikali katika kutimiza malengo ya maendeleo. Lengo ni kuzifikia jamii zaidi na kuleta mabadiliko chanya katika maisha ya wananchi wa Kahama.
“Kauli mbiu yetu ni ‘Kahama Kwanza Kwa Maendeleo Endelevu’. Tunataka kuhakikisha usawa wa maendeleo kwa wote na kuunga mkono juhudi za Rais Dk. Samia Suluhu Hassan,” alisema Mhandisi Manala, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa wananchi na taasisi za kijamii katika kufikia malengo ya Taifa.