- Mabilioni yanayokopwa na ‘Matajiri Chechefu’ na kukataa kulipa madeni yatajwa kuathiri mifumo ya mizunguzo ya fedha katika jamii
- Kugoma kwao kurejesha mikopo kunasababisha mabenki kushindwa kuwakopesha wajasiriamali na wafanyabiashara wenye mitaji midogo na wenye uhitaji
- yabainika ni chanzo namba moja cha kushamiri kwa MIKOPO KAUSHA DAMU ambayo inaongoza kuwaumiza watanzania wa chini
- Wachumi, wanasheria wazidi kuichambua na athari zake
“Sio rahisi kwa ndoto za Rais Samia za kutaka mikopo ya riba chini ya asilimia 10. Haiwezekani kwa sababu matajiri wachache wanakopa pesa nyingi ambazo kama wangekuwa waaminifu na kuzirudisha basi wajasiriamali wengi wangekopeshwa na kuchagiza uchumi”. John Sembuyu, Mchumi
Na. Mwandiahi wetu,
Ndoto na matamanio ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya watanzania kukopeshwa mikopo nafuu yenye riba chini ya asilimia 10 ili waweze kujiimarisha kiuchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa inaelezwa kuwa ngumu kutokana na wafanyabiashara wachache kujitajirisha isivyo halali kupitia mikopo wanayokopa katika mabenki kadhaa ndani nan je ya nchi kisha kukataa kulipa na hivyo kuzifanya taasisi za fedha kujihami kwa kuweka riba kubwa ina masharti magumu ili kulinda mitaji yao kukwepa kinachoitwa MIKOPO CHECHEFU
Ni kutokana na sababu hii ya uwepo wa MIKOPO CHECHEFU ambayo wakopaji hukopa mabilioni ya pes ana kukataa kulipa kwa kutumia njia mbalimbali ikiwemo kukimbilia mahakamani na kushinda kesi kiujanja ujanja, ndipo sasa pamezaliwa aina mpya ya mikopo inayowatesa mamilioni ya watanzania maarufu kama MIKOPO KAUSHA DAMU inayozidi kushamiri kila kona nchini kila siku
Hii ni mikopo inayotajwa kuongoza kuwafilisi wananchi hasa wa vipato vya chini ikiwemo watumishi wa serikali na binafsi kutokana na riba kuwa kubwa inayotolewa kirahisi bila ya masharti mengi hivyo kuvutia watu wengi kuikimbilia ambapo unaweza ukakopa milioni moja ukalipa milioni kumi kama utani
Taarifa zinaonyesha kuwa urahisi wa upatikanaji wa mikopo hii ndio unaowaponza wakopaji ambapo mteja anaweza kujaza fomu saa nane mchana, dakika chache baadae akakopeshwa, na huku akiambiwa riba ni ndogo kumbe kila milioni moja anayochukua ina riba yake, kufika siku anatakiwa kulipa kuangalia anajikuta hawezi kulipa deni lote, na riba huanza kupanda kila mwezi
Uchunguzi unaonyesha kuwa ni kutokana na kushamiri kwa mikopo chechefu ndiko kunakopelekea kuongezeka kwa mikopo inayoumiza ambayo hufanywa na taasisi ama watu binafsi wanaokuwa kimbilio la wananchi wasio na uwezo wa kupenya kwenye mikopo rasmi ya kibenki
‘’kama tunaambiwa mfanyabiashara mmoja tu amekopa zaidi ya bilioni 100 na akakataa kulipa, huyo ni mmoja tu!, hebu jiulize ni wajasiliamali wangapi wa aina yangu na wenye mitaji isiyozidi milioni 5, au mama lishe wangapi au wamachinga wangapi wangeweza kukopeshwa hizo bilioni 100 zilizokaliwa na mtu mmoja bila huruma’’.? Ananukuliwa Joshua Mwaibage mfanyabiashara mdogo sokoni kariakoo
