Kwa maneno yake mwenyewe, Ndala amesisitiza:
“ACT Wazalendo haiwezi kuendelea kuvunja Katiba hadharani huku ikiwanyima haki wanachama wake wanaokirekebisha.”
Dar es Salaam, 3 Septemba 2025 – Mgogoro wa ndani ya ACT Wazalendo umeingia hatua mpya baada ya Monalisa Joseph Ndala, mwanachama wa mkoa wa Dar es Salaam na Katibu Mwenezi wa chama hicho, kuwasilisha malalamiko rasmi kwa Msajili wa Vyama vya Siasa. Ndala ameliomba ofisi hiyo kuchukua hatua kali na za kinidhamu kwa kile anachodai ni mwenendo wa chama chake kuvunja Katiba na Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura 258

Katika barua yake ya malalamiko, Ndala ametaja mambo mawili makuu yaliyomfanya kuchukua hatua hiyo ikiwemo:
- Uteuzi tata wa Bw. Luhaga Mpina – Ndala anadai kuwa chama kiliingiza na kumteua Mpina bila kufuata taratibu za kikatiba, jambo analoona linadhoofisha uhalali wa misingi ya chama.
- Kufutwa kwake uanachama kinyume cha taratibu – Tawi la Mafifi, Iringa Mjini lilitoa barua ya kumbukumbu ACT/IR/IRM/KH/MF/001 likidai kuwa amepoteza sifa za uanachama. Ndala anapinga vikali akisema: yeye si mwanachama wa tawi hilo, hakupatiwa nafasi ya kujitetea, na zaidi tawi hilo halina mamlaka ya mwisho ya kumvua uanachama
Katika malalamiko yake, Ndala ameeleza:
“Chama kimehusika katika mchakato wa kumuingiza na kumteua Bw. Luhaga Mpina bila kufuata utaratibu wa kikatiba na kanuni za chama. Uteuzi huo umefanyika kinyume na taratibu zinazotambulika na zinazolindwa na sheria ya usajili wa vyama vya siasa.”
Aidha, akizungumzia hatua ya Tawi la Mafifi – Iringa Mjini lililotangaza kumvua uanachama, Ndala amesema:
“Mimi si mwanachama wa tawi hilo, na hata kama ningekuwa mwanachama bado sikupata nafasi ya kusikilizwa wala kujitetea. Tawi halina mamlaka ya mwisho ya kumvua mwanachama uanachama.”
Ndala amesisitiza kuwa haki yake ya kikatiba ya kukata rufaa imepuuzwa na kwamba barua ya kufutwa kwake uanachama “imenukuu vifungu visivyo na maelezo mahsusi”
Uamuzi huu wa Ndala unaweza kuathiri taswira ya chama kinachojitambulisha kama “mbadala wa kisiasa chenye demokrasia ya kweli.” Malalamiko haya yanazua maswali juu ya uongozi wa ndani, taratibu za uteuzi wa viongozi, na namna chama kinavyoshughulikia haki za wanachama wake.

Wachambuzi wa siasa wanaona hatua ya Ndala si tu inalenga kulinda nafasi yake kama mwanachama, bali pia ni ujumbe kwamba chama hicho kinapaswa kurejea kwenye misingi ya Katiba yake na kuheshimu demokrasia ya ndani.
Ndala ameomba Msajili wa Vyama vya Siasa kuchukua hatua tatu kuu:
- Kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya ACT Wazalendo.
- Kufuta uamuzi wa Tawi la Mafifi dhidi yake.
- Kuelekeza chama kuhakikisha uteuzi na usimamizi wa wanachama unafuata sheria na Katiba.
Kwa maneno yake mwenyewe, Ndala amesisitiza:
“ACT Wazalendo haiwezi kuendelea kuvunja Katiba hadharani huku ikiwanyima haki wanachama wake wanaokirekebisha.”
Kwa sasa macho ya wanachama na wananchi yanaelekezwa kwa Msajili wa Vyama vya Siasa kuona iwapo atachukua hatua kali dhidi ya ACT Wazalendo au la! jitihada za kuzipata pande zinazohusishwa na mgogoro huo zinaendela