MWANZONI mwa miaka ya 1990, klabu ya Simba ilibahatika kusajili wachezaji wengi chipukizi ambao baadaye wakifanikiwa kuwa mahiri na kuiletea mafanikio klabu hiyo yenye maskani yake makuu Kariakoo, mtaa wa Msimbazi.
Miongoni mwa wachezaji hao aliyeipatia mafanikio klabu hiyo ni mpachikaji mabao, George Lucas au ‘Gaza’ kama wapenzi wa soka nchini walivyozoea kumwita.
Nyota huyo ambaye alikuwa na umbo la kawaida la kimichezo, pamoja na uwezo mkubwa aliokuwa nao wa kumiliki mpira chenga za maudhi, uwezo mkubwa wa kupachika mabao na mashuti makali yaliyowafanya magolikipa wa timu pinzani kupata wakati mgumu kudaka michomo yake.
Nyota huyo pamoja na kujulikana akiwa na klabu ya Pilsner ya Dar e s Salaam, lakini umarufu wake ulizidi kuongezeka mwaka 1992 wakati aliposajiliwa na Simba na kuwa miongoni mwa wachezaji wa kutegemewa wa klabu hiyo.
Nyota huyo baada ya kujiunga na Simba, miongoni mwa wachezaji aliowakuta ni Edward Chumila (marehemu), Idd Seleman ‘Meya’ (marehemu), Abuu Omari, Malota Soma ‘Ball Juggler’, Twaha Hamidu ‘Noriega’, Bakari Iddi na Itutu Kigi ‘Road Master’.
Ikumbukwe kwamba mwaka 1991, Simba haikufanya vizuri katika ligi, mbali na kutwaa taji la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, hivyo mwaka huo wa 1992, Simba iliongeza nguvu kwa kusajili wachezaji wengine ambao waliingia na George Lucas.
Miongoni mwa wachezaji ambao walisajiliwa mwaka huo wa 1992 pamoja na Lucas ni Mohamed Mwameja, Kasongo Athumani, Fikiri Magoso, Hussein Marsha, Nico Kiondo, Abdul Mashine, Alfred Kategile na Michael Paul ‘Nylon’.
Kutokana na umahiri wake mkubwa aliokuwa akiuonesha uwanjani, wapenzi wa soka nchini walimbatiza jina la ‘Gaza’ wakimfananisha na mshambuliaji wa zamani wa timu ya Taifa ya England, Paul Gascoigne Gaza.
Mwaka huo wa 1992, Lucas alikuwa ni miongoni mwa wachezaji walioiwezesha Simba kutwaa taji la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, baada ya kuifunga Yanga mabao 6-5. Mabao hayo yalipatikana kwa mikwaju ya penalti, baada ya kutoka sare ya bao 1-1, katika muda wa dakika 120.
Fainali hiyo ilichezwa kwenye Uwanja wa Aman mjini Zanzibar. Mwaka huo huo wa 1992, Simba pamoja na kutwaa Ubingwa wa Soka Afrika Mashariki na Kati, pia Lucas alikuwa ni miongoni mwa wachezaji walioiwezesha timu hiyo kutwaa taji la Jamhuri ya Muungano.
Novemba 27, 1993, Lucas alikuwa katika kikosi cha Simba, kilichotinga katika fainali ya Kombe la CAF, lakini ilifungwa na Stella Abidjan ya Ivory Coast mabao 2-0. Julai 2, 1994, Lucas alikuwa katika kikosi cha Simba, kilichoifunga Yanga mabao 4-1, mechi ya mzunguko wa pili ya Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara (sasa Ligi Kuu), iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam (sasa Uhuru).
Pia Lucas kutokana kuwa katika kiwango bora cha soka, mwaka huo wa 1994, alichaguliwa kwa mara ya kwanza kuchezea timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars iliyokuwa ikinolewa na Salum Madadi aliyekuwa akisaidiana na Paul West Gwivaha(marehemu).
Miongoni mwa wachezaji aliokuwa nao katika timu hiyo ya taifa, ni Stephen Nemes, Mwanamtwa Kihwelo, Alfonce Modest, Mustapha Hoza, George Masatu, Hussein Marsha, Nteze John, Juma Amiri, Madaraka Seleiman, Said Mwamba ‘Kizota’ (marehemu) na Edibily Lunyamila.
Kikosi hicho cha Taifa Stars, baada ya kuchaguliwa kilitwaa taji la Ubingwa wa Chalenji baada ya miaka 20, kwani mara ya mwisho Stars ilitwaa taji hilo mwaka 1974. Lucas akiwa na klabu ya Simba, miaka miwili mfululizo 1994 na 1995, alikuwa ni miongoni mwa wachezaji walioiwezesha timu hiyo kutwaa taji la Ubingwa wa Soka Tanzania Bara.
‘Gaza’ baada ya kucheza kwa mafanikio makubwa hapa nchini, mwaka 1995 mwishoni, Lucas alitimkia nchini Oman kucheza soka la kulipwa katika klabu ya Oman SC ambayo alikaa nayo msimu mmoja tu, kabla ya kurudi nchini na kustaafu kucheza soka ya ushindani mwaka 2003 akiwa na klabu ya Kariakoo FC ya Lindi.