NA MWANDISHI WETU
WAKATI ikiwa ni kilio kikubwa juu ya ‘‘Chuma Ulete’, kitu ambacho kinawakondesha wajasiriamali wengi, baadhi yao wanaamini kuna watu wanaishi maisha ya anasa na starehe bila kufanya kazi.
Wanaamini kuwa nguvu ya “Chuma Ulete’ imesababisha madhara makubwa kwao, lakini imewafaidisha wao na wanawajua baadhi ya watu ambao wanatembea na ‘bidhaa’ hiyo mfukoni ili tu mambo yao yaende sawa.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wachuuzi na wafanyabiashara walidai ‘Chuma Ulete’ ni aina ya mazingaombwe yanayofanywa na baadhi ya watu wanaoishi kwa kutofanya kazi kwa kuwaibia wengine kwa njia za Imani isiyofaa.
Mmoja kati ya wafanyabiashara hao, Sakina Abdallah anayeoka mikate katika eneo la Tandika, Dar es Salaam alisema kitu kinchoitwa ‘Chuma Ulete’ kinawatesa mno na kinawafanya wawe maskini wa kutupwa.
“Yaani ni balaa tupu, kama mimi nilipo hapa naweza kujikuta nimeuza sana lakini ikifika jioni sina kitu, unajiuliza hela imekwenda wapi kumbe watu wa “Chuma Ulete’ wameshakupitia,” alisema.
Katika mahojiano maalumu na uchunguzi uliofanywa na JAMVIMEDIA GROUP kwa kina ulibaini mambo mengi yaliyo na simulizi ya kusisimua juu ya kitu kinachoitwa ‘Chuma Ulete’ na kimesambaa miongoni mwa jamii ya Watanzania walio wengi.