WIZARA ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kushirikiana na Taasisi ya CRDB Foundation zimekubaliana kushirikiana katika kutoa elimu kwa wajasiriamali kutumia teknolojia ya kidijitali na upatikanaji wa masoko kwa kuzingatia ushirikishwaji wa kijinsia.
Hayo yamebainika wiki iliyopita , katika kikao kilichowakutanisha Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Amon Mpanju na uongozi wa CRDB Foundation.
Walikutana ili kujadili mpango kazi wa utekelezaji wa mradi wa kukuza na kuimarisha ujumuishaji wa kifedha kwa wanawake na wafanyabiashara ndogondogo, kwa kutumia teknolojia ya kidijitali na upatikanaji wa masoko kwa kuzingatia ushirikishwaji wa kijinsia unaofadhiliwa na CRDB Foundation.
Mpanju ameipongeza Taasisi ya CRDB Foundation kuwa na Hati ya Makubaliano (MoU) na Wizara ambayo imeweka utaratibu mzuri wa ushirikiano na utekelezaji wa program hiyo ili kuweza kufikialengo lake.
Kwa upande wao Taasisi ya CRDB Foundation imepongeza hatua ya wizara kushirikiana nao katika kutoa elimu ya fedha, ujasiriamali, mitaji wezeshi, na utambuzi na usajili wa wafanyabiashara ndogondogo.