- Matamanio ya Rais Dkt. Samia ya benki kukopesha kwa riba ya chini ya asilimia 10 hayawezi kutimia kutokana na wafanyabiashara wakubwa wanaokopa mabilioni kukwepa kurudisha mikopo hiyo na kugeuka
- Hii inasababisha hasara itokanayo na mikopo chechefu iwahusu watanzania wote na sio mabenki pekee kwani wanaoathirika na hali hii wengi wao ni masikini
- Wakati Serikali ikikopa mabilioni kuiwezesha TADP ijinusuru baada ya kupungukiwa mtaji, wajanja wachache wameramba zaidi ya bilioni 80 kichechefu
- Zaidi ya bilioni 100 zinahitajika kuwekezwa na serikali ili benki ya TIB iweze kufanya biashara baada na yenyewe pia kukutana na upepo chechefu
- TCB ‘Tanzania Comercial Bank’ nayo hoi, Serikali imeweka zaidi ya bilioni 130 kuinusuru iweze kujiendesha baada ya madhara ya mikopo chechefu
- TCB imeundwa baada ya kuziunganisha benki kadhaa zilizofilisika kutokana na mikopo chechefu zikiwemo Benki ya wanawake. Benki ya Posta, Twiga Bancorp na TIB Corporate
Na. Mwandishi wetu,
Wakati serikali ikitumia mabilioni ya fedha kuwezesha mabenki kujiendesha inayoyamiliki kujiendesha kutokana na kukosa mitaji, dalili za fedha hizo kupotea ama kutafunwa na wajanja inaonekana wazi kama Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan hatachukua hatua za haraka kudhibiti michezo michafu ya upigaji wa fedha za mabenki hayo kupitia mikopo isiyolipika kwa makusudi
Taarifa zinaonyesha kuwa Serikali imepanga kuiwezesha Benji TCB (Tanzania Commecia Bank) mtaji wa zaidi ya shilingi bilioni 130 ili kuihuisha benki hiyo inayoundwa na mjumuiko wa benki kadhaa zilizofilisika kutokana na mikopo chechefu nchini
Miongoni mwa benki zilizofilisika na kuungwa pamoja kuunda TCB ni pamoja na benki ya wanawake, benki ya Posta, Twiga Bancorp na TIB Corporate ambazo kwa nyakati tofauti benki hizo zilifilisika pamoja na mambo mengine lakini pia mikopo chechefu ikitamalaki
Aidha serikali inaelezwa kuweka zaidi ya shilingi bilioni 100 kuhuisha mtaji wa benki ya uwekezaji TIB ili iendelee na biashara ambayo hadi sasa inasua sua kutokana na kuelekea kufilisika kwa mikopo chechefu ambayo hailipiki
mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere anasema Serikali inahitaji kuongeza mtaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) ili kukidhi matakwa ya mtaji kwa mdhibiti siri zimezidi kuvuja kuwa sababu ya benki hiyo kujikongoja ni uwepo wa Mikopo chechefu kwa wafanyabiashara wakubwa walioamua kuigeuza benki hiyo kuwa shamba la bibi kwa kukopa na kukataa kulipa
wakati wa makabidhiano ya ripoti ya mwaka wa fedha 2022/23 kwa Rais Samia Suluhu Hassan mjini Dodoma CAG alisema kuwa benki hiyo ina mtaji mdogo ikiwa na mtaji wa 88.12bn/- tu kinyume na matakwa ya 200bn/- kwa mujibu wa mwongozo wa benki na taasisi za fedha wa mwaka 2020. /21.
“Benki ya kilimo inakabiliwa na changamoto kubwa ya uhaba wa mtaji, hivyo kutoa wito kwa serikali kuendelea kuingiza pesa zaidi ili kuboresha mtaji wa wakopeshaji wa kilimo,” alisema Bw Kichere kwenye hafla hiyo.
Hata hivyo alisema anafahamu mipango ya serikali ya kuingiza 118.88bn/- ili kukuza mtaji wa wakopeshaji wa kilimo na kukidhi mahitaji ya mtaji. Katika maendeleo ya hivi karibuni mwezi uliopita, serikali ilipata mikataba ya mikopo ya kimataifa kufadhili sekta ya miundombinu na kilimo.
Katika utaratibu huu wa mikopo, sekta ya kilimo ilipata shilingi bilioni 166.4 ili kuongeza mtaji wa TADB unaolenga kugharamia shughuli za kilimo hivyo kuongeza uzalishaji, kuimarisha usalama wa chakula, kukuza biashara ya bidhaa zinazouzwa ndani na nje ya nchi pamoja na kuongeza ajira na kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja. , familia na taifa kwa ujumla.
Taarifa za uhakika ambazo gazeti hili linazo, zinaonyesha kuwa zaidi ya shilingi bilioni 100 za benki hiyo zipo kwa wafanyabiashara wachache waliogoma kulipa mikopo kwa sababu mbalimbali ikiwemo kukimbilia mahakamani kujificha
Miongoni mwa wafanyabiashara waliokopa kiasi kikubwa cha fedha katika benki hiyo ni pamoja na kampuni ya Global agency iliyochukua bilioni 26 kwa mradi wa shamba la kilimo mkoani kagera huku Chobo Investment ikichukua bilioni 12 bila kurudisha
Mwingine anayetajwa kukomba mabilioni ya shilingi katika benki hiyo ni kampuni ya Kahama oil millers (KOMU) ambayo imechukua zaidi ya shilingi bilioni 40 na hadi sasa haijulikani itarejeshaje kiasi hicho cha pesa
Kukithiri kwa mikopo chechefu sio tu kunayaathiri mabenki yanayotoa mikopo hiyo bali pia hupeleka athari za moja kwa moja kwa Watanzania ambao wanategemea mikopo ishuke riba ili na wao wakope
‘’miongoni mwa sababu za kisayansi za riba kuwa zaidi ya asilimia 18 ni wastani wa mikopo chechefu, mikopo mingi inayoshindwa kurejeshwa inayatia mabenki hasara kubwa na kwa bahati mbaya wengi wanaoshindwa kurejesha ni wafanyabiashara wakubwa ambao hukopa mabilioni, hivyo ili benki kujilinda na hasara hizo huweka riba kubwa kufidia mapengo hayo’’ anasema CPA Crispin Peter, mtaalam wa masuala ya fedha
Anaongeza kuwa ni vyema serikali iendelee kuweka kanuni ngumu zinazosimamia urejeshwaji wa mikopo ili kutokuruhusu wanyonge wengi wanaotaka kukopa kujiimarisha kibiashara kukutana na vikwazo ambavyo ki msingi hawastahili kukutana navyo
‘’wafanyabiashara wakubwa wakikopa wanakopa kweli, imagine mtu amekopa bilioni 40, halafu amekataa kulipa na akibanwa anakimbilia mahakamani, bilioni 40 ukisema uwakopeshe mama lishe, au bodaboda, au vijana tu wa biashara za mtaji mdogo ungekopesha watu wangapi?, mkopo huo ungezalisha ajira ngapi?, mapato kiasi gani yangekusanywa?, lakini wapi, anachukua mfanyabiashara mmoja, anakwenda kununua V8 anatamba nazo mjini na akipita tunamuamkia ukifika wakati wa kulipa anakimbilia mahakamani’’. Aliongeza Crispin