Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemuagiza Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Lazaro Kilahala, kuwasilisha Ofisini kwake orodha ya Taasisi zote za Serikali zinazodaiwa na Wakala huo ili aweze kuwaandikia baraua ya kusisitiza kulipa madeni yao.
Agizo hilo amelitoa leo, Agosti 20, 2024 jijini Arusha wakati akifungua kongamano la Tatu la madereva wa Serikali ambapo pamoja na mambo mengine amesisitiza Wakuu wa Taasisi kuhakikisha wanalipa madeni hayo mara moja ili TEMESA iweze kuhakikisha wajibu wa vyombo vya usafiri vinakuwa salama na vinatengenezwa kwa wakati.
“Wakuu wa Taasisi, popote mlipo mnanisikia, kama mpo hapa ndani au kupitia vyombo vya habari, hakikisheni mnalipa madeni yenu TEMESA, mkiwalipa hawa matengenezo ya magari yenu yatafanyika kwa muda sahihi” amesema Majaliwa.
Aidha, Waziri Mkuu Majaliwa ameipongeza TEMESA kwa kuwa na mitambo ya kisasa ya kutengeneza magari na kuwataka kuongeza ubunifu na uadilifu ili kuleta tija katika utengenezaji wa magari ya Serikali.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Majaliwa amewataka viongozi kuthamini kada ya madereva kwa kuwapa mahitaji yao ili wafanye kazi kwa ufanisi na hivyo kulinda usalama wa viongozi, wananchi na magari wanayoyaendesha.
Ameongeza kuwa Serikali inatambua, inaheshimu na kuthamini mchango wa madereva nchini na itaendelea kuzitafutia ufumbuzi changamoto za madereva ili kuikuza kada hiyo muhimu kwa maendeleo ya nchi.
Naye Naibu waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey Kasekenya amemhakikishia Waziri Mkuu kuwa Wizara itaendelea kusimamia na kukilea chama cha madereva ili kikue na kufanya kazi kwa weledi.
“Wizara itahakikisha madereva wanapata elimu stahiki ya magari wanayoyaendesha ili kuendelea na ukuaji wa teknolojia na kuwawezesha kushiriki vikao vyao ili kukuza weledi.
Zaidi ya madereva 1200 kutoka Tanzania bara na Zanzibar wanashiriki kongamano hilo linaloongozwa na kauli mbiu isemayo ” Dereva wa Serikali jitambue, timiza wajibu wako, usalama barabarani unaanza na wewe kazi iendelee”.