- Ni wa wafanyabiashara wanaokopa kukataa kulipa na kukimbilia mahakamani
- Mahakama ya Rufaa yairufaa yaipiga chini hotel ya Gold Crest iliyokopa mabilioni EXIM BANK na kukataa kulipa
- Majaji A.M Mwampashi,R.K Mkuye na Z.G. MURUKE wagoma kuitumia mahakama kama kichaka cha wajanja kukwepa kulipa madeni
- Ni dhahiri sasa dawa ya deni ni kulipa
- hukumu ya kesi kama hiyo baina ya kampuni ya NAS na benki ya Equity yasubiriwa kwa hamu
- waliopata ushindi mahakama ya biashara licha ya kukiri kukopeshwa bidhaa za mabilioni ya pesa na kukataa kulipa, sasa wahaha kujinasua na kitanzi cha hukumu ya majaji hao watatu wanaoonekana kulinda heshima ya mahakama
Na. Mwandishi wetu
Usemi wa DAWA YA DENI NI KULIPA , unaweza kuwa ndio tafsiri ya Mahakama inayoitoa dhidi ya makampuni na wafanyabiashara wakubwa waliokopa mabilioni ya pesa na kisha kukataa kulipa kwa kukimbilia mahakamani ambapo baadhi ya watumishi wa mahakama wasio na maadili walishiriki kubariki uchafu wao.
Hukumu kadhaa zilizotolewa na mahakama ya rufaa na mahakama kuu katika kipindi hiki ni kielelezo kwamba mahakama hiyo imekataa kutumika kama kichaka cha wakwepa kulipa madeni na badala yake kunyoosha haki kama lengo la uwepo wa mahakama Duniani linavyotaka
Itakumbukwa kwamba wiki kadhaa nyuma mahakama ya rufaa chini ya majaji watatu jaji Muruke, jaji Mwampashi na jaji Mkuye waliifutilia mbali hukumu ya kesi baina ya kampuni ya State Oil na benki za Equity kenya na Tanzania na kuelekeza kesi hiyo ianze upya kusikilizwa baada ya majaji hao kugundua kuwa uendeshaji wa kesi hiyo katika mahakama ya biashara haukufuata misingi ya haki na hivyo kuwepo na viashiria vya sintofahamu
Katika kesi hiyo kampuni ya State Oil ikiwakilishwa na wakili frank mwalongo iliiomba mahakama iiruhusu isilipe mabilioni ya pesa iliyokopa katika benki hizo na mahakama ilikubali na kuiamuru benki hiyo kutokulipwa na wadai wao, hukumu ambayo benki iliipinga mahakama ya rufaa.
Ni katika mfukulizo wa hukumu hizo ndipo pia kampuni ya ZAS investment imeamuliwa kulipa mabilioni ya shilingi iliyokopa kutoka benki za Equity kenya na Tanzania ambazo ilizitumia pamoja na mambo mengine lakini pia kulipa madeni katika benki nyingine walizokuwa wanadaiwa, mahakama kuu divisheni ya biashara ikaiamuru kampuni hiyo kulipa kiasi chote cha pesa ilichokopa na riba.
Kana mwamba haitoshi, hivi karibuni mahakama ya Rufaa tena chini ya majaji watatu Mkuye, Mwampashi, na Muruke imefuta hukumu ya mahakama kuu iliyoipa ushindi hotel ya Gold Crest ya mwanza dhidi ya benki ya EXIM katika kesi iliyofunguliwa miaka kadhaa nyuma
Kutokea kwa hukumu hizi ni kielelezo kuwa mahakama za Tanzania zinachafuliwa na baadhi ya watendaji wasio waaminifu ikiwemo baadhi ya majaji na sio kweli kwamba mfumo wote wa mahakama umeathirika
Akizungumzia hukumu hizi Shaaban Selemani mtaalam wa masuala ya fedha anasema kuwa kuna nyakati matukio fulani hutokea ili jamii itengeneze mfumo sahihi wa kuishi ambapo kama si kufanya hivyo mambo mengi yasingewezekana
“Mahakama ni sehemu ya haki, hivyo inatarajiwa mahakamani pawe mahala patakatifu mno, lakini hii haizuii mahala hapo kuwepo na watu wasio waaminifu ambao kimsingi wapo Dunia nzima, watu hawa wasio waaminifu ndio wanaweza kufumba macho na kupindisha haki wakizani wanajinufaisha kumbe wanauchafua muhimili muhimu wa kutoa haki nchink”. Amesema Shabani
Ameongeza kuwa sio jambo la kawaida kwa mahakama kukubaliana na maombi ya mkopaji anayekataa kulipa mkopo kwa visingizio visivyokuwa na kichwa wala miguu.
” unawezaje kusema haujakopa halafu huyo unayedai yajakukopesha umemkabidhi kisheria mali zako zinazohamishika na zisizohamishika, kama si uongo na kuipotezea muda mahakama ni nini?. jambo kama hili hata kama ukishinda mahakama ya chini wala usishangilie uahindi wako kwa sababu ushindi wako hautokani na haki”. Amesisitiza
Hukumu hiyo ya Exim inatoka huku kukisubiriwa kwa hamu kwa hukumu baina ya benki za Equity Kenya na Tanzania ambapo benki hizo zimekata rufaa iliyosikilizwa mbele ya majaji hao hao rufaa baina ya benki hizo na kampuni ya NAS HAULIERS ambayo kama ilivyo kampuni nyingine imekopeshwa mabilioni ya shilingi na imegoma kulipa ikitetewa na wakili yule yule wa kampuni zote zinazogoma kulipa na kuibuka na ushinzi katika mahakama kuu divisheni ya biashara ushindi ambao hadi sasa hakuna mtu yeyote mwenye akili timamu anaweza akauelezea umepatikanaje patikanaje
Gazeti litaendelea kuhabarisha umma kuhusiana na masuala haya hadi yatakapofika tamati