– ni Fatuma karume, Mwabukusi, Kambole, Tito Magoti na wenzao- walikimbilia CANADA kuishtaki Tanzania kupitia kampuni ya Twiga-Barrick wakitaka walipwe Mabilioni ya pesa
– Jaji wa Mahakama hiyo awatoa nishai, awaambia Mahakama Tanzania ziko huru na zinaweza kusikiliza kesi hiyo
– Fatma Karume aumbuliwa alipotaka mahakama hiyo iamini kuwa amevuliwa uwakili kwa sababu ya serikali badala yake akaambiwa amevuliwa kutokana na yeye kukiuka maadili
– Mwambukusi aambiwa hata CANADA wakili haruhusiwi kuongea na vyombo vya habari akiwa na joho la kiwakili linalotumika Mahakamani
– Ushahidi wa Tito Magoti nao wapigwa chini, waambiwa waheshimu mahakama na sheria
Na Mwandishi Wetu
MAHAKAMA Kuu ya Ontario nchini Canada imesema inatambua na kuuheshimu uhuru na uwezo wa mfumo wa Mahakama wa Tanzania katika kutoa na kusimamia haki.
Uamuzi huo umefikiwa katika kesi iliyofunguliwa na asasi ya kiraia ya ‘Mining Watch Canada’ kwa niaba ya wanavijiji 32 kutoka jamii zinazozunguka Mgodi wa Dhahabu wa North Mara. Awali, wakili wa wadai aliiambia mahakama kuwa hawakupeleka shauri hilo Tanzania kwa sababu mahakama zake si huru na kuwa kuna uwezekano wa wateja wao kutokutendewa haki, wakati upande wa utetezi ulibainisha kuwa mahakama za Tanzania ni huru.Kesi hiyo ya madai ilifunguliwa Novemba 23, 2022 na ‘Mining Watch Canada’ kwa niaba ya wanavijiji 32 wa Tanzania, ikidai kuwa mpango wa usalama wa Barrick kwa Mgodi wa North Mara unaotekelezwa na Jeshi la Polisi la Tanzania unawanyanyasa raia.
Aidha, madai hao yanaeleza kuwa mpango tajwa wa usalama umesababisha ukiukwaji wa haki za binadamu na vitendo vya ukatili vilivyofanywa na polisi, na kusababisha vifo, majeraha, na mateso kwa raia.Mjadala mkali ulitokea mahakamani hapo kuhusu uhalali wa Mahakama ya Canada kusikiliza shauri hili chini ya hoja ya ‘forum non conveniens’ (uhalali wa mahakama kusikiliza shauri).Lilikuwa jukumu la Barrick kuonyesha ugumu wa mahakama hiyo iliyochaguliwa na wadai kutekeleza wajibu wake.
Barrick pia ilipaswa kuonyesha kuwa mahakama mbadala ya Tanzania ilikuwa na nafasi bora zaidi kusikiliza kesi.
Hoja hii ilileta ushindani kati ya Ontario na Tanzania; kwamba ni mahakama ipi hasa inayostahili kusikiliza shauri hilo.Pande hizo, ziliwekeza nguvu kubwa katika kueleza faida na hasara za mahakama hizo na ipi ina nafasi nzuri zaidi ya kutenda haki katika kesi hiyo.
Katika malubano hayo ya kisheria, mfumo wa kisheria wa Tanzania ulimulikwa kwa kurunzi kali la uchunguzi kuhusu uwezo wake na majaji wake katika kutoa hukumu za haki. Wadai walitoa ripoti kadhaa za wataalamu katika jitihada za kuonyesha kuwa mfumo wa kisheria wa Tanzania haukuwa jukwaa sahihi la kusikiliza shauri lao, wakati Barrick ilitoa ripoti kadhaa za wataalamu kuonyesha kuwa ukosoajiwa wadai kuhusu mfumo wa Tanzania haukuwa na msingi na kwamba mfumo wake wa haki una uwezo wa kushughulikia kesi hii.Jaji Morgan alikubali ombi la Barrick la ‘forum non conveniens’, akisema mahakama za Tanzania zina nafasi nzuri zaidi kusikiliza shauri hilo kuliko Mahakama ya Ontario. Jaji alikataa madai kwamba mfumo wa Mahakama wa Tanzania ulikuwa na upungufu na kwamba mahakama za Tanzania kuna ‘ukiukaji wazi wa sheria za kimataifa na haki za msingi za binadamu’.
