wakati mwingine si lazima uwe ‘Tomaso’ ili uweze kuamini na kuona kile kinachofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita katika kuvutia wawekezaji hapa nchini, kwani yote yanajidhihirisha wazi bila ficho lolote lile.
Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeandika historia kwa kuvutia uwekezaji mkubwa zaidi katika mwaka 2024, ambapo miradi 901 ilisajiliwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).
Mfano ulio dhahiri ni kwa miradi ya maendeleo ambayo imevutia jumla ya mitaji ya Dola za Kimarekani bilioni 127, kiwango ambacho hakijawahi kufikiwa tangu kuanzishwa kwa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).
Hayo yalidhihirishwa pia na Waziri wa Nchi, Mipango na Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo, ambaye alisema, mafanikio hayo ni ushahidi wa dhamira thabiti ya Rais Samia katika kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.
“Hii ni miradi mingi zaidi kuwahi kusajiliwa, na Rais Samia ameonyesha maono makubwa tangu ahadi yake aliyoitoa Aprili 2021 alipohutubia Bunge,” alisema Profesa Mkumbo.
Prof. Mkumbo alitanabaisha kuwa mafanikio hayo pamoja na mambo mengingine yametokana na maboresho makubwa ya kisera na kisheria yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita, amabayo ni pamoja na kuimarisha mifumo ya kidijitali, kupunguza urasimu, na kutoa vivutio vya kikodi kwa wawekezaji.
Aidha, juhudi za Rais Samia katika ushawishi wa makampuni makubwa kupitia ziara za kimataifa na mikutano zimeimarisha imani ya wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Pia uanzishwaji wa ofisi mpya ya TIC Kanda ya Kaskazini, mkoani Arusha, umetajwa kuwa kichocheo kikubwa cha uwekezaji kwenye sekta ya utalii ambapo aliseifu jitihada za wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na mamlaka za mikoa kwa kuhamasisha biashara na uwekezaji katika maeneo yao.
Hivyo, wakati Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan akiendelea kujipambanua vyema katika utendaji wake kazi, imebainika miradi ya maendeleo iliyosajiliwa mwaka jana inatarajiwa kuzalisha ajira 212,293 kwa Watanzania.
Hii ni kutokana na miradi 901 iliyosajiliwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kuanzia Januari hadi Desemba 2024 kulinganisha na miradi 526 katika kipindi hicho mwaka 2023.
Miradi hii iliyosajiliwa mwaka jana inatarajiwa kuzalisha idadi hiyo ya ajira kwa Watanzania, kulinganisha na ajira 137,010 zilizozalishwa mwaka 2023.
Mikoa iliyoongoza kwa kuvutia uwekezaji ni Dar es Salaam, Pwani, Arusha na Dodoma.
Prof. Mkumbo alisema, Dar es Salaam ilifanikiwa kusajili miradi 356, Pwani ikisajili miradi 166, Arusha miradi 64 na Dodoma ikiwa na miradi 47 ambayo ni sawa na asilimia 70.3 sawa na jumla ya miradi 633 iliyosajiliwa katika mikoa hiyo.
Alitaja sekta tano zinazoongoza kwa kusajili miradi mingi ya uwekezaji kuwa ni uzalishaji viwandani, usafirishaji, ujenzi wa majengo ya biashara, utalii na kilimo.
“Mwaka 2024 tunaweza kuutangaza ni mwaka bora zaidi katika sekta ya uwekezaji Tanzania, kutokana na ukweli kwamba ndio mwaka ambao TIC ilisajili miradi mingi zaidi ya uwekezaji (miradi 901) tangu Tanzania ianzishe kituo hiki,” alisema Prof. Mkumbo.
Alisema kuwa, mafanikio hayo ni ushahidi wa dhamira thabiti ya Rais Dkt. Samia katika kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.
“Hii ni miradi mingi zaidi kuwahi kusajiliwa na Rais Samia ameonyesha maono makubwa tangu ahadi yake aliyoitoa Aprili 2021 alipohutubia Bunge,” alisema.
Katika kuonyesha hatanii katika hili, juzi Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alisisitiza Tanzania itaendelea kuwa nchi ya kutegemewa katika kukuza ushirikiano wa kimataifa, kuchochea ukuaji wa kiuchumi, na kudumisha amani na usalama barani Afrika na duniani kwa ujumla.
Rais Dkt, Samia aliyasema hayo wakati wa hafla maalum aliyoiandaa kwa ajili ya Mabalozi wanaowakilisha nchi zao nchini Tanzania na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa yaliyopo nchini.
Hafla hiyo huandaliwa kila mwanzo wa mwaka kutakiana heri, kuzungumzia maendeleo nchini na kueleza vipaumbele vya Tanzania ikiwemo kikanda na kimataifa.
Pamoja na mambo mengine, Rais Dkt. Samia ameeleza kuwa pamoja na kuadhimisha miaka 60 ya Muungano, mwaka 2024 Tanzania ilishuhudia ukuaji wa kiuchumi wa asilimia 5.4 ambao umechagizwa na kukua kwa uzalishaji, uwekezaji na utalii.
Rais Dkt. Samia ameeleza kuwa nchi ilipiga hatua za kihistoria katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya reli na nishati inayoenda kuleta mageuzi ya kiuchumi nchini Tanzania.
Hivyo Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweka alama isiyofutika katika historia ya maendeleo ya Tanzania. Uwekezaji wa mwaka 2024 siyo tu unachochea uchumi wa Taifa, bali pia unatoa matumaini mapya kwa Watanzania kuhusu mustakabali wa maendeleo yao.