– waamua kuondoa kesi mahakamani na kukiri kuwa walikopa na wamekubali kulipa dola milioni 13.5 sawa na zaidi ya Shilingi Bilioni 35 walizokataa kulipa awali
– Ni za mkopo walioukopa kwa kampuni ya nje na kudhaminiwa na benki za Equity kenya na Tanzania kisha kukataa kuulipa
– Wakili wa chechefu aliwarubuni wakaenda Mahakama ya biashara kukataa kulipa, Jaji Magoiga akawapa ushindi wenye mashaka wa wao kutokulipa walichokopa
– Mahaka ya rufaa ikafutilia mbali hukumu ya magoiga na kuagiza kesi ianze upya mahakama ya biashara – Nilesh (Mmiliki STATE OIL) akaamua kuheshimu kanuni ya kukopa inayosema ‘DAWA YA DENI KULIPA’
– Akubaliana na benki kuondoa shauri alilolifungua akiahidi kulipa dola milioni 13.5 (wastani wa bilioni 35) kwa awamu mbili- awamu ya kwanza kabla ya tarehe 30 juni 2025 na awamu ya pili ni mwaka mmoja baadae ambapo kila awamu atalipa dola milioni 6.75
– Wakili wa Chechefu sasa atakiwa kujitafakari, kama anastahili kuendelea kujiita wakili msomi kwa vitendo vyake vya kuwarubuni wafanyabiashara waliokopa kukataa kulipa madeni kwa kukimbilia mahakamani ambako anajua fika dawa ya deni ni nini
– Jamvi la Habari, lapongezwa kusimamia ukweli
“Mwaka 2018 State Oil ilichukua mkopo wa Dola za Marekani 18.64 milioni kutoka kwa mkopeshaji wa nje, kampuni ya Lamar Commodity Trading DMMC of Dubai kwa udhamini wa Equity Bank Kenya.Ili kupata udhamini huo, State Oil pia iliweka dhamana zake kwa Equity Bank Kenya, chini ya usimamizi wa Equity Tanzania.Hata hivyo State Oil ama ilishindwa au ilipuuza kulipa mkopo huo kwa kampuni ya Lamar na hivyo mdhamini wake Equity Bank Kenya ikalazimika kuulipa, na hivyo yenyewe ndio ikabaki inaidai kampuni hiyo.”
Na. Mwandishi wetu,
DAWA YA DENI NI KULIPA ndivyo unavyoweza kusema ameamua kufanya Nilesh Kumar Suchak mmiliki wa kampuni ya mafuta ya State Oil baada ya kuamua kuachana na danadana za kukataa kulipa mkopo wa mabilioni ya fedha aliokopeshwa na benki za Equity kenya na Tanzania kwa kukimbilia mahakamani.
kampuni ya State Oil Tanzania Limited imekubali yaishe mahakamani kuhusiana na malipo ya mkopo wa Dola za Marekani 18.64 milioni (zaidi ya Sh47 bilioni) za Benki za Equity, Equity Bank Tanzania Limited (EBT) na Equity Bank Kenya (EBK) uliokuwa unabishaniwa.
Hii inatokana na uamuzi kampuni hiyo kuiondoa mahakamani kesi iliyokuwa imeifungua ikipinga malipo ya mkopo huo kwa madai kuwa haikuwahi kukopeshwa na benki hizo, badala yake imekubali kuzilipa benki hizo Dola za Marekani 13.5 milioni.
Kampuni hiyo awali ilifungua kesi Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara dhidi ya Benki hizo ikipinga kudaiwa pesa yoyote na benki hizo.Hata hivyo benki hizo pia zilifungua madai kinzani zikdai kuwa zinadia kampuni hiyo zaidi ya Dola za Marekani 26.47 milioni likia ni deni la mkopo ambao ziliipatia kampuni hiyo Novemba 21, 2018.
Mahakama Kuu katika uamuzi wake ilikubaliana na madai ya kampuini hiyo na kuipa ushindi ikieleza kuwa benki hizo hazikuwahi kuikopesha kiasi hicho cha fedha.
Benki hizo zilikata rufaa Mahakama ya Rufani zikipinga hukumu hiyo ya Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani katika uamuzi wake ilioutoa Mei 16, 2024 ilibatilisha hukumu hiyo ya Mahakama bila hata kusikiliza hoja za msingi za rufaa ya benki hizo.Uamuzi huo umetolewa na jopo la majaji watatu, Rehema Mkuye (Kiongozi wa joo), Abraham Mwampashi na Zainabu Muruke, Alhamisi, baada ya kubaini kasoro katika mwenendo wa kesi hiyo ya msingi.
Kasoro hiyo ilikuwa ni Mahakama Kuu kuendelea kusikiliza na kuamua kesi hiyo bila hati ya madai kufanyiwa marekebisho baada ya wadaiwa katika kesi ya msingi kuongezeka kutoka mmoja na kuwa wawili.
Mahakama hiyo imesema kuwa kasoro hiyo inavunja masharti ya lazima ya Amri ya 1 Kanuni ya 10 (4) ya Sheria ya Kanuni za Madai (CPC) na kwamba pia kumeathiri Mwenendo na vilevile hukumu iliyotokana na Mwenendo huo.
Hivyo Mahakama ya Rufani ilitengua hukumu hiyo na kurejesha kumbukumbu (jalada) za kesi ya kibiashara namba 105 ya mwaka 2020, Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara kwa ajili ya kesi kusikilizwa upya baada ya kukidhi matakwa ya Amri ya 1 Kanuni ya 10 (4) ya CPC.
