WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake, na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima amewahimiza wananchi kuchangamkia fursa za kiuchumi zinazotolewa na Serikali, ikiwemo mikopo yenye lengo la kuwawezesha wananchi kuinuka kiuchumi.
Dkt. Gwajima alitoa wito huo hivi karibuni, ambapo alisisitiza umuhimu wa wafanyabiashara ndogondogo kujisajili kwenye mfumo rasmi ili waweze kupata mikopo.

Dkt. Gwajima amewahimiza wananchi kufuatilia taarifa mbalimbali zinazotolewa na Serikali kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, ili watambue na kutumia fursa za kiuchumi zinazopatikana. Amesisitiza umuhimu wa wafanyabiashara ndogondogo kujisajili kwenye mifumo rasmi ili kupata vitambulisho vya kidijitali, hatua ambayo itawawezesha kufikia mikopo yenye riba nafuu.
“Ndugu wananchi, nimegundua wengi wenu hamfuatilii taarifa zinazotolewa na Serikali na hivyo mnashindwa kupata taarifa sahihi za uwezeshaji wa wananchi kiuchumi. Naomba mjitahidi kufuatilia taarifa hizi, kama mnavyofuatilia habari za michezo, ili mtambue fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali na kuzitumia kujikwamua kiuchumi,” alisema Dkt. Gwajima