‘’unaona lile Guta pale? (anaonyesha pikipiki ya matairi matatu), unayaona yanavyopiga kazi?, na unaona vijana walivyoyachangamkia kubeba mizigo hapa Kariakoo kutumia maguta?, sasa yale yanauzwa milioni kama tano hivi, jiulize sasa bilioni 100 unaweza nunua mangapi kama yale na yangeweza kutoa ajira kiasi gani…muda mwingine hizi benki zipunguze kushobokea matajiri, sisi wapiganaji tupo huku na nakuhakikishia hakuna mtu angeweza kushindwa kurejesha mikopo ya maguta kama yale…maana mzigo wa kubeba upo kila siku’’. Aliongeza
‘’Hapo sijazungumzia bodaboda ambazo ni chini ya milioni 3 kila moja, kwa mabilioni hayo tungejiajiri watanzania wangapi, achana na hawa wauza madafu, wauza kahawa na watembeza bidhaa nyinginezo ambao mitaji yao haifiki hata laki tano…tungejiajiri wangapi?..kuna haja sasa ya serikali kuangalia upya vipaumbele vya namna ya ukopeshaji, bila hivyo tutaendelea kukimbilia KAUSHA DAMU tu hakuna namna nyingine’’. Amezidi kusisitiza
Naye John Sembuyu mchambuzi na mtaalam wa masuala ya Uchumi alipoombwa kutoa maoni yake kama kwa hali iliyo ya mikopo chechefu hali ikoje kwa matarajio ya serikali kutaka taasisi za fedha kukopesha chini ya riba ya asilimia 10 amesema ni ndoto kwa jambo hilo kutokea kwa mazingira ya sasa ikiwa jitihada mahsusi hazitachukuliwa kudhibiti hali hiyo
‘’uchumi wa kibenki una vipimo vyake, kadri kasi ya mikopo isiyolipika inavyozidi kuongezeka, ndivyo urahisi wa mabenki kukopesha unazidi kupungua, lazima benki zijihami kukwepa kuingia mtego wa BOT unaozuia kiwango cha mikopo isiyolipika kuvuka asilimia 5 ya mikopo yote, kwa mantiki hiyo lazima benki zikomae na riba kubwa na masharti magumu ili kujihakikishia usalama wa pesa zake’’ amesema
Gazeti hili limewahi kuandika kuhusu Utekelezaji wa tangazo la Gavana wa Benki kuu ya Tanzania la tarehe 13, mei mwaka huu la kuwataka watanzania kutoa taarifa kwa benki hiyo juu ya wafanyabiashara wanaojihusisha na kutoa mikopo bila kuwa na leseni za kufanya hivyo kama wanavyotakiwa na kifungu cha 17 cha sheria za huduma ndogo za fedha 2018 umekuwa mgumu kutokana na ukweli kuwa uwezo wa wananchi kuifikia benki hiyo na kuchambua kwa kutambua kama anayewakopesha ni taasisi iliyosajiliwa ama haijasajiliwa ni mdogo sana
Aidha, hali ya wananchi wengi wanaojikuta wanaingia na kuangukia kwenye taasisi zinazokopesha mikopo kwa riba kubwa haziwaruhusu hata kufikiria mara mbili kipindi wanataka kukopa kwani wengi wao hukimbilia kukopa kama chaguo la mwisho baada ya kukwama kwa majaribio yao mengi hasa kushindwa kukopeshwa benki
Taarifa za uchunguzi zinaonyesha kuwa sio wananchi wasio wafanya kazi tu ndio wanateseka na aina hii ya mikopo lakini pia hata watumishi wa serikali hasa wafanyakazi wapya wanaoanza maisha mapya kazini hukutana na aina hii ya mikopo kutokana kuwa na uhitaji mkubwa wa kupata fedha za kujikimu na kuanzishia maisha kabla ya kupokea mshahara na hivyo kujikuta wanaangukia mikononi mwa wakopeshaji hawa
