ULINZI shirikishi ni ushirikishwaji wa jamii nzima na wadau wa masuala ya usalama katika kubaini , kuzuia na kutatua uhalifu na kero mbalimbali za uhalifu katika jamii kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi.
Jukumu la kutambua maeneo dhaifu kiusalama, mianya na vishawishi vya uhalifu Ni la wote , likishirikisha vyombo vya Dola , Kama polisi na Serikali kwa ujumla, lakini pia Serikali za mitaa na wadau mbalimbali na jamii kwa ujumla.
Dhana ya ulinzi Ni kwa mujibu wa sheria na katiba ambapo, ibara ya 145 na 146 ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977.
Inaeleza Katika majukumu ya Serikali za mitaa , watu wanapaswa kushiriki Katika shughuli zote za maendeleo ikiwemo kutekeleza sheria ya ulinzi na usalama Katika maeneo yao.
Jamii utambue kuwa, panapokuwa na kikundi Cha wananchi, waliojiunga kwa ajili ya kutoa ulinzi katika maeneo yao, Jeshi la polisi Lina wajibu wa kuwapa mafunzo mbalimbali ya kuzuia uhalifu pamoja na kudumisha Amani.
Hawapaswi kujichukulia sheria mkononi, au kukiuka sheria za nchi katika ukamataji au namna ya ukamataji wa wahalifu au watuhumiwa wa uhalifu.
Vikundi vya ulinzi shirikishi vinapaswa kuwa na nia moja ya kutunza amani ya nchi na kutoa ulinzi wa mahali na endapo watakamata wahalifu, hatua moja wapo iwe kuwakabidhi katika vituo vya polisi kuwezesha sheria ichukue mkondo wake kwa mujibu wa taratibu.
Akizungumza katika gazeti hili kueleza mipango ya kulinda na kuendeleza ulinzi shirikishi, Mkaguzi wa Kata ya Makumbusho, Inspekta wa Polisi, Hussein Mchange, alisema amejipanga kikamilifu kulinda na kuendeleza ulinzi shirikishi.
Alisema mimi pamoja na wenzangu tumedhamiria kupambana na uhalifu katika eneo letu kuhakikisha amani inatawala pamoja na kutekeleza maagizo ya viongozi wetu kuanzia ngazi ya wilaya, mkoa, kanda maalumu hadi taifa.
“Tuna mipango mingi lakini moja kubwa ni kuhakikisha nakuwa na askari wa ulinzi shirikishi wa kutosha katika mitaa yote sita inayounda Kata ya Makumbusho” alisema
Aliongeza; “Mitaa hiyo ni Mchangani, Kisiwani, Mbuyuni, Sindano, Minazini na Mtaa wa Makumbusho walinzi wenye weledi wa kazi, nidhamu na ufanisi wenye tija kwenye kazi ya ulinzi wa watu na mali zao kwenye mitaa yao”.
Kwa mujibu wa Inspekta Mchange, ndio maana katika hili kwa kufuaata dira ya Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa, ACP Ally Wendo tumeanzisha mafunzo ya walinzi shirikishi wa mitaa yote sita ya Kata ya Makumbusho.
Alisema katika mafunzo hayo, askari wanafundishwa kuhusu haki za binadamu, ukamataji, matumizi ya nguvu, sera ya polisi jamii na ukakamavu kuhakikisha jamii inakuwa na umoja na mshikamano mkubwa.
“Tulianza mafunzo Januari 29 hadi Februari 19 yamemalizika ambapo lengo la mafunzo hayo ni kutoa uelewa na elimu kwa wananchi. Kushirikiana na Wenyeviti wa Serikali za Mitaa” alisema
Aliongeza; “Wananchi na wadau wengine ndani ya mitaa kuwawezesha walinzi shirikishi vifaa vya kazi kama vile reflector, fulana, tochi na filimbi ili viwasaidie kwenye utendaji wao”.
Inspekta Mchange alisema wamepanga kuhakikisha wanaendelea kuwasimamia kwa karibu katika utendaji wao wajihisi wapo pamoja na Polisi pamoja na kuwafanya wajiamini zaidi kwenye kila wanalolifanya.
“Mimi kama polisi kata natekeleza sera ya jeshi la polisi ya kuishirikisha jamii
katika kutatua kero za uhalifu katika maeneo yao. Katika sera ya ushirikishwaji
jamii ndipo inapozaliwa falsafa ya polisi jamii ambapo ndani yake kuna miradi
kadhaa yenye lengo la kutanzua kero za uhalifu na wahalifu katika jamii” alisema.
