NA ASHA SEKEFU
KAULI ya Kocha wa Yanga, Saed Ramovic, ya kudai Ligi Kuu Tanzania Bara imewaibua wadau mbalimbali ambao wamesema, anatakiwa kuomba radhi kwani kusema hivyo ni kuikosea heshima nchi na soka kwa ujumla.
Mmoja wa wadau hao, Mecky Mexime alidai, Ramovic ametoa kauli ya ukakasi na haifai, kwani kushindwa kwa Yanga kufanya vizuri katika michuano ya Kimataifa asichanganye na mambo mengine.
“Akiri kwamba timu yake imeshindwa kufuzu kucheza robo fainali, lakini asiwe na visingizio vingi vya kutaka kuonesha ligi ni dhaifu, anapaswa kuadhibiwa na kuomba radhi,” alisema.
Ramovic alidai, moja ya sababu zilizofanya timu yake ishindwe kutinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ni udhaifu wa Ligi ya Tanzania, ambayo haina timu nyingi ngumu na zenye ubora, nguvu na kasi, ambazo zingesababisha timu yake kuzoea hali hiyo.
“Tunapaswa kuwa wakweli kwamba ligi ya hapa Tanzania, ugumu unaokutana nao unapocheza dhidi ya timu nyingine za Tanzania si wa kiwango kikubwa sana. Ukiona ligi za Algeria, Afrika Kusini, Morocco, Tunisia, tunahitaji nguvu hiyo ya juu ili kushindana na tuweze kuzoea hali hiyo.
“Ukali wa ligi ya Tanzania, ni mdogo sana ukilinganisha na nchi hizo, wao ligi yao ni ngumu na kila timu kali sana, tunahitaji ugumu kama wa ligi hizo ili tushindane,” alisema kocha huyo.
Alisema urahisi wa kupata ushindi katika michezo ya Ligi Kuu hauwajengi, badala yake unawafanya kudumaa na kupata shida wanapocheza na timu ambazo zinatoka kwenye ligi zenye ushindani, akisema suala hili likifanyiwa kazi haitokuwa faida kwa Yanga tu, bali kwa timu zote nchini ambazo zitakwenda kucheza mechi za kimataifa.