Idadi ya vijana walioanza kazi na wanaoshuhudia kishahara yao inapita Kwenda kulipa mikopo hii ni kubwa na inasikitisha kwani kutokana na kukithiri kwa mikopo hii kunawafanya watumishi hao kukosa hamu ya kufanya kazi
‘’hata sisi wafanyakazi wa serikali tunapambana nayo mikopo ya namna hiyo, vijana wengi sana wanaoanza kazi wanateseka na mikopo hiyo, yupo kijana mmoja alikopa milioni 8, mpaka sasa amerejesha milioni 21 na bado mkopo haujaisha. Kwa kifupi ni hatari’’. Anasema mmoja wa wakopaji aliyeomba jina lake lihifadhiwe
‘’tamko tu la benki kuu ama Waziri kuwa watu watoe taarifa juu ya uwepo wa mikopo ama taaisi za hivi wala halitoshi, wakopaji hukimbilia huko baada ya kubanwa sana, serikali kupitia BOT lazima watafute suluhu ya uhakika hasa kupitia mabenki’’. Ameongeza
‘’lazima tujue ni kwanini kuna ugumu kwa mabenki kutoa mikopo yenye unafuu wa masharti kiasi cha watu kukimbilia KAUSHA DAMU, maana kama benki zingekuwa zinatoa mikopo bila shida nina hakika hii kausha damu isingekuwepo’’. Amesisitiza
Uzoefu unaonyesha kuwa mikopo ya KAUSHA DAMU ipo ya aina mbalimbali mingineyo ikihusisha hadi taasisi zilizosajiliwa kisheria lakini wanaweka vipengele vigumu katika mikataba yao hasa utata wa uchakataji wa rib ana hivyo kuwatesa wakopaji kulipa
Kadhalika, wiki kadhaa nyuma tuliripoti kuwa
Wakati serikali ikitumia mabilioni ya fedha kuwezesha mabenki kujiendesha inayoyamiliki kujiendesha kutokana na kukosa mitaji, dalili za fedha hizo kupotea ama kutafunwa na wajanja inaonekana wazi kama Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan hatachukua hatua za haraka kudhibiti michezo michafu ya upigaji wa fedha za mabenki hayo kupitia mikopo isiyolipika kwa makusudi
Taarifa zinaonyesha kuwa Serikali imepanga kuiwezesha Benji TCB (Tanzania Commecia Bank) mtaji wa zaidi ya shilingi bilioni 130 ili kuihuisha benki hiyo inayoundwa na mjumuiko wa benki kadhaa zilizofilisika kutokana na mikopo chechefu nchini
Miongoni mwa benki zilizofilisika na kuungwa pamoja kuunda TCB ni pamoja na benki ya wanawake, benki ya Posta, Twiga Bancorp na TIB Corporate ambazo kwa nyakati tofauti benki hizo zilifilisika pamoja na mambo mengine lakini pia mikopo chechefu ikitamalaki
Aidha serikali inaelezwa kuweka zaidi ya shilingi bilioni 100 kuhuisha mtaji wa benki ya uwekezaji TIB ili iendelee na biashara ambayo hadi sasa inasua sua kutokana na kuelekea kufilisika kwa mikopo chechefu ambayo hailipiki
mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere anasema Serikali inahitaji kuongeza mtaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) ili kukidhi matakwa ya mtaji kwa mdhibiti siri zimezidi kuvuja kuwa sababu ya benki hiyo kujikongoja ni uwepo wa Mikopo chechefu kwa wafanyabiashara wakubwa walioamua kuigeuza benki hiyo kuwa shamba la bibi kwa kukopa na kukataa kulipa
wakati wa makabidhiano ya ripoti ya mwaka wa fedha 2022/23 kwa Rais Samia Suluhu Hassan mjini Dodoma CAG alisema kuwa benki hiyo ina mtaji mdogo ikiwa na mtaji wa 88.12bn/- tu kinyume na matakwa ya 200bn/- kwa mujibu wa mwongozo wa benki na taasisi za fedha wa mwaka 2020. /21.
