KONGAMANO la Nishati la Afrika lililofanyika nchini Tanzania tarehe 27-28 Januari 2025 linatoa fursa muhimu kwa nchi yetu na bara zima katika kuimarisha ajenda ya maendeleo endelevu kupitia upatikanaji wa nishati safi na ya uhakika.
Licha ya Tanzania kuwa na rasilimali kubwa za kuzalisha umeme wa jua na upepo, bado tunategemea vyanzo vya nishati visivyo endelevu kama mafuta na kuni, jambo linalohitaji mabadiliko ya haraka.
Katika kongamano hilo, Mhandisi Manala Tabu Mbumba alisema kuwa Afrika imebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi za nishati jadidifu, kama vile jua, upepo, na maji. Hata hivyo, uwekezaji katika sekta hii bado ni mdogo, hali inayohitaji juhudi za kushirikiana kikanda na kuvutia uwekezaji wa ndani na nje katika teknolojia za nishati safi.
Mhandisi Manala aligusia changamoto kubwa ya upatikanaji wa nishati vijijini, akisema kuwa zaidi ya asilimia 50 ya watu barani Afrika hawana umeme, na sehemu kubwa ya watu hao ni kutoka vijijini.
Alisisitiza umuhimu wa kutumia teknolojia ya mini-grids na off-grid inayotumia vyanzo vya nishati jadidifu ili kuwafikia wananchi wa vijijini kwa bei nafuu.
Pia, alizungumzia umuhimu wa ushirikiano wa kikanda katika miradi ya nishati, akisisitiza kwamba miradi kama mabomba ya gesi, usambazaji wa umeme wa kikanda, na sera zinazowezesha biashara ya nishati baina ya nchi zitasaidia kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza upatikanaji wa nishati.
Kwa upande mwingine, Mhandisi Manala alisisitiza haja ya kuwekeza katika teknolojia za kisasa na kukuza wataalamu wa ndani katika sekta ya nishati.
Alisema serikali, sekta binafsi, na taasisi za elimu zinapaswa kushirikiana kuhakikisha kuwa tuna nguvu kazi inayoweza kutumia, kutengeneza, na kudumisha teknolojia mpya za nishati.
Katika kujibu changamoto za mabadiliko ya tabianchi, alieleza kuwa sekta ya nishati ina mchango mkubwa katika kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi na kulinda mazingira.
Aliongeza kuwa Afrika, ikiwa ni mojawapo ya mabara yanayoathirika zaidi na mabadiliko ya tabianchi, inapaswa kuwa kinara wa kuonyesha mfano wa kupunguza utegemezi wa mafuta na kuhamia kwenye nishati safi.
Mhandisi Manala pia alisisitiza kwamba ili kufanikisha ajenda ya nishati safi, ni muhimu kuvutia wawekezaji kwa kutoa motisha kama punguzo la kodi na usaidizi wa kifedha kwa miradi ya nishati safi.
Pamoja na mambo mengine mtaalamu huyo Aliitaka Tanzania kutumia kongamano hili kama fursa ya kuonyesha hatua inazochukua katika kuimarisha sekta ya nishati, ikiwa ni pamoja na miradi mikubwa ya umeme wa maji na juhudi za kukuza nishati jadidifu.
“Namshukuru Mungu kwa kuwa Mhe.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kututeulia kiongozi mxhapa kazi Mhe.Dk.Doto Biteko Naibu Waziri mkuu wa Tanzania na Waziri wa Nishati kunwwka eneo kama hili muhimu naamini atalimudu na kuhakikisha Watanzania tunatumiza ndoto zetu, Bila nishati endelevu, maendeleo endelevu ni ndoto,” aliongeza.
Hivyo, tunapaswa kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa nishati safi kwa maendeleo ya Taifa letu na bara letu la Afrika kwa ujumla.