Na Mwandishi Wetu
Naibu Waziri mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko ameielekeza Tanesco kuifumua menejimenti ya kampuni ya usambazaji wa vifaa ya Tanesco ETDCO na kuivunja bodi ya kampuni hiyo na kuunda nyingine baada ya kampuni hiyo kukithiri kwa vitendo vya wizi kunakoonekana kutokana na uzenmbe wa menejimenti ya kampuni hiyo
Dkt. Biteko amesema kuwa kama kuna taasisi inafanya hovyo kwenye wizara yake basi ni kampuni hiyo na kueleza kuwa madudu wanayofanya ni mengi na makubwa tofauti na sababu za uanzishwaji wake
‘’Kama kuna mtu ametutia nchi hii ni ETDCO, wamefanya vitu vya hovyo ambavyo mimi hata nikianza kuvisema hapa mtashika kichwa. Kule mafinga Mbeya wafanyakazi wao wame skim au ku plote wakaiba vifaa orodha ninayo hapa thamani yake milioni 35’’ amesema Dkt. Biteko
Dkt. Biteko amesima pia Mwezi wa tisa mwaka jana ETDCO wakiwa kwenye gari inaendeshwa na bwana mmoja Bryson kashombe walikuwa na vifaa vya wizi, walikamatwa na vifaa hivyo vyenye thamani ya shilingi milioni 69, hao ni watu wa ETDCO hao..tabora vile vile na kwenyewe kuna mtu mmoja foreman wenu na mtunza bohari walitoa vifaa bohari na kuvisafirisha kwa nia ya Kwenda kuviuza na kujipatia kipato binafsi vya shilingi milioni 61
‘’Mkoa mmoja wa Mbeya watu wa ETDCO 1.4 bilion vifaa vimeibiwa halafu watu wa namna hiyo unacheka nao tu, ETDCO kuna management, ETDCO kuna bodi, sasa jana nilisema meneja mkuu wa ETDCO aondolewe na nafurahi kwamba mmeshamuondoa, lakini bado menejimenti yote ya ETDCO lazima ifumuliwe yote, bodi ya ETDCO ambayo inateuliwa na bodi ya tanesco, waambie bodi hiyo waivunje waunde nyingine. Pili wale wote waliohusika na wizi wa vifaa hivi, wale waliofikishwa kwenye vyombo vya sheria waendelee wale ambao bado wapelekwe kwenye vyombo vya sheria lakini chukueni taratibu za ndani za kiutumishi kuwachukulia hatua watumishi wote wanaohusika na wizi wote uliofanyika’’ Ameongeza
Maamuzi hayo ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, yametokana baadhi ya watendaji wa TANESCO na kampuni zake Tanzu kushindwa kutekeleza maelekezo yake aliyoyatoa tarehe 2 Desemba 2023 ya kupambana na rushwa, kujenga mahusiano na wananchi wanaowahudumia, kuimarisha uaminifu ndani na nje ya Taasisi, kuacha visingizio na kutatua matatizo ya umeme yanaapojitokeza.
Dkt. Biteko ameagiza Watumishi wote wanaojihusisha na wizi ndani ya Shirika wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria ikiwemo kuwaweka pembeni katika Utumishi maana wao ni sababu ya watanzania kutokupata umeme wa uhakika.
Aidha ameelekeza wananchi waliotoa taarifa zilizopelekea kubaini wezi hao wa vifaa vya umeme kupewa barua za pongezi na fedha taslimu.
Dkt. Biteko amewataja baadhi ya watumishi wasio waaminifu wa TANESCO ambao wamekuwa wakishiriki kufanya wizi wa vifaa mbalimbali ikiwemo vyenye asili ya shaba, mafuta ya transfoma, vifaa vya miradi na ujenzi wa laini haramu ambazo hazipo kwenye mipango ya TANESCO huku mtumishi akiwa amelipwa pesa binafsi.
Vilevile, Dkt. Biteko ametoa onyo kwa viwanda na wanaofanya biashara ya vyuma chakavu nchini, kuwa wakikutwa na vifaa vya umeme watachukuliwa hatua kali za kisheria na watu hao watachukuliwa kama wezi na si wanunuaji wa vifaa hivyo.
Ili kuimarisha utendaji wa TANESCO, Dkt. Biteko amesema kuwa kuanzia sasa kutakuwa na upimaji wa kazi mkoa kwa mkoa katika kila kipindi cha robo mwaka ambapo vigezo mbalimbali vitapimwa ikiwemo uhudumiaji wa wateja na kukatika mara kwa mara kwa umeme ambako muda mwingine kunatokana na uzembe wa kutochukua hatua kwa wakati.
Ameongeza kuwa, wale watakaoonekana hawana utendaji mzuri wa kazi watatafutiwa kazi nyingine.
Aidha, ameagiza Wakurugenzi na Mameneja wa Mikoa wa TANESCO kushirikiana na Wakuu wa Mikoa yote nchini katika kuimarisha ulinzi wa miundombinu ya umeme hasa katika kipindi hiki ambacho hali ya umeme inaendelea kuimarika na miundombinu hiyo ikihitajika kufikisha umeme kwa wananchi.
Dkt. Biteko pia ameagiza Kitengo cha Usalama ndani ya TANESCO kuendelea kuimarisha ulinzi wa vifaa vya umeme na kutofanya urafiki na wezi wa vifaa vya umeme.
Katika hatua nyingine Dkt. Biteko amesema kuwa kwa ujumla kazi nzuri inafanyika TANESCO akitolea mfano ufanyaji kazi wakati wa dharura umeimarika ikiwemo kurekebisha hitilafu mbalimbali zinapojitokeza.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba amewataka watendaji wa TANESCO kujirekebisha wao wenyewe na wasisubiri kurekebishwa kwani yapo maeneo ambayo wanaweza kusimamia bila kusubiri viongozi ikiwemo kuwafanya watumishi walio chini kufanya kazi ya kuwahudumia wananchi.
Amesema kuwa, maelezo yote yaliyotolewa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati atayasimamia ipasavyo.
Pia Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. James Mataragio ameweka msisitizo kwa Watendaji wa TANESCO kuwa lazima wabadilishe taswira ya Shirika hilo kwa wananchi kwa kuhakikisha kuwa wanatoa huduma bora.
Baadhi ya Watendaji wa TANESCO kwenye kikao hicho wamekiri kuwa taswira ya Shirika hilo kwa wananchi bado inahitaji kuboreshwa ili kuweza kuaminika zaidi kwa wananchi ikiwemo taarifa mbalimbali zinazotolewa na Shirika hilo