- >>Kwa buku tano tu unalala hifadhini
- >>Msosi unaanzia shilingi elfu moja mia tano
- >>Waliokuwa wanaogopa kuhofia gharama kubwa watolewa hofu, wakaribishwa
Na Mwandishi, MOROGORO
Watanzania wanaotaka kwenda kutalii hifadhini na kusita kufanya hivyo wakihofia gharama kubwa za kulala hotelini wawapo hifadhini wametolewa hofu hiyo kutokana kuwepo kwa malazi mazuri yanayomilikiwa na TANAPA ambayo bei zake ni nafuu
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na wanahabari waliotembelea hifadhi ya Taifa mikumi mhifadhi mkuu wa hifadhi hiyo Kamishina Msaidizi wa Uhifadhi Agustine Masesa na Mhifadhi Msaidizi Herman Mtei wamewataka watanzania wakafurahie maisha hifadhini bila hofu ya gharama.
“Kama mlivyoona hapa tuna vyumba vinavyoanzia shilingi elfu tano, tunavyo pia vya elfu 23 kwa mtu mmoja ambayo hii unapata na chai ya asubuhi kizungu wanaita breakfast”- amesema Masesa
Masesa ameongeza kuwa hata gharama za vyakula ukiwa hifadhini humo ni nafuu sana kwani vyakula vinaanzia shilingi elfu moja mia tano
“Ukiwa na buku jero unafika sehemu ya kulia chakula na unapata msosi bila shida yoyote, lazima watanzania wajue kuwa gharama sio kubwa kabisa na inawezekana kuja kufurahia maisha ” ameongeza Masesa
Kwa upande wake Mtei amesisitiza kwa wanaopenda vinywaji vya kileo na laini kuwa bei ni ile ile waliyoizoea mtaani na kuongeza kuwa kuna baadhi ya maeneo mtaani bei za vinywaji huwa ghali kulinganisha na hifadhini
“hapa bei ya vinywaji ni nafuu sana, unapata bia kwa elfu mbili tu kama uko nje, soda elfu moja na hata maji unanunua kwa gharama za kawaida “- amesisitiza Mtei
Kwa kipindi kirefu dhama imejengeka kuwa ni gharama kubwa kulala katika hifadhi za Taifa na hivyo kuwafanya watu kutamani kwenda kutembelea hifadhi hizo lakini wanaogopa gharama
Kufahamika kwa gharama hizi kwa wananchi kutasaidia kuimarisha na kuongeza idadi ya watalii wa ndani wanaotembelea vivutio mbalimbali vilivtopo nchini.