FIKRA ZA MJASIRIAMALI
MWANZONI mwa wiki kulikuwa na mkutano wa siku mbili kujadili mustakabali wa umeme ndani ya Bara la Afrika, ambapo ulishirikisha wakuu wa nchi zilizomo ndani ya bara hili, pamoja na wakuu wa taasisi mbalimbali za kimataifa.
Tunasema Afrika imejikomboa yenyewe kuhusu suala la nishati, baada ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Afrika Kuhusu Nishati kuhitimishwa, huku wakuu waliohudhuria wakitia saini ‘Azimio la Dar’ litakalowezesha Waafrika milioni 300 kufikishiwa huduma ya umeme ifikapo mwaka 2030.
Mkutano wa wakuu wa nchi na viongozi wengine a vyombo vya fedha, ulimalizika lakini kabla ya hapo ulitanguliwa na mawaziri wa kisekta kabla ya viongozi hao kuhitimisha mkutano huo.
Tulimsikia Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan akisema Tanzania ni moja kati ya nchi 12 zitakazozindua mpango mahususi wa kitaifa kuhusu nishati. Kupitia mpango huo unatarajiwa kuongeza kasi ya kuunganisha umeme nchini hadi kufikia asilimia 72 ifikapo mwaka 2030.
Fahamu akiwa ameibeba ajenda ya nishati salama mkononi mwake, Rais Dkt. Samia alivunja na kuandika rekodi ya aina yake kwa kuwa Rais wa kwanza nchini aliyewahi kupokea idadi kubwa ya wakuu wa nchi 25 kujai kwa pamoja nchini.
Nchi ambao wakuu wake walishiriki ni Algeria, Comoro, Liberia, Lesotho, Botswana, Kenya, Ghana, Gabon, Sierra Leone, Ethiopia, Sudan, Malawi, Zambia, Somalia, Guine Bisau, Burundi, Mauritania, Kongo Brazzaville, Madagascar, Libya, Nigeria, Djibouti na Gabon.
Mbali na hilo, Afrika imeelezwa kupiga hatua katika suala zima la upatikanaji nishati ya umeme toka nyingi kati ya hizo zipte uhuru miaka ya 1960.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko amesema baada ya kupata uhuru, nchi za Afrika zimepiga hatua kubwa katika kuzalisha na kusambaza umeme kwa wananchi wao.
Dk. Biteko alisema hayo jana kwenye Mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika ‘Mission 300’ uliokuwa unafanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es salaam
“Inasikitisha kwamba idadi ya Waafrika ambao hawana umeme inakadiriwa kuwa milioni 571.kutokana na hali hii, Mkutano huu uliitishwa, ukiwa na lengo kubwa lakini linaloweza kufikiwa la kuongeza upatikanaji wa umeme kwa angalau watu milioni 300 barani Afrika katika miaka mitano ijayo
“Kama ilivyobainishwa katika Ajenda ya Afrika 2063 na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), leo Dar es Salaam inayo heshima ya kuwa mwenyeji wa wajumbe kutoka Afrika na kwingineko, wakihudhuria Mkutano huu muhimu unaolenga kuimarisha azma ya Afrika ya kuipatia bara hili nishati.
“Baada ya kupata Uhuru mwaka 1960, nchi za Afrika zimepiga hatua kubwa katika kuzalisha na kusambaza umeme kwa wananchi wao. Tanzania ilikuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 21 pekee wakati wa Uhuru, kwa sasa nchi ina uwezo wa kuzalisha megawati 3,160.”
Kwangu nishati ni kila kitu kwani inakwenda kumkomboa mjasiriamali ambaye anapambana, ili tu awe na maisha bora na hilo linatimia kutimiza ndoto za wengi kutaka kuwa na maisha yanayofanana na utu wa binadamu.
Mjasiriamali yoyote atakaa na kufurahi azimio lililopitishwa, sasa ni mwanzo wa kuitoa Afrika katika giza lililo kuu.
![](https://jamvilahabari.co.tz/wp-content/uploads/2025/01/fa361582-c812-4457-905d-257c4cef28c9.jpg)
![](https://jamvilahabari.co.tz/wp-content/uploads/2025/01/MJASIRIAMALI-14-1024x576.png)