Jaji ameeleza mahakamani hapo kwamba madai ya watuhumiwa yanataka kutumia mahakama hiyo kama chombo cha kuanzisha mashambulizi kwa mfumo wa kisheria wa Tanzania. Aidha alitupilia mbali hoja ya wadai kwamba wangeweza kuwa na ugumu wa kifedha kupata wakili nchini Tanzania, akionyesha kwamba Tanzania kuna vituo vingi vya msaada wa kisheria ambavyo vimeonyesha uwezo wa kuwasadia wenye mahitaji.
Ili kuthibitisha madai yao kuhusu upungufu wa mahakama za Tanzania, wadai waliwatumia mawakili mashuhuri wa Tanzania; Fatma Karume na Boniface Mwambukusi, kama mashahidi wakati upande wa utetezi ulikuwa na Jaji Mkuu (mstaafu) Mohamed Chande Othman. Moja ya ushahidi uliopelekwa mahakamni hapo ni ripoti ya kitaalamu ya Jaji Mkuu Chande ambayo sehemu yake, inasema: “Kwa maoni yangu, yaliyotokana na uzoefu wangu wa muda mrefu kwa mahakama na ujaji mwenye uzoefu Tanzania, pamoja na uzoefu wa kimataifa niliopata, mfumo wa mahakama wa Tanzania ni wazi, umeandaliwa vizuri, na ni wa kiwango cha juu na unatoa haki isiyo na upendeleo kwa njia ya haki na inayofaa.
”Jaji Mkuu Chande alipohojiwa na mawakili wa upande wa mashtaka, alifafanua vyema jinsi mfumo wa Tanzania unavyofanya kazi kiasi kwamba baada ya hapo Jaji Morgan alibainisha katika hukumu yake kwamba:“…ni vyema kusema kwamba maelezo haya ya mfumo wa haki wa Tanzania yaliyotolewa wakati wa ‘cross examination’ (shahidi akihojiwa na upande wa mashtaka) yameueleza vizuri zaidi mfumo huo.
”Katika kuonyesha walakini mfumo wa sheria wa Tanzania, shahidi wa wadai, Fatma Karume, alishuhudia akisema kwamba amewahi kufungua shauri la kikatiba dhidi ya serikali hatua iliyosababisha ashtakiwe kwa makosa ya kitaaluma. Jaji Morgan amesema rekodi inaonyesha, hata hivyo, kwamba Fatma alipata adhabu kwa kuwa na tabia mbaya na matusi katika mawasilisho yake; ukosefu wa adabu kitendo ambacho mtu anaweza kukabiliwa na mashtaka ya nidhamu ya kitaaluma hata Ontario nchini Canada.
“Katika kusikiliza kwake kuhusu makosa, Fatma alishindwa kutoa ushahidi wowote katika utetezi wake; zaidi ya hayo, anadai kuwa alitukana wafanyakazi wa mahakama, yote haya yalisababisha kufukuzwa kwake.
“Ukweli kwamba Fatma alikuwa amefungua kesi ya kikatiba hapo awali, haikuwa chanzo cha matatizo yake ya kitaaluma,” amesema Morgan.
Vivyo hivyo, shahidi wa wadai, Mwabukusi ambaye ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), anasema alifungua kesimahakamani dhidi ya serikali kuhusu usimamizi wa bandari na kudai kwamba alikabiliwa na mchakato wa nidhamu ya kitaaluma kama matokeo ya hatia yake hiyo. “Rekodi inaonyesha, hata hivyo, kwamba Mwabukusi alifanya mkutano wa waandishi wa habari wakati kesi ilikuwa inasubiri huku akiwa amevaa mavazi yake ya mahakama, vitendo ambavyo vinakatazwa chini ya sheria za Tanzania,” amesema Jaji Morgan.
Wadai walidai kwamba mfumo wa mahakama wa Tanzania hauna uhuru kwa sababu Katiba ya Tanzania inatoa uhuru mwingi kwa serikali katika kuteua majaji na kupanga mishahara yao
Ameongeza kuwa ingawa Katiba ya Tanzania inampa Rais uwezo wa kuteua majaji, nguvu hiyo inatekelezwa tu baada ya ushirikiano na tume huru ya kisheria iliyoundwa na majaji waliopo.
“Utaratibu huu unatajwa kikatiba na hakuna Jaji aliyeteuliwa nje ya mapendekezo yaliyotolewa na tume,” amesema.
Akichambua ushahidi huo, Jaji Morgan amesema ingawa Deya anaweza kuwa na mtazamo wa kulinganisha wa kupendeza katika kulinganisha Tanzania na majirani zake kadhaa wa Afrika Mashariki, hana ujuzi wa kulinganisha Tanzania na Ontario au Canada. “Na hoja iliyopo mhakamani ni kulinganisha uhalali wa mahakama za Tanzania na Canada, kwani hayo ndiyo majukwaa yanayohusika,” amesema.
Jaji huyo ameeleza kuwa mfumo wa Tanzania ni kama ulivyo Canada ambako uteuzi wa majaji wa Mahakama Kuu za majimbo ni jukumu la kikatiba la serikali ya shirikisho chini ya kifungu cha 96 cha Sheria ya Katiba ya 1867.“Mchakato wa uteuzi ni suala la mamlaka ya Waziri Mkuu ambapo halazimishwi kushauriana na yeyote,” anafafanua Jaji Morgan katika hukumu yake.
Amesema chini ya Katiba ya Tanzania, Rais, kama ilivyoelezwa katika ushahidi wa kitaalamu mbele yake, anafanya jukumu sawa katika uteuzi wa majaji kama Waziri Mkuu wa Canada. Amesema Katiba ya Tanzania imeweka mfumo mzuri zaidi wa kuteua majaji kuliko Katiba ya Canada,” amesema Jaji Morgan.
Madai mengine yalikuwa ni kwamba wadai hawawezi kupata wakili wa kusikiliza kesi yao nchini Tanzania kwa wao ni masikini sana hawawezi kumudu gharama na kwamba mawakili wa Tanzania wamekusanyika mijini wakati wadai wako vijiji vya mbali.
Wakadai kwamba mawakili huogopa kushtakiwa katika ‘baraza la mawakili’ kama wakitetea kesi dhidi ya serikali.
Hata hivyo, ushahidi juu ya jambo hili unatolewa na Jaji Mkuu Chande, akisema kuna vituo vingi vya msaada wa kisheria nchini Tanzania ambavyo hutoa huduma wakati mwingine bure kwa niaba ya watu masikini.
Shahidi mwingine wa Barrick, mtaalamu wa msaada wa kisheria, Ulimboka Mwasomola, amesema kuna uwezekano mkubwa kwamba wadai wanaweza kupata uwakilishi wa ufadhili wa msaada wa kisheria nchini Tanzania.
Kuhusu ukosefu wa mawakili kuwatetea wadai, Jaji Morgan anasema: “Cha kushangaza, hakuna ushahidi kwamba yeyote miongoni mwa wadai amewasiliana na mawakili wengine au vituo vya msaada wa kisheria nchini Tanzania ili kujua gharama na hata kukubaliana kuhusu utaratibu wa malipo, au huduma za usaidizi au hata ‘pro bono’ kama zinaweza kupatikana.
“Hakuna yeyote ambaye amejitokeza kusema kwamba kesi hiyo ilikataliwa na wakili wa Tanzania au kituo cha msaada wa kisheria. Hiyo inaonekana kuwa ni upungufu muhimu katika rekodi, na kukosekana kwake kunafanya iwe vigumu kutathmini ukweli wa madai ya wadai kwamba uwakilishi wa kisheria wa ndani haupatikani kwao.”
Amesema kwa kuzingatia umbali wa Ontario (kutoka Tanzania) na ukweli kwamba mashahidi muhimu bila shaka wangeweza kukosekana, kesi hii kusikilizwa Tanzania ndiyo njia pekee ya kupata ushahidi wote muhimu kutoka pande zote mahakamani.