Alieleza; “Mojawapo ni ulinzi shirikishi ambapo lengo ni kushirikiana na jamii katika kujilinda dhidi ya uhalifu na wahalifu, mimi kama polisi kata kwenye hili
nimejiwekea lengo la kuvitunza, kuvilinda na kuendelea kuvijengea uwezo vikundi vya ulinzi shirikishi vilivyopo katika kata”
Inspekta Mchange alisema lengo la kufanya hayo ni kusaidia Polisi Jamii iwe na mafanikio na kuwajenga walinzi shirikishi kuwa na uwezo na uweledi wa kupambana na uhalifu ndani ya jamii.
“Kupitia mradi wa ulinzi jirani mimi kama polisi naishirikisha jamii katika kuwapa elimu namna gani ya majirani katika mitaa yangu wanaweza kuwa na mawasiliano na ushirikiano wa kupeana taarifa” alisema
Alieleza; “Endapo kuna viashiria vya uhalifu katika maeneo hayo ambapo mwisho wa siku taarifa hii itanifikia mimi polisi kata ama viongozi wa mashina au mitaa ili wasaidiwe katika kukikabiri kiashiria hicho”.
Pia, alisema kutoa elimu ya ukatili wa kijinsia katika mitaa ya kata yangu ili jamii iwe na uelewa wa swala zima la ukatili wa kijinsia na wauchukie kwakua ni makosa chini ya sheria zetu.
Kuendelea kuhamasisha jamii katika mitaa ya kata yangu waendelee kujiunga na vikundi vya ulinzi shirikishi ambapo kupitia vikundi hivyo, jamii itajilinda yenyewe wakati wote.
“Na mimi kama polisi kata ntawajengea uwezo kama mtaalamu wa masuala ya usalama kwenye kata yangu. Mimi kama polisi kata naendelea kutekeleza falsafa ya huduma bora kwa wateja ambapo natambua huduma bora kwa wateja ni chachu ya kuboresha ubia wa kiutendaji baina yangu na jamii” alisema
Alisema “Kupitia hilo najenga imani ya jamii kwangu na kupitia imani yao naweza kupata taarifa zitakazo nisaidia kutanzua kero ya wahalifu na uhalifu pamoja na kutekeleza kauli mbiu ya ushirikishaji jamii”
Kwa mujibu wa Inspakta Mchange, kauli mbiu ni POLISI JAMII KWA USALAMA WETU NA MAENDELEO YETU ambapo wamenuia kuitumia kwa nguvu kutokana na kata hiyo kuwa na waraibu wa dawa za kulevya.
“Dawa za kulevya yana athiri vijana kama nguvu kazi ya taifa na chanzo cha uhalifu na wahalifu. Naendelea kutoa elimu wakati wote ninapokutana na makundi mbalimbali ya vijana kama bodaboda na wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kupitia mipango ya polisi” alisema
Alisema mipango hiyo ni pamoja na “POLISI NA WATOTO” na “MPANGO WA MICHEZO KWA VIJANA KATIKA KUZUIA NA KUPAMBANA NA UHALIFU” inayosaidia kuwawezesha kutambua madhara na athari za madawa ya kulevya kwao.
“Kwa vijana ambao wameathirika kwa uraibu tunaishirikisha familia kwa pamoja tuwashauri vijana hao wajiunge na vituo vya waraibu wapate tiba ya Methadone ambapo kwenye kata yangu tumepakana na hospitali ya Mwananyamala ambapo kunapatikana tiba hiyo” alisema
Pia, alisema tunatumia mpango wa kuzuia uhalifu wa FAMILIA YANGU HAINA MHALIFU NA ULINZI JIRANI pamoja na kushirikiana na jamii kupata taarifa fiche za wahalifu wanaojishughulisha na uuzaji wa dawa za kulevya katika kata yangu.
MTENDAJI, DIWANI WAFUNGUKA
Kwa upande wake, Afsa mtendaji kata ya makumbusho Suzana Mseti alisema wanalipongeza Jeshi la Polisi kwa kazi kubwa wanayoifanya ya ulinzi shirikishi na kuleta matokeo bora.
“Ulinzi shirikishi ni mkubwa na umekuwa na mafanikio makubwa yenye maendeleo, Hii ni hatua mojawapo yenye kulinda amani na utulivu kwa wananchi”alisema
Diwani Kata ya Makumbusho, Mohamed Ally Mohamed alimpongeza Inspketa Mchange kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuleta maendeleo makubwa kwa wananchi.
“Tunampongeza sana Inspekta Mchange kwa kuwa mstari wa mbele na kuleta maendeleo, amekuwa msikivu na mtu anayependa kushirikisha watu hususan vijana na kuibeba agenda ya Polisi Jamii kwa umakini mkubwa” alisema
Naye, Mwenyekiti Mtaa Sindano, Selemani Mohamed Yusuph alisema katika mtaa wao matukio ya uhalifu yamepungua kutokana na juhudi kubwa zinazochukuliwa na Polisi Kata.