Hata hivyo badala ya kuendelea na usikilizwaji upya kampuni hiyo imefanya majadiliano na benki hizo na kufikia makubaliano na benki hizo, ambapo sasa imekubali kudaiwa na benki hizo na imekubali kulipa kiasi cha Dola za Marekani 13.5 milioni ( sawa na zaidi ya ShMakubaliano hayo yamefikiwa na pande zote Agosti 16, 2024, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya hatua usuluhishi mbele ya Naibu Msajili Joyce Minde.
Majadiliano hayo baina ya wadaawa (pande zote mbili) yalifanyika mbele ya wakili wa kampuni hiyo Frank Mwalongo na mawakil wa benki hizo Mpaya Kamara na Tumaini Michael na wawakilishi wa kampuni hiyo, Nilesh Kumar Suchak na Anil Nilesh Suchak.Makubaliano hayo yamesajiliwa na kuwa amri ya mahakama hiyo ambayo inapaswa kutekelewa kulingana na makubaliano hayo.
Kwa mujibu wa amri hiyo ya mahakama ya Agosti 16, 2024, inayotokana na makubaliano hayo, State Oil imekubali kuzilipa benki hizo kiasi hicho cha fedha, Dola za Marekani 13.5 milioni kwa awamu mbili.Katika awamu ya kwanza imekubali kulipa kiasi cha Dola za Marekani 6,75 milioni zitalipwa Juni 30, 2025 au kabla ya tarehe hiyo na awali ya pili imekubali pia kulipa kiasi kama hicho Dola 6.75 mpaka kufikia au kabla ya Juni 30, 2026.
“Mdaiwa hata hivyo atakuwa huru kulipa kiasi chote kilichokubaliwa katika makubaliano hayo au sehemu yake wakati wowote hata mapema kabla ya muda uliopangwa kama ulivyoelezwa hapo juu,” inaeleza amri hiyo ya mahakama.
Vilevile mahakama hiyo katika amri yake hiyo imeamuru kuwa dhamana zilizokuwa zimewekwa na wadaiwa wa mkopo huo (state oili na wadhamini wake) zitaachiliwa na benki hizo baada ya kampuni hiyo kukamilisha malipo yote.
Pia mahakama hiyo imebainisha kuwa isipokuwa kama kutakuwa na ukiukwaji wa makubaliano hayo, malipo hayo yaliyobainishwa katika awamu hizo mbili hayatakuwa na riba au adhabu ndani ya muda wa malipo ulioanishwa.
Hata hivyo imesema kuwa kama kutakuwa na ukiukwaji wa makubaliano hayo wa namna yoyote katika ulipaji katika awamu hizo basi malipo hayo yatakuwa na riba na benki hizo zitakuwa huru kuchukua hatua zozote.
Hatua hizo ni pamoja na kupiga mnada mali zilizowekwa kama dhamana kufikia deni hilo au kuomba utekelezaji wa makubaliano hayo kwa namna ileile kama amri ya mahakama.Awali State Oil ilifungua kesi hiyo dhidi ya EBT, kama wakala wa EBK, kufuatia mgogoro wa malipo ya mkopo wa Dola za Marekani 18,640,000 ambazo EBK inaidai State Oil.
Makubaliano hayo ni ushindi kwa benki hizo na hii inakuwa ni kesi ya pili kwa benki hizo kushinda miongoni mwa kesi kadhaa zilizofunguliwa na kampuni mbalimbali zikipinga kulipa mikopo kutoka katika benki hizo huku kampuni zote hizo zikitetewa na wakili Frank Mwalongo
Historia ya mgogoro
Mwaka 2018 State Oil ilichukua mkopo wa Dola za Marekani 18.64 milioni kutoka kwa mkopeshaji wa nje, kampuni ya Lamar Commodity Trading DMMC of Dubai kwa udhamini wa Equity Bank Kenya.
Ili kupata udhamini huo, State Oil pia iliweka dhamana zake kwa Equity Bank Kenya, chini ya usimamizi wa Equity Tanzania.
Hata hivyo State Oil ama ilishindwa au ilipuuza kulipa mkopo huo kwa kampuni ya Lamar na hivyo mdhamini wake Equity Bank Kenya ikalazimika kuulipa, na hivyo yenyewe ndio ikabaki inaidai kampuni hiyo.
Baada ya muda iliopewa kulipa deni hilo kuisha bila kulipa Equity Bank Tanzania ilipoidai State Oil kwa niaba ya Equity Bank Kenya kama wakala wake aliyepewa dhamana hiyo, ndipo State Oil ilipokimbilia mahakamani.
Katika kesi hiyo kampuni hiyo iliiomba mahakama iiamuru Equity Bank Tanzania iirejeshee hati za mali ilizokuwa imeziweka dhamana, kwa ajili ya kupata udhamini kutoka kwa Equity Bank Kenya, huku ikidai kuwa haidaiwi na benki hizo.
Wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo miongoni mwa mashahidi hao walikuwa ni pamoja na mwakilishi wa kampuni ya Lamar iliyotoa mkopo huo ambayo ilieleza kuwa State Oil ilishindwa kulipa mkopo wake na badala yake mdhamini wake, Equity Bank Kenya ndo akaulipa.
Hata hivyo mahakama hiyo katika hukumu yake iliyotolewa na Jaji Stephen Magoiga Oktoba Mosi, 2021, alikubaliana na madai ya State Oil, kuwa ilikuwa imeshalipa deni lake lote na hivyo benki hizo hazikuwa na madai dhidi yake.
jaji Magoiga aliamuru hati za mali zote zilizokuwa zimewekwa dhamana na State Oil, zinashikiliwa zirejeshwe kwa kampuni hiyo, uamuzi ambao benki hizo hazikukubaliana nao ndipo zikakata rufaa Mahakama ya Rufani.