NA MWANDISHI WETU, Z’bar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema Zanzibar itaendelea kuweka mazingira mazuri zaidi ya kuwavutia wawekezaji zaidi kuwekeza nchini.
Rais Dkt. Mwinyi ametoa tamko hilo alipozungumza na Balozi wa Tanzania Nchini, Celestine Kakele aliyefika Ikulu kujitambulisha.
Rais Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa kuna fursa kubwa ya nchi hizo mbili kushirikiana hasa katika Sekta ya Utalii na Uwekezaji ambazo zikifanyika vyema nchi hizo zinaweza kunufaika kwa kiasi kikubwa.
Dk. Mwinyi amemsisitiza Balozi Kakele kufanya juhudi maalum za kuwavutia wawekezaji kutoka Nigeria kuja kuangalia fursa za Uwekezaji na Serikali inaandaa Mazingira mazuri ya kuwa na Uwekezaji wenye tija na Endelevu.
Amemuhakikishia Balozi huyo kuwa Serikali inaimarisha Uwekezaji kwa kuondoa vikwazo vinavyozorotesha ushirikiano kwa lengo la kuwavutia wawekezaji.
Amefahamisha kuwa utalii na uwekezaji ni vichocheo muhimu vya uchumi wa Zanzibar hivyo ni vema akaweka mkazo katika kuwavutia wawekezaji katika maeneo hayo.
Rais Dkt. Mwinyi ameilezea Sekta ya Biashara kuwa ni eneo jengine ambalo nchi hizo mbili zinaweza zikashirikiana katika kuuziana bidhaa za ndani, huku akisema bidhaa nyingi toka Afrika Magharibi zinauzwa nje ya Afrika kuliko zile zinazouzwa katika Ukanda wa Afrika.
Naye Balozi Kakele amesema Nigeria ina fursa nyingi ambazo Tanzania ikiwemo Zanzibar zinaweza kushirikiana hususani uwekezaji katika biashara na huduma za kibenki na kushauri kuandaliwa mazingira wezeshi ya upatikanaji viza baina ya nchi hizo.