- Ashuhudia upokeaji wa gawio la zaidi ya bilioni 600 kwa serikali kutoka mashirika na makampuni ambayo serikali ina hisa ama kumiliki
- Bandari watia fora, watoa gawio la zaidi ya bilioni 150, matunda ya uwekezaji Madhubuti yaanza kuonekana
- Asema anaamini mwakani gawio litaongezeka zaidi ya hapo
- Awapuuza wapotoshaji wanaokesha kuzusha taharuki, kumkejeli na kumtukana akisisitiza anachotaka ni mapinduzi ya kiuchumi
- Makamu mwenyekiti MECIRA ammwagia pongezi kusimama kidete bila kuyumba
Na. Mwandishi wetu
Rais Samia Suluhu Hassan ameipongeza Mamlaka ya usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa kutoa gawio kwa serikali kiasi cha Bilioni 153.9 na kwamba wanaopiga kelele kuwa ‘mama kauza bandari’ ni wazi kuwa wameona faida ya uwekezaji uliyofanywa bandarini hapo.
Rais Samia ameyasema hayo jana Ikulu, jijini Dar es Salaam wakati wa halfa ya kukabidhi gawio kwa serikali kutoka kwenye mashirika ya umma na binafsi, hafla hiyo yenye kauli mbiu ‘Mageuzi ya mashirika ya umma na wajibu wa kuchangia maendelwo ya Tanzania.
Amesema anaamini kuwa TPA itaendelea kupata faida na kutoa gawio kubwa zaidi kwa serikali hasa kutokana na mageuzi hayo yaliyofanyika.
“Pongezi maalum kwa makampuni yaliyoleta gawio kwa serikali ikiwemo TPA ambayo nina uhakika mwaka jana hii haikuwa level yenu, lakini kwa mageuzi yaliyotokea bandarini mmeweza kufikia kiwango hiki na mwakani nina uhakika mnaweza kuleta double ya mlichokitoa leo.
“Huko ndiko tulikuwa tunaelekea ndugu zangu, wale waliokuwa wanapiga kelele mama kauza bandari, mama kauza bandari, mama kauza nini, mauzo yale faida yake ni hii hapa na huu ni mwanzo tu tunatarajia kupata faida kubwa zaidi,” amesema Rais Samia
Kwa upande wake Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu aliwataka watendaji wakuuu na Wakurugenzi wa mashirika ya umma wawe tayari kwa mabadiliko yatakayowawezesha kubadili namna yao ya kuendesha mambo na kutoa gawio kwa serikali.
Amesema watendaji hao kuhakikisha wanaongeza ubinifu na kukuza mapato ya taasisi zao ili yaweze kuingia kwenye mfuko mkuu wa serikali na kusaidia katika maendeleo ya Taifa
“Gawio linatolewa na taasisi za umma ni chini ya asilimia tatu na hivyo lazima mabadiliko makubwa yafanyike kufikia lengo la serikali la kupata gawio kwa asilimia 100,” amesema Mchechu.
Amesema taasisi ambazo serikali ina asilimia ndogo inachangia fedha nyingi katika mfuko mkuu wa serikali tofauti na mchango mdogo unatolewa na taasisi zinazomilikiwa na serikali kwa asilimia 100.
Ameongeza kuwa ofisi yake imekusudia kuja na mfumo thabiti ili kusaidia serikali kufanya uamuzi sahihi wakati wa uteuzi wa viongozi wa taasisi na mashirika mbalimbali.
Mchechu amesema mifumo hiyo itaondoa changamoto ya kuteua na kutengua ndani ya muda mfupi baada ya kuteuliwa
Aidha, Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limejitokeza kama moja ya taasisi za serikali zilizoshiriki katika utoaji wa gawio kwa mfuko wa Hazina ya Taifa gawio lililosilishwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Mussa Mandia pamoja na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Bw. Nahson Sigalla.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukabidhi gawio hilo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu, Bw. Nahson Sigala, ameishukuru Serikali ya awamu ya Sita kwa kuchagiza Sekta ya Usafiri Majini na kupelekea matokeo ya ukusanyaji mzuri wa mapato.
“Tunaipongeza sana Serikali ya awamu ya Sita chini ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uongozi thabiti hasa katika sekta hii ya Uchukuzi na kusababisha na sisi TASAC Kuchangia katika mfuko huu wa Hazina ya Taifa kwa kiasi cha shilingi bilioni 19.057 kama matokeo mazuri ya utekelezaji wa majukumu yetu”.
Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, alithibitisha kwamba TASAC imetoa gawio la shilingi bilioni 19.1 kwa mwaka unaoishia Juni 2024, huku akitoa shukrani za dhati kwa utendaji wao mzuri.
Aidha Rais Samia Suluhu Hassan amesema hatakubali mtu yoyote amkwamishe kwenye azma yake ya kuleta mageuzi ya kiuchumi anayoendelea nayo na kwamba kila mmoja akafanye mageuzi ili kuongeza tija katika kukuza uchumi.
Akihutubia mara baada ya kupokea gawio na michango kutoka kwa mashirika na taasisi za umma, Rais Samia amesema ajenda kubwa kwa sasa ni kukuza uchumi kupitia mageuzi ya kisekta ambayo yataipeleka nchi kwenye uchumi
wa juu zaidi.
Amesema hataki kuona mtu yoyote anamkwamisha katika jambo hilo na kuwataka wakuu wa taasisi na viongozi wengine kuhakikisha wanaifanyia kazi falsafa hiyo na kuleta tija kwa Taifa na kuendelea kubakia katika uchumi wa kati.
“Hivi karibuni tumeingia tena kwenye kundi la uchumi wa kati kama ambavyo imeainishwa na wenzetu wa Benki ya Dunia, sasa ili uendelee kubakia katika kundi hilo ni lazima kuwe na mageuzi makubwa katika uchumi ili kuendelea kuaminika zaidi”, amesema Rais Samia
Kuhusiana na mashirika yasiyofanya vizuri, Rais Samia amemtaka Msajili wa Hazina kuhakikisha anasimamia zoezi hilo na akishindwa basi yeye mwenyewe (Rais Samia) ataingilia kati na kuyafuta.
Amerudia tena agizo lake la kuhakikisha mifumo ya Serikali inasomana ifikapo mwezi Disemba mwaka huu bila kuwa na kisingizio chochote.