“Benki ya kilimo inakabiliwa na changamoto kubwa ya uhaba wa mtaji, hivyo kutoa wito kwa serikali kuendelea kuingiza pesa zaidi ili kuboresha mtaji wa wakopeshaji wa kilimo,” alisema Bw Kichere kwenye hafla hiyo.
Hata hivyo alisema anafahamu mipango ya serikali ya kuingiza 118.88bn/- ili kukuza mtaji wa wakopeshaji wa kilimo na kukidhi mahitaji ya mtaji. Katika maendeleo ya hivi karibuni mwezi uliopita, serikali ilipata mikataba ya mikopo ya kimataifa kufadhili sekta ya miundombinu na kilimo.
Katika utaratibu huu wa mikopo, sekta ya kilimo ilipata shilingi bilioni 166.4 ili kuongeza mtaji wa TADB unaolenga kugharamia shughuli za kilimo hivyo kuongeza uzalishaji, kuimarisha usalama wa chakula, kukuza biashara ya bidhaa zinazouzwa ndani na nje ya nchi pamoja na kuongeza ajira na kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja. , familia na taifa kwa ujumla.
Taarifa za uhakika ambazo gazeti hili linazo, zinaonyesha kuwa zaidi ya shilingi bilioni 100 za benki hiyo zipo kwa wafanyabiashara wachache waliogoma kulipa mikopo kwa sababu mbalimbali ikiwemo kukimbilia mahakamani kujificha
Miongoni mwa wafanyabiashara waliokopa kiasi kikubwa cha fedha katika benki hiyo ni pamoja na kampuni ya Global agency iliyochukua bilioni 26 kwa mradi wa shamba la kilimo mkoani kagera huku Chobo Investment ikichukua bilioni 12 bila kurudisha
Mwingine anayetajwa kukomba mabilioni ya shilingi katika benki hiyo ni kampuni ya Kahama oil millers (KOMU) ambayo imechukua zaidi ya shilingi bilioni 40 na hadi sasa haijulikani itarejeshaje kiasi hicho cha pesa
Kukithiri kwa mikopo chechefu sio tu kunayaathiri mabenki yanayotoa mikopo hiyo bali pia hupeleka athari za moja kwa moja kwa Watanzania ambao wanategemea mikopo ishuke riba ili na wao wakope
‘’miongoni mwa sababu za kisayansi za riba kuwa zaidi ya asilimia 18 ni wastani wa mikopo chechefu, mikopo mingi inayoshindwa kurejeshwa inayatia mabenki hasara kubwa na kwa bahati mbaya wengi wanaoshindwa kurejesha ni wafanyabiashara wakubwa ambao hukopa mabilioni, hivyo ili benki kujilinda na hasara hizo huweka riba kubwa kufidia mapengo hayo’’ anasema CPA Crispin Peter, mtaalam wa masuala ya fedha
Anaongeza kuwa ni vyema serikali iendelee kuweka kanuni ngumu zinazosimamia urejeshwaji wa mikopo ili kutokuruhusu wanyonge wengi wanaotaka kukopa kujiimarisha kibiashara kukutana na vikwazo ambavyo ki msingi hawastahili kukutana navyo
‘’wafanyabiashara wakubwa wakikopa wanakopa kweli, imagine mtu amekopa bilioni 40, halafu amekataa kulipa na akibanwa anakimbilia mahakamani, bilioni 40 ukisema uwakopeshe mama lishe, au bodaboda, au vijana tu wa biashara za mtaji mdogo ungekopesha watu wangapi?, mkopo huo ungezalisha ajira ngapi?, mapato kiasi gani yangekusanywa?, lakini wapi, anachukua mfanyabiashara mmoja, anakwenda kununua V8 anatamba nazo mjini na akipita tunamuamkia ukifika wakati wa kulipa anakimbilia mahakamani’’. Aliongeza Crispin