Na Mwandishi Wetu
WAKATI Watanzania wakielekea kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu na Uchaguzi Mkuu mwakani, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), imewataka wapiga kura kuichukia rushwa ili waweze kupata viongozi bora watakaowaletea maendeleo kwenye maeneo yao.
Hayo, yalisemwa na Mkurugenzi Kuu wa TAKUKURU, Kamishna wa Polisi, Salum Hamdun wakati alipokutana na Wahariri na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam jana akisema tasisi hiyo ipo tayari kushirikiana nao katika mapambano ya vitendo hivyo katika chaguzi hizo.
Alisema wananchi wanapaswa kutambua kuwa rushwa katika chaguzi ina madhara mengi ikiwemo upatikanaji viongozi wasio waadilifu.
“Rushwa katika uchaguzi ina madhara mengi sana, madhara hayo ni pamoja na upatikanaji viongozi wasio waadilifu, wanaojihusisha na vitendo vya rushwa pamoja na kutozingatia misingi ya haki, usawa, uwazi, uwajibikaji na uzalendo mambo ambayo ni muhimu katika ustawi wa wananchi.
“Rushwa inadhoofisha utawala bora na demokrasia, ambapo baadhi ya wananchi wenye sifa za uongozi bora hushindwa kugombea au kutoteuliwa na kutochaguliwa kwa kuwa hawajatoa hongo,”alisema Kamishna Hamduni.
Kamishna Hamduni ametaja athari nyingine za rushwa kwenye uchaguzi ni uvunjifu wa amani kutokana na migogoro ya kisiasa, nchi kugubikwa na rushwa, wananchi kukosa imani na serikali na hata kusababisha machafuko.
“La kusikitisha zaidi ni kudhalilisha utu kwa kufananisha thamani ya mtu na hongo (fedha, nguo, chakula), anayopewa ili apige au asipige kura.
“Kutokana na ukubwa wa athari zinazoweza kusababishwa na vitendo ya rushwa katika uchaguzi, TAKUKURU imeona ni busara kukutana nanyi kwa lengo la kujadili tatizo la rushwa katika uchaguzi, madhara yake na kisha kuweka mikakati ya pamoja ya kuzuia na kupambana nayo kabla madhara hayajatokea,”alisema Kamishna Hamduni.
Kamishna Hamduni, alisema vyombo vya habari vimekuwa mstari wa mbele katika kutetea haki na usawa, kuelimisha na kuhamasisha wananchi kutambua haki na wajibu wao katika masuala ya kijamii, kiuchumi na kisiasa ikiwamo kushiriki katika uchaguzi pamoja na shughuli za maendeleo, hivyo vinavyo nafasi ya kusaidia vita dhidi ya rushwa.
“Ukaribu huu mlionao kwa jamii unawafanya kuwa kundi muhimu sana ambalo linaweza kusaidia kuandaa mkakati wa kudhibiti vitendo vya rushwa kwenye uchaguzi.
“TAKUKURU inaamini ushiriki wenu katika kuandaa mkakati wa kudhibiti vitendo ya rushwa kwenye uchaguzi una faida kubwa, ikiwamo kuchaguliwa kwa viongozi bora watakaoongoza kwa mujibu wa sheria na kutekeleza mipango ya maendeleo,”alisema.
Aidha, Kamishna Hamduni, alisema TAKUKURU kupitia Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sura 329, imejizatiti kuzuia na kupambana na rushwa katika uchaguzi kwa kuelimisha umma kuhusu madhara ya rushwa ili uchague viongozi waadilifu.
Kamishna Hamduni alisema, “Ninaamini kupitia warsha hii tutaweza kuja na makakati kabambe wa kudhibiti rushwa katika uchaguzi…Ni rai yangu kwenu kuwa mtumie warsha hii kama fursa muhimu sana ya kuijenga Tanzania ambayo viongozi wake wamepatikana bila kujihusisha na vitendo vya rushwa.”
TAKUKURU: Wananchi msichaguwe viongozi wala rushwa, watawaletea umasikini
Leave a comment
Leave a comment