NA MWANDISHI MAALUM
SAMAKI ni lishe miongoni mwa Watanzania wengi, pia wafanyabiashara wamekuwa wakijipatia kipato kizuri kwa kufanya biashara ya samaki.
Mbali na samaki kutumika kutengeneza vitoweo mbalimbali pia huunda sampuli ya mafuta yanayotumika kama lishe kwa watoto.
Biashara ya kufuga samaki ina faida nzuri kwa sababu soko lake ni pana na wala sio la kuhangaika, ilimradi mkulima azalishe samaki wa kutosha.

Mradi huu unaweza kumsaidia mkulima akaanzisha kukuza aina nyingine ya mimea kama vile mawele ambayo hutoa lishe kwa samaki.
Nilifanya ufuatiliaji wa karibu kuhusu suala la ufugaji wa samaki kwa mtindo wa kisasa katika baadhi ya maeneo kadhaa, iwe kwa watu binafsi au taasisi mbalimbali na kujifunza jinsi watu wanavyoweza kufaidika.

Badala ya kutegemea vidimbwi na mabwawa kama inavyofanywa na wafugaji kwa sasa, uvumbuzi mpya umefanya ufugaji wa samaki kuwa rahisi ikiaminika kuwa changamoto sio upatikanaji wa maji bali kufanya shughuli nzima ipasavyo.
Ijapo mfumo wa samaki unahitaji maji yaliyotulia, mkulima anahitaji kuwa na samaki watatu mmoja awe wa jike na mwingine wa kiume. Haijalishi yule wa tatu ni wa kike au kiume, kwa sababu kazi yake ni kushinikiza uzalishaji.
INAVYOKUWA
Unayachukua mayai ya samaki kisha yakachanganywa na chembe chembe za uzalishaji kutoka kwa samaki wa kiume, ambao huchukua masaa 48 kuzalisha samaki wadogo (fingerlings).
Samaki wadogo huchukua siku tano kabla ya kulishwa vyakula vya kawaida vilivyochanganywa na unga na viungo muhimu vya majani.

Ufugaji wa samaki kupitia mbinu za kisasa unaweza kusaidia kwenye utunzaji wa mali asili, pasipokuwa na uchafuzi wa maji wala mazingira wanamokulia viumbe hawa
Mfugaji anaweza kufuga samaki kwenye kipande kidogo cha ardhi, ambayo kufikia sasa ni teknolojia ya kisasa ambayo ni nyepesi kujifunza.
Fursa hii ya kisasa inawalenga wakulima wadogo wanaopatikana mijini, wenye ari ya kuwekeza kwenye mradi wenyewe.

Huu ni ufugaji ambao tunaweza kusema unajumuisha makasha makubwa au matangi safi kuhifadhi samaki, hata wakulima wanaoishi kwenye maeneo kame wanaweza kufuga samaki.
Labda matanki haya yalikuwa yakitumia kuhifadhi maji lakini yakabadilishwa kufugia samaki, ambapo kila tanki hubeba takriban lita 4,000 ya maji.
Lakini tambua mtu mmoja anatosha kuwafuga samaki mradi maji na hewa zinapenya kwenye muundo mzima wa mikondo ya maji na hewa safi.
Kinachohitajika ni kuhakikisha samaki wanapata lishe kwa wakati ufaao na kila tanki linaweza kulinda samaki aina ya tilapia wakubwa wenye kilo zaidi ya 25 na unaweza kuanza na samaki wadogo 200 kwenye tanki moja.

Matanki haya ya kisasa yasipungue kina cha mita mbili, bwawa la tanki lisiwe fupi kwenye kina kwani samaki wanahitaji maji ya kina kirefu ili waweze kukua kwa haraka.
Kilimo hiki kinaweza kumsaidia mkulima kuweka samaki wengi kwenye nafasi ndogo, ambapo maji yanayoingia na kutoka kupitia mikondo ya paipu hupishana.
Maji ya kufugia samaki lazima yawe baridi na haishauriwi kuwafuga ndani ya maji ya chumvi. Inatakiwa kiwango cha chumvi ndani ya maji kupimwa ili kubaini endapo samaki wanaweza kuishi salama bila kupata maradhi au kupambana na chumvi nyingi ya mwilini.

Mfugaji atumie eneo tulivu ambalo halina migogoro, lenye maji ya kutosha lakini pia atengeneze bwawa la kuhifadhi maji ili maji yasipungue wakati wa ufugaji na anaweza kuwafuga samaki wadogo sawia na wale wakubwa ili kupunguza shinikizo la samaki kupungua baada ya kuwauza na ikiwa utazingatia hatua zote zinazohitajika kwenye mradi wa kufuga samaki changamoto za ufugaji huwa zinapungua.
Kwanza wafugaji kuchunguza ubora wa maji, ikiwa mfugaji atashindwa kubadilisha maji ya kufugia samaki wake kwa wakati ina maana kuwa samaki wataanza kuugua.
FANGASI
Ugonjwa mkubwa unaosumbua samaki ni ule wa fangasi ambao hutokana na maji machafu, ambapo magamba huanza kumtokea samaki.
Ili mfugaji aweze kuanza ufugaji wa samaki ni muhimu kupata kibali cha matumizi ya maji kwa mfano kupata kibali kutoka kwa serikali kwa sababu samaki ni tofauti na wanyama wengine.
Ili mkulima aweze kufuga samaki kibiashara mkulima anahitaji kuwa na mabwawa takriban sita ili uvunaji wa samaki usipunguze upatikanaji wa bidhaa hii muhimu sokoni.
Mkulima akiwa na bwawa moja hatuwezi kusema anafuga samaki bali anajifundisha tu kufuga samaki na ikiwa maji na hewa ya majini ni chafu samaki hupata wasiwasi na watajaribu kuhama na baadhi yao kufa.
Tiba ya haraka anayotakiwa kutoa mkulima anapopata baadhi ya samaki wameanza kupoteza maisha ni muhimu kusafisha bwawa kwa haraka.
Ikiwa mkulima si mzoefu pia anaweza kutafuta ushauri kutoka kwa mtaalam ili kujipunguzia hasara zinazoweza kuepukika.
