Mshambuliaji mahiri wa Norway, Erling Haaland, ameweka rekodi mpya baada ya kusaini mkataba wa miaka tisa na nusu na klabu ya Manchester City.
Mkataba huo mkubwa, ambao utaweka mustakabali wake Etihad hadi mwaka 2034, umethibitishwa kuwa moja ya mikataba mikubwa katika historia ya soka.
Tangu alipojiunga na klabu hiyo miaka mitatu iliyopita kwa dau la pauni milioni 51, Haaland ameonyesha uwezo wa hali ya juu kwa kufunga mabao 111 katika mechi 126 katika mashindano yote.
Kwa mujibu wa taarifa za Mail Sport, mshambuliaji huyo atapokea mshahara wa pauni 400,000 kwa wiki. Hata hivyo, masharti mawili ya kuachiliwa yaliyokuwapo kwenye mkataba wake wa awali yameondolewa, hatua inayotafsiriwa kama kumaliza uwezekano wa kuhamia LaLiga, ambapo awali kulikuwa na tetesi za kuvutiwa na klabu ya Real Madrid.
Hali hii inaonyesha mabadiliko makubwa ya msimamo wa Haaland, huku mkataba wake mpya ukimhakikishia kuendelea kuwa sehemu muhimu ya mabingwa hao wa Ligi Kuu ya England.
Licha ya mafanikio haya makubwa ya kibiashara na kiufundi, Manchester City inakabiliwa na changamoto kubwa nje ya uwanja. Klabu hiyo imeshtakiwa kwa ukiukaji wa kanuni 130 za fedha za Ligi Kuu na mashtaka mengine 15 yameongezwa baadaye.
Hata hivyo Adhabu zinazoweza kutolewa kwa klabu hiyo ni pamoja na faini, kukatwa pointi, au hata kushushwa daraja iwapo watapatikana na hatia. Hukumu ya kesi hiyo, ambayo ilikamilika kusikilizwa Desemba 6, inatarajiwa kutolewa mwezi Februari mwaka huu.
Hata hivyo, wadau wa soka wanasema mkataba mpya wa Haaland ni ishara ya kujitolea kwa City kujenga msingi imara wa muda mrefu licha ya changamoto zinazowakabili. Mashabiki wa soka kwenye mitandao ya kijamii wameonyesha hisia mchanganyiko, huku baadhi wakiona ni uamuzi wa kijasiri wakati huu wa hali ya sintofahamu kuhusu hatma ya klabu hiyo.