Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) unatarajiwa kufanyika kwa siku mbili mfululizo, tarehe 18 na 19 Januari 2025, jijini Dodoma.
Mkutano huu ni tukio kubwa na la kihistoria kwa chama hicho, ukilenga kujadili masuala muhimu ya chama na taifa kwa ujumla.
Aidha Moja ya ajenda kuu za mkutano huu ni uchaguzi wa kura za ndiyo, utakaofanywa na wanachama wa CCM ili kumchagua mtu atakayechukua nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, nafasi iliyoachwa wazi baada ya Abdulrahman Kinana kujiuzulu. Uchaguzi huu unatarajiwa kuwa wa kipekee, wenye ushindani wa kistaarabu, na wenye kuzingatia demokrasia ndani ya chama.
Hata hivyo Mkutano huu umefungua fursa nyingi za kijamii na kiuchumi jijini Dodoma. Biashara zimeongezeka maradufu, huku hoteli na nyumba za wageni zikijaa kupita kawaida, hali ambayo haijawahi kushuhudiwa katika mikutano mingine iliyopita.
Aidha, huduma za usafirishaji zimeimarika kwa kasi kubwa. Wasafiri kutoka ndani na nje ya nchi wanatumia ndege, mabasi, na Treni ya Umeme ya SGR kufika Dodoma. Ongezeko hili la wageni limeonyesha mchango mkubwa wa miundombinu ya kisasa inayosimamiwa na Serikali ya Awamu ya Sita, ikiongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Tofauti na mikutano mingine ya CCM, mwaka huu mkutano umeonyesha uwezo wa kuunganisha shughuli za chama na maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Hali ya Dodoma kwa sasa ni ya shauku kubwa, ikionyesha jinsi mkutano huu unavyoimarisha mshikamano wa chama na kuleta faida kwa jamii nzima.
Mkutano huu siyo tu tukio la kisiasa bali pia ni chachu ya maendeleo ya kitaifa kupitia fursa mbalimbali zinazotolewa kwa wananchi na wawekezaji.