Kongamano la uwekezaji
jiji la Tanga kuibua fursa
L Mkurugenzi Mhandisi Hamsini awaita wafanyabiashara, wawekezaji kuchangamkia fursa zilizopo
L Asema uwepo wa miundombinu ya uhakika ya usafiri ikiwemo reli, barabara, anga na bahari chachu ya ufanyaji biashara
Na Mwandishi Wetu, Tanga
OKTOBA 26 na 27, ni siku ya mageuzi makubwa ya kiuchumi kwa wananchi wa Jiji la Tanga kutokana na kufanyika kwa kongamano kubwa la uwekezaji lililoanzishwa na ofisi ya jiji kwa ushirikiano na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Tanga.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Jiji la Tanga, Mhandisi Juma Hamsini alisema wamekuja na kongamano la kuufungua mkoa wa Tanga hususan jiji hilo ambalo lina historia kubwa kibiashara toka enzi za ukoloni.
Alisema Jiji la Tanga ni jiji la kimkakati kibiashara, lina fursa lukuki ikiwemo maeneo bora ya ardhi kwa ajili ya uwekezaji wa mambo mbalimbali ikiwemo michezo ya watoto, ujenzi wa hoteli za kitalii, kilimo, viwanda na mambo mengo.
“Tumeamua kuja na kongamano la kuwekeza Tanga ambalo watu zaidi ya 1000 watahudhuria. Kongamano lina dhima, dhamira ya kutangaza vivutio vya uwekezaji vilivyopo ndani ya halmashauri ya jiji hilo,” alisema
Aliongeza; “Tunania ya kuwakutanisha wafanyabiashara wa Tanga na wafanyabiasharta wengine kutoka nje ya jiji hilo. Nawaomba sana wafanyabiashara wajitokeze kwa wingi kuhudhuria kongamano hilo”
Alisema Mkoa wa Tanga una jumla ya watu 2,617,597 kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022. Tanga ni kati ya mikoa 31 ya Tanzania ambapo shughuli kuu ni uvuvi, kilimo na ufugaji.
“Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan imekuwa mstari wa mbele kutekeleza miradi lukuki ya maendeleo mkoani humo na kuweka mazingira bora ya uwekezaji kwa wananchi.” alisema
Alieleza; “Akiwa kama mtendaji wa halmashauri ya Jiji wamedhamiria kutangaza fursa zilizopo kwa wananchi waweze kuwekeza. Tumekuja na kongamano hili ambalo kwa namna moja au nyingine litakuwa na mafanikio makubwa”
Mhandisi Hamsini alisema uwepo wa fursa nyingi katika kila sekta ni moja ya mambo yanayopaswa kuungwa mkono na kila mpenda maendeleo mkoani humo kujitokeza kwa wingi katika kongamano la uwekezaji Tanga.
“Tanga ina kila kitu, kuna usafiri wa kila aina. Ukiwa Tanga ukitaka kwenda mkoa wowote Tanzania ni karibu. Ukitaka kwenda nchi ya jirani ya Kenya nayo ni karibu mno. Sasa tumeamua kuufungua mkoa” alisema
Kwa mujibu wa Mhandisi Hamsini, serikali imewekeza fedha nyingi za ukarabati wa bandari ya Tanga na kumeanza kuleta shehena nyingi za mizigo ambayo imeanza kutoa fursa ya uwepo wa wafanyabiashara kujenga bandari kavu.
“Tanga ni kitovu cha biashara, tuna maeneo tumetenga kwa ajili ya ujenzi wa bandari kavu, mahoteli, viwanja vya mpira, viwanda na mambo mengine mengi ambayo mwekezaji akija hana shida ya kushindwa kupata fursa” alisema
Alisema; “Tanga ni mkoa muhimu ambayo kila mfanyabiashara au mwekezaji anapaswa kuchangamkia fursa zilizopo kutokana na uwepo wa rasilimali nyingi na za kutosha pamoja na usafiri wa reli, barabara, ndege na hata maji.”
Kwa mujibu wa Mhandisi Hamsini, Tanga ni mkoa wa kimkakati wa viwanda una ardhi ya kutosha na yenye rutuba. Uwepo wa mazingira salama, miundombinu bora ya kuingia na kutoka ni chachu ya wawekezaji kwenda kuwekeza.
“Kauli yetu mbiu ni Tanga ni langu kuu la kibiashara kwa nchi za Afrika Mashariki. Hilo linatokana na upekee wake ambao umekuwa ni rahisi kwa wafanyabaishara kufanya shughuli zao za kila siku na kupata faida kubwa” alisema
Pia, alisema mkoa una rasilimali watu ya kutosha na yenye uwezo mkubwa wa uzalishaji ambapo kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu imebainisha pato la mtu mmoja mmoja ni sh. milioni 2.8 kwa mwaka 2023.
“Tafsiri ya takwimu hizo ni kwamba hali ya umasikini kwa mkoa sio mbaya kutokana na wananchi wengi wanajishulisha na shughuli mbalimbali ikiwemo kilimo cha mazao ya biashara, chakula.” alisema
Pia, alisema kuna fursa kubwa katika eneo la uchumi wa buluu kutokana na uwpeo wa bahari ya Hindi huku uvuvi ukiwa umeajiri asilimia 80 ya wakazi wa mkoa huo huku asilimia tisa wakijishughulisha na shughuli za misitu ambazo nazo zimekuwa na faida kubwa.
“Jiji la Tanga ni halmashauri ambayo ni eneo sahihi la kufanya shughuli za kibiashara kutokana na uwepo wa bandari bora na yenye historia bora ya usafirishaji wa bidhaa kutokana ndani na nje ya nchi” alisema
Alisema uwepo wa uwanja wa ndege wa Tanga unaopokea ndege kila siku kutoka viwanja vya ndege mbalimbali ikiwemo cha Kimataifa cha Mwalimu Julius Nyerere, Kuilimanjaro na Abeid Amaan Karume cha Zanzibar ni wakati wawekezaji kuja kuwekeza.
“Huu ni wakati mwafaka wa kuchangamkia maeneo sita ya kiuwekezaji ikiwemo uanzishwaji wa viwanda na maeneo ya uwekezaji katika kilimo, viwanda vya usindikizaji mazao, viwanda vya biashara za kilimo, uwekezaji katika maliasili na uwekezaji katika shughuli za huduma.” alisisitiza
MKUU WA WILAYA
Mkuu wa Wilaya, Japhary Kubecha alisema Mkoa wa Tanga wenye jumla ya watu 2,617,597 kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, ni kati ya mikoa 31 ya Tanzania ambao umekuwa na kasi kubwa ya kiuchumi.
“Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia imekuwa mstari wa mbele kutekeleza miradi lukuki ya maendeleo mkoani humo na kuweka mazingira bora ya uwekezaji kwa wananchi.” alisema
Aliongeza; “Uwepo wa fursa hizo ni moja ya mambo yanayopaswa kuungwa mkono na kila mpenda maendeleo kujitokeza kwa wingi katika kongamano la uwekezaji Tanga ambalo linakwenda kuonyesha kwa vitendo dhana ya uwekezaji.”
Alisema Tanga ni mkoa muhimu ambayo kila mfanyabiashara au mwekezaji anapaswa kuchangamkia fursa kubwa zilizopo kutokana na uwepo wa rasilimali nyingi na za kutosha pamoja na usafiri wa reli, barabara, ndege na hata maji.
“Kuna kila aina fursa, tunawaita wawekezaji wa bandari kavu waje kwa wingi na maeneo mengi ya uwekezaji yapo, uanzishwaji wa viwanda na maeneo ya uwekezaji katika kilimo, viwanda vya usindikizaji mazao, viwanda vya biashara za kilimo, uwekezaji katika maliasili” alisema
Alisema;”Pia kuna fursa kubwa katika eneo la shughuli za utoaji huduma. Wafanyabiashara wengi wajitokeze kwa wingi katika kongamano la uwekezaji kwa kuwa dhamira kubwa tuliyokuwa nayo kuufungua mkoa wa Tanga kiuwekezaji”
Kwa mujibu wa Kubecha, kongamano hilo ambalo mgeni rasmi atakuwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dk. Batilda Burian linakwenda kuakisi kauli mbiu ya mkoa, hivyo Watanzania wanakaribishwa kushiriki katika kongamano la uwekezaji.