KILIMO cha vitunguu saumu nchini Tanzania kinapata umaarufu kwa kasi kama biashara ya kilimo yenye matumaini, kutokana na ongezeko kubwa la mahitaji ya ndani na katika soko la kimataifa.
Vitunguu saumu, kwa harufu na ladha yake kali na ya kipekee, uwezo wake kitiba, na kutumika kwake katika matumizi mbalimbali ya mapishi, vimejipatia nafasi muhimu katika majiko ya kaya nyingi za Kitanzania.
Umaarufu wake haujaja tu kwa bahati, bali ni ushahidi wa matumizi yake lukuki na faida zake nyingi za kiafya. Hali mbalimbali za hewa na udongo wenye rutuba nchini Tanzania hutoa mazingira bora kwa kilimo cha vitunguu saumu.
Kuanzia milima ya kijani ya Arusha na Kilimanjaro hadi tambarare za Morogoro na Singida, maeneo mbalimbali ya kijiografia ya nchi yetu yanachangia katika ukuaji wa zao hili muhimu. Kila eneo lina faida za kipekee; iwe ni baridi kali la milimani linalonenepesha punje na kuzipa ladha yake ya ukali au udongo wenye rutuba usiotuamisha maji unaostawisha na kuleta tija kwenye vitunguu saumu.
Kwenye makala hii, tutaangalia mambo muhimu kwenye kilimo cha vitunguu saumu nchini Tanzania, na kutoa mwongozo kamili kwa wakulima wenye uzoefu na wale wapya kwenye uwanja huu.
Tutazidadavua mada muhimu kama vile kuchagua aina za vitunguu saumu zinazofaa kwa eneo lako, kutekeleza mbinu bora za kilimo, na kugusia mienendo ya soko la vitunguu saumu.
Ukielewa misingi hii, utakuwa na maarifa ya kutosha kufanikiwa katika kilimo cha vitunguu saumu, kukidhi mahitaji ya soko, na hatimaye kuchangia kwenye ukuaji wa sekta ya vitunguu saumu nchini. Uwe mkulima mzoefu anayetaka kuangazia fursa kwenye mazao mengine au mkulima mpya anayetaka kuanza safari ya kilimo, kitabu hiki kinalenga kukupa maarifa ya msingi na mwongozo wa vitendo utakaohitaji ili kufanikiwa katika kilimo cha vitunguu saumu.
Ambatana nasi tunapoibua fursa na changamoto kwenye kilimo hiki, na uone jinsi utakavyoweza kuifanya kuwa biashara yenye faida na mafanikio. Hali ya hewa na maji au mvua Vitunguu saumu vinapendelea hali ya joto la kati ya nyuzi 12 – 24 za sentigredi. Wastani wa mm 500 – 600 za mvua zinatosha kwa msimu wote wa uzalishaji.
Unyevu anga na au mvua nyingi sana huvutia magonjwa ya ukungu. Kwa mantiki hii vitunguu saumu vinafaa zaidi kulimwa katika maeneo yoyote ambayo yanamvua chache na uhakika wa maji ya kumwagilia. Udongo na Mwinuko Vitunguu saumu hupendelea udongo wenye rutuba usiotuamisha maji na wenye pH ya kati ya 5.5 – 7.5.
Vitunguu saumu vinapendelea maeneo yenye miinuko ya kati ya mita 1000 hadi 2500 kutoka usawa wa bahari. Udongo wa tifutifu kichanga (sandy loam) unafaa zaidi kwa vitunguu saumu kwa kuwa unapitisha hewa vizuri na hautuamishi maji. Udongo wa mfinyanzi mzito hauruhusu vitunguu kujitanua na hutunza maji kwa muda mrefu sana hivyo kuozesha vitunguu.
Mikoa inayolima vitunguu saumu Tanzania Kwa hapa Tanzania vitunguu saumu vinalimwa zaidi katika mikoa ya Mbeya, Iringa, Manyara, Arusha, na Kilimanjaro. Mikoa mingine ni Morogoro (Mgeta) na Singida. Maeneo ya nyanda za juu yana miinuko stahiki , hali ya hewa ya baridi na mtawanyiko mzuri wa mvua (vitu) ambavyo huchagiza sana ustawi wa vitunguu saumu hasa vya hardneck.
Tuna Mwongozo wa kilimo biashara wa zao hili, kwanini usiupate ili upate maelezo mengi yenye kina zaidi? K w e n y e m w o n g o z o u t a p a t a mapendekezo maalum kutoka kwetu juu ya aina bora na kiasi sahihi cha mbegu, mbolea na viuatilifu. Pamoja na uchambuzi wa gharama za uzalishaji katika kila hatua na faida utakayopata.
Vitunguu saumu vipo vya aina mbili: Vitunguu saumu vya shingo laini (soft[1]neck garlic) na Vitunguu saumu vya shingo ngumu (hard-neck garlic). Aina hizi zote zinalimwa hapa nchini.
Vitunguu saumu vya shingo laini (Soft-neck Garlic) Hivi ni vitunguu saumu ambavyo shina lake au shingo yake ni laini na ina tabia ya kuanguka (au kulala) vitunguu vinapokomaa. Shina la vitunguu hivi huwa ni laini hata baada ya vitunguu kuvunwa na inaweza kusokotwa kama kamba.
Dalili ya kukomaa vitunguu hivi ni kulala au kuanguka kwa shina lake. Mfano wa vitunguu saumu vya shingo laini ni Egyptian white garlic na Chinese white garlic. Sifa za vitunguu saumu vya shingo laini Shingo yake ni laini kiasi kwamba inaweza kukunjwa au kusokotwa kama kamba. Vina punje (cloves) ndogondogo nyingi (12 – 25) zilizopangwa katika safu nyingi ndani ya tunguu (bulb).
Kutokana na uwingi wa punje, matunguu (bulbs) yake ni makubwa kuliko ya hardneck. Vina ladha na harufu yenye ukali wa wastani, inayofaa kwa matumizi ya kawaida ya nyumbani. Ladha yake ni laini kuliko ile ya vitunguu saumu vya shingo ngumu. Ni rahisi kulima na vinahifadhika kwa muda mrefu zaidi: kati ya miezi 10 hadi 12.
Vinastawi katika maeneo yenye hali za hewa mbalimbali, kuanzia baridi hadi joto la wastani, na vinaweza kupandwa katika maeneo ya kitropiki na uwanda wa kati.
Vitunguu saumu vya shingo ngumu (Hard-neck Garlic) Hivi ni vitunguu ambavyo shina lake (au shingo yake) ni ngumu kama mti na hubakia imesima hata vitunguu saumu vinapokomaa. Dalili ya kukomaa kwa aina hii ni majani kubadilika rangi kuwa kahawia na kuanza kukauka. Sifa za vitunguu saumu vya shingo ngumu Vitunguu saumu vya hardneck hutoa shina linaloitwa scape.
Shina hilo linaanzia kwenye kitako cha kitunguu na kupanda hadi kwenye shingo, na hivyo kuvipa jina la “hard-neck – shingo ngumu”. Shingo yake ni ngumu na hubaki imesimama kama mti, na hutoa maua kwa juu. Vina punje (cloves) chache kubwa (4 – 12) zilizopangwa katika mduara mmoja ndani ya tunguu (bulb) kuzunguka shingo ngumu (scape). Matunguu yake ni madogo kuliko ya softneck.
Vina ladha na harufu k ali zaidi inayopendwa na wapishi wengi. Ni vigumu kulima na vinahifadhika kwa muda mfupi zaidi: kati ya miezi 4 hadi 8. Vinapendelea zaidi katika maeneo yenye baridi kali, na hivyo kustawi vizuri zaidi maeneo ya nyanda za juu. Hali hii ya baridi ndio hufanya vitengeneze punje (cloves) nene zenye ladha na harufu kali.