KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii imeipongeza Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kuratibu kwa ufanisi utekelezaji wa Programu ya Tanzania ya Kizazi chenye Usawa (GEF) na Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake (WDF).
Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Fatma Toufiq wakati wa uwasilishaji wa utekelezaji wa majukumu ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Januari 22, 2025 jijini Dodoma.
Toufiq amesema wizara imekuwa nguvu kuhakikisha jamii inapata maendeleo kupitia fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali katika sekta mbalimbali nchini jitihada hizo zinasadia kutatua changamoto za wananchi na kuwainua kiuchumi.
“Wizara mnafanya kazi kubwa sana kuhakikisha jamii inapata maendeleo na ustawi, tunaiona kazi yenu kamati itaendelea kuwaunga mkono ili kufikia maono ya rais ya kuanzisha wizara hii ya mambo ya maendeleo na ustawi wa jamii,” amesema Toufiq
Akiwasilisha taarifa mbele ya Kamati ya Bunge, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima amesema, wizara itaendelea kuratibu utekelezaji wa Programu mbalimbali kuhakikisha zinafikia malengo yake na kuunga mkono jitihada za Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuleta maendeleo na kuboresha ustawi wa wananchi.