NAIBU Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mwanaidi Ali Khamisi amewataka Wanawake, Vijana, Watu Wenye Ulemavu mkoani Tanga na maeneo mengine ya nchi kuchangamkia fursa ya kuomba mikopo ya wafanyabiashara ndogondogo inayotolewa na Serikali kupitia Benki ya NMB kwa lengo la kuwainua wananchi kiuchumi.
Naibu Waziri Mwanaidi amesema hayo hivi karibuni, wakati akizungumza wakati wa mafunzo ya elimu ya utolewaji wa mikopo ya 10%, matumizi ya nishati safi, elimu kuhusu ukatili wa kijinsia na uwezeshaji wanawake kiuchumi.
Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua zaidi za kuongeza fursa ya uwezeshaji wananchi kiuchumi na kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalu myenye dhamana ya kuratibu na kusimamia Wafanyabiashara Wadogo (MACHINGA), imesaini Mkataba na Benki ya NMB ya utoaji mikopo kwa ajili ya wafanyabiashara hao.
“Niwaombe Wanawake, Vijana, Watu Wenye Ulemavu wa mkoani Tanga na maeneo mengine ya nchi kuchangamkia fursa hii kujisajili na kupata vitambulisho vya kidijitali kwaajili ya Wafanyabiashara ndogondogo ili muweze kupata mikopo hiyo, fikeni Halmashauri hususani katika Ofisi za Maendeleo ya Jamii ili wawape utaratibu wa kujisajili” amesema Naibu Waziri Mwanaidi.
Aidha, amesisizitiza kwamba Serikali imeendelea kusimamia utekelezajii wa Sera ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ya Mwaka 2004 ambayo ilianzishwa kwa lengo la kuhakikisha wananchi wa natambuana kutumia fursa mbalimbali za kiuchumi zinazopatikana nchini.
Sera hiyo imewezesha kuanzishwa kwa Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi ambalo linawaleta wanawake pamoja na kujadili fursa zilizopo, namna ya kuzifikia na kuweka mipango ya kutatua changamoto zao kiuchumi.