Wawekezaji wa ndani na nje ya nchi na wenye kampuni za uwakala wa utalii wametakiwa kujitokeza kuwekeza katika sekta ya utalii hasa kanda ya kusini hususani katika Hifadhi ya taifa ya Katavi.
Wito huo umetolewa Machi mosi, 2024 na Mhifadhi Mkuu, Utalii na Mipango Kanda ya Kusini, Jonathan Kaihura mbele ya wanahabari waliotembelea hifadhi zilizoko kusini mwa Tanzania kujionea vivutio ndani ya hifadhi hizo.
Moja ya sababu ya kutolewa wito huo hasa kwa hifadhi ya Katavi ni kuwapo kwa vivutio vya kutosha lakini havina msukumo wa kutosha kwa wawekezaji ambao ndio chachu ya kuvutia watalii.
Hifadhi ya Katavi tunavyo vivutipo vingi na vizuri na tumeweza kuona upekee wa hifadhi zilizoko kusini mwa Tanzania, zipo fursa nyingi za uwekezaji hasa katika fursa za ujenzi wa mahoteli, nyumba za kulala wageni pamoja na uwekezaji mazao ya utalii,” amesema Kaihura.
Na Kwa upande wake, Mhifadhi Mwandamizi wa Hifadhi ya Taifa Katavi, Manendo Maziku amesema kwa sasa hifadhi ya Katavi inaye wakala mmoja wa utalii anayeleta watalii hasa wakati wa kiangazi ila kipindi cha masika husitisha shughuli za kuleta watalii.
“Hatuwaiti tu watu wanaokuja kutalii, tunawaita hata wawekezaji wanaotaka kuja kuwekeza waje wawekeze, tunayo maeneo ya uwekezaji mazuri mwekezaji akija tutamuonyesha kuwa kuna hili na hilii yeye atachagua eneo lipi kulingana na chaguo lake.
Atafuata utaratibu wa kwetu wa namna ya kufanya uwekezaji ndani ya hifadhi na huyu anakuwa ni mmoja wa wadau wetu muhimu wa kuuza utalii wa hifadhi ya Katavi amesema Maziku”,
amesema mkakati wanaoutekeleza ni wa kujitangaza kupitia vyombo mbalimbali vya habari ikiwemo Mpanda FM na nyinginezo.
Mbali na kutumia vyombo hivyo vya habari kujitangaza amesema wanahamasisha makundi mbalimbali katika mkoa wa Katavi kujikusanya pamoja na kwenda kutalii katika hifadhi hiyo.
Ameongeza kuwa Miongoni mwa vivutio vikubwa vilivyopo katika hifadhi hiyo ni pamoja na kuona kwa urahisi makundi makubwa ya viboko, mamba, tembo, nyati na wanyama wengine.
“Mara nyingi katika hifadhi nyingine viboko huonekana wakiwa nje ya maji nyakati za usiku lakini ndani ya hifadhi hii wanyama hao huonekana hata mchana tena wakiwa katika makundi makubwa.
Tabia ya viboko kuonekana mchana inawawezesha wageni kuwaona kwa ukaribu bila kuzongwa na msongamano wa watu wengi wenye magari yao amesema Maziku”,
Hifadhi ya Katavi ni ya tano kwa ukubwa baada ya hifadhi za Mwalimu Nyerere, Ruaha, Serengeti na Burigi Chato.
Mbali na kuwa na makundi makubwa ya wanyama pamoja na ndege ina sifa ya kuwa na maeneo ya wazi na tambalale yaliyojaa nyasi tupu bila miti huku maeneo mengine yakiwa yamefunikwa kwa vichaka na misitu.
“Tuna eneo la wazi la Katisunga, Paradasi, mbuga ya chada na mbuga nyeupe, pia tuna safu za milima ya Lyamba lya mfipa, safu zinapendezesha hifadhi yetu,” amesema Maziku
Na kuongeza kuwa ndani ya hifadhi wanalo ziwa Katavi ambalo ni mahususi kwa utalii wa kuvua samaki (Spot fishing).
Kwa wanaotaka kutembelea hifadhi ya Katavi amesema inafikika kwa nyakati zote iwe Masika au kipindi cha kiangazi, na inatumia njia ya barabara na anga.