NA MWANDISHI WETU
WAZIRI wa Madini,Anthony Mavunde,amebainisha kuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imenunua tani 2.6 za dhahabu inayochimbwa na kusafishwa hapa nchini ikiwa ni sehemu ya juhudi za kukabiliana na changamoto ya upungufu wa fedha za kigeni, kuboresha akiba ya fedha za kigeni, na kuimarisha thamani ya shilingi ya Tanzania.
Mavunde ameyasema hayo,jijini Dodoma, wakati akiwasilisha taarifa kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, taarifa inayohusu utendaji wa viwanda vya kusafisha dhahabu nchini kwa kipindi cha Machi hadi Desemba 2024 pamoja na mwenendo wa ununuzi wa dhahabu unaotekelezwa na BoT.
Kwa mujibu wa Waziri Mavunde,Oktoba Mosi 2024, Tume ya Madini ilitoa tangazo linalowataka wachimbaji na wafanyabiashara wa dhahabu kutekeleza takwa la Kifungu cha 59 cha Sheria ya Madini Sura 123, ambalo linawataka kutenga asilimia 20 ya dhahabu na kuiuzia BoT kupitia viwanda vya usafishaji vilivyoidhinishwa.
โMheshimiwa Mwenyekiti, Tangu kutolewa kwa tangazo hilo hadi Januari 21, 2025, BoT imefanikiwa kununua tani 2.6 za dhahabu kutoka kwa wachimbaji wa kati, wachimbaji wadogo, na wafanyabiashara wa dhahabu.
Thamani ya dhahabu hiyo ni zaidi ya shilingi bilioni 570 kwa mujibu wa bei ya soko la dunia ya tarehe 22 Januari 2025โ amesema,Mavunde.
Halikadhalika, Waziri Mavunde amesisitiza kuwa, kupitia mpango huo wa BoT, lengo la Serikali ni kuifanya Tanzania kuwa moja ya mataifa 10 yenye hifadhi kubwa ya dhahabu barani Afrika kwa ustawi wa taifa.
Ongezeko la Mapato ya Serikali
Kwa upande wa mapato, Waziri Mavunde amebainisha kuwa, mwenendo wa ukusanyaji wa mrabaha kwa upande wa madini ya dhahabu umeendelea kuimarika na kwamba kuanzia Julai 1, 2024 hadi Desemba 31, 2024, Serikali iliingiza shilingi bilioni 400.22 kutokana na mauzo ya kilogramu 34,826.75 za dhahabu, ikiwa ni ongezeko la asilimia 5.55 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2023, ambapo kilogramu 32,995.54 ziliuzwa na Serikali kupata shilingi bilioni